JAMII ya wafugaji imetakiwa kutumia juhudi zao binafsi kubadilisha
mawazo na imani ya jamii, kwamba mila na desturi hazibadiliki ili
kutengeneza mfumo bora mpya unaothamini maisha ya wanawake.
Mwito huo umetolewa na Mtaalamu wa masuala ya vyombo vya habari vya
kijamii na Mkufunzi, Rose Haji wakati akiwasilisha mada kwenye kongamano
la viongozi wa mila wa kabila la Wamasai (Laigwanani) na wanawake
mashuhuri yenye lengo la kushawishi uondoaji wa mila potofu
zinazorudisha nyuma maendeleo katika jamii za wafugaji.
Aliwataka washiriki wa warsha kusimama kidete na kutumia elimu
waliyoipata katika kushawishi jamii kubadilika na kuachana na mila za
ukeketaji, ndoa za utotoni na pia unyanyasaji mwingine wa kijinsia
unaoonesha ubabe wa wanaume na mfumo dume.
Aliwataka wanajamii hao kutumia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya
habari, rediojamii, vikao mbalimbali vya kata na vijiji pamoja na nyumba
za ibada kuhimiza watu kubadilika na kuacha mila hizo za ukeketaji na
kuozesha watoto katika umri mdogo.
Aidha Haji katika kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Elimu,
Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) amewataka wanawake
kuvunja ukimya na kuacha woga na kuibua vitu vinavyowanyima haki zao za
msingi.
Aliwataka wanawake kujitambua ili kutumia sheria zinazowalinda
kuondokana na unyanyasaji pamoja na ukatili wa kijinsia unaoendelea
katika jamii za kifugaji na kuwaomba viongozi wa mila washiriki katika
kuondoa mfumo dume.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro,
Benezeth Bwikizo, alisema kama watu watajitokeza na kueleza ukweli
serikali itachukua hatua hasa ya kulinda wanawake na watoto kupitia
mamlaka iliyokabidhiwa na Katiba ya nchi.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, KatibuTawala wa Wilaya
ya Ngorongoro, Lemuel Kileo, amelishukuru Shirika la UNESCO kwa
kuendesha mafunzo hayo ya kutoa elimu na kujenga uwezo kwa viongozi wa
mila na wanawake mashuhuri ili kuondoa mila potofu katika jamii ikiwemo
ukeketaji, mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Sunday, 15 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment