WAKATI Rais John Magufuli akieleza kusikitishwa na vitendo vya kitoto
vilivyofanywa bungeni na Kambi ya Upinzani jana, Spika wa Bunge, Job
Ndugai amewataka wabunge wasimfanye awe Spika mbabe.
Akizungumza baada ya Dk Magufuli kumaliza kutoa hotuba yake, Ndugai
alisema amesikitishwa na tukio lililofanywa na wabunge wa upinzani na
kuahidi kwamba halitajirudia siku za usoni.
“Naomba niwapelekee ujumbe rafiki zangu waliotoka kwamba nyie ndiyo
mnaweza kunifanya niwe Spika mpole, lakini pia mnaweza kunijenga nikawa
Spika mbabe. Vitendo hivi naomba visijirudie, leo iwe mwisho,” alisema
Spika Ndugai na kufafanua kwamba amevumilia leo kutokana na ugeni mzito
uliohudhuria.
Ugeni huo ni pamoja na marais wastaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi wa
Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu, Jakaya Kikwete wa Awamu
ya Nne, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, mawaziri wakuu
wastaafu, maspika wastaafu, mabalozi na viongozi wengine.
Awali katika hotuba yake, Dk Magufuli alisema kilichofanywa na
wabunge hao si kitendo cha kiungwana na ni aibu na utoto kwa hadhi ya
Bunge. Aliwaeleza wabunge kwamba wote ni kitu kimoja na kuwa lugha za
vijembe, mipasho, ushabiki wa vyama visiwe na nafasi katika Bunge hilo
na kuwataka wazungumze masuala yao na si kwa njia ya kuzomea au kutoka
nje kwani mambo hayo yanaaibisha Bunge.
Dk Magufuli aliyetumia muda wa saa 1:38 akianza kuhutubia saa tisa na
dakika 52 alasiri hadi saa 11 na nusu jioni, alisema kazi iliyo mbele
ya wabunge ni kubwa katika kuwatumikia Watanzania.
Alimpongeza Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) kwa
kuonesha ukomavu wa kisiasa na kusema kuwa hivyo ndivyo inavyotakiwa
mwanasiasa awe.
Jana wabunge wa kambi ya upinzani kutoka vyama vya CUF, Chadema na
NCCR Mageuzi walitolewa nje na Spika Ndugai baada ya kukaidi amri yake
ya kuwataka wakae muda mfupi baada ya Rais kuingia ukumbini. Wabunge hao
walianza kwa kuimba huku wakipiga meza na kusema:
“Maalim Seif… Maalim Seif...(Katibu Mkuu wa CUF na mgombea urais wa
Zanzibar),” walitoa kauli hiyo baada ya kutolewa tangazo bungeni la
kuwasili wageni mbalimbali ndani ya ukumbi huo.
Tukio hilo la fedheha lilianza saa tisa na nusu wakati Spika wa
Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alipokuwa anaingia ukumbi
hapo, pia dakika tatu baadaye lilijirudia wakati anaingia Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
Lakini hali ilionekana kuzidi wakati alipoingia Rais wa Zanzibar, Dk
Ali Mohammed Shein saa tisa na dakika 40, wakipiga meza na kumtaja
Maalim Seif na hata alipoingia Dk Magufuli saa tisa na dakika 45
waliendelea kuimba kwa staili hiyo hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai alitamka mara tatu wabunge hao
wakae chini na wawe watulivu, lakini walikaidi amri hiyo hivyo kuwataka
watoke nje kwa hiari yao.
Pengine kwa kuhofia askari wa aina tofauti waliokuwepo nje na ndani
ya ukumbi, wabunge hao bila kushurutishwa walitoka nje ya ukumbi na
baadaye walitolewa kabisa nje ya viwanja vya Bunge.
Awali Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alianza kwa kuomba
Muongozo wa Spika muda mfupi baada ya Bunge kutengua kanuni ya
kuwaingiza ukumbini viongozi ambao kikatiba hawatajwi kuingia katika
eneo hilo. Lissu alisema ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar inasema
Rais wa Zanzibar ataachia wadhifa huo miaka mitano baada ya kuapishwa na
kwamba Dk Shein aliapishwa Novemba 3, 2010 hivyo muda wake kikatiba
ulimalizika Novemba 2 mwaka huu.
Akijibu muongozo huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema Tundu
Lissu alisoma ibara ya 28 (2), lakini ibara ya 28(1) inasema Rais wa
Zanzibar ataendelea kushika wadhifa huo hadi Rais mpya atakapoapa na
kueleza kuwa Dk Shein ni Rais halali wa Zanzibar kikatiba.
Created by Gazeti la HabariLeo
Saturday, 21 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment