* Wapigwa marufuku kula, kunywa wakati wa kuaga
*Lowassa, Mbowe na Sumaye kuongoza waombolezaji
NA BENJAMIN MASESE, MWANZA
HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela imetoa saa tano kwa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutumia Uwanja wa Furahisha kwa ajili ya
kuaga mwili wa marehemu Alphonce Mawazo, kutokana na mlipuko wa ugonjwa
wa kipindupindu.
Akitoa ratiba mpya ya kuaga mwili wa Mawazo, aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Geita mjini hapa
jana, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu, alisema shughuli
hiyo itafanyika katika uwanja huo na kuhudhuriwa na wabunge wa vyama
vinavyoundwa Ukawa na watajitahidi kuzingatia maelekezo hayo ili watoe
heshima zote zinazostahili.
Pia alisema shughuli hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho
Taifa, Freeman Mbowe na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na
Frederick Sumaye.
“Kiongozi mkuu atakayeongoza shughuli za kuaga mwili wa Mawazo
atakuwa Mbowe, lakini katika shughuli hiyo kutakuwa na viongozi wa
kitaifa ambao ni aliyekuwa mgombea nafasi ya urais kupitia Chadema,
Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, wabunge wa
Ukawa na watu wengine maarufu.
“Sasa kutokana na kupewa saa tano za kutumia uwanja huo, tutakuwa na
makundi maalumu ya watu katika kupewa nafasi ya kuzungumza ili
kuwawakilisha wengine, tunaomba wananchi watakaohudhuria pale waepuka
kula chakula ovyo au kunywa, isije ikatokea mmoja akatapika, kuugua
tumbo wakasingizia mkusanyiko wetu.
“Tambueni tulikuwa tumepewa saa tatu, ikabidi tuzungumze na
Mkurugenzi wa Ilemela, John Wanga, ili kuongeza muda, natumia nafasi hii
kuwataarifu Watanzania kwa ujumla kuwa Mawazo ataagwa kwa awamu nne,
tunaaga hapa Mwanza kama kitaifa, kisha Geita Mjini sehemu ya mkoa
aliokuwa akiongoza.
“Pia tutaaga Katoro kama sehemu ya Jimbo la Busanda alilogombea
ubunge na mwisho atazikwa kijijini kwao Chikobe Jumatatu ya Novemba 30,
mwaka huu, ambapo wananchi wa pale watapewa nafasi ya kumuaga,” alisema
Mwalimu.
Kwa mujibu wa ratiba aliyoisoma, inaonyesha mwili wa Mawazo
utaondolewa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza leo kati ya saa
2:30 – 3:00 asubuhi na kupelekwa nyumbani kwa Mchungaji Charles Lugiko,
ambaye ni baba yake mdogo eneo la Nyagezi-Sweya na utaagwa kwa taratibu
za mila na desturi.
Pia ratiba hiyo iliyonyesha kuwa kati ya saa tano asubuhi hadi saa
sita mchana, mwili wa Mawazo utakuwa njiani kuelekea Uwanja wa Furahisha
kwa ajili ya kuagwa kitaifa na inakadiriwa kufanyika kuanzia saa 6:30
hadi saa 8:00 mchana kabla ya kuanza safari ya kwenda Geita Mjini na
waombolezaji watalazimika kulala hapo.
Ratiba hiyo inaendelea kuonyesha kuwa kesho asubuhi mwili wa Mawazo
utaagwa tena Geita Mjini katika Uwanja wa Magereza, kabla ya
kusafirishwa hadi Katoro ambako utaagwa tena kama sehemu ya jimbo lake
na baadaye kuupeleka kijijini kwao Chikobe na mazishi keshokutwa
asubuhi.
Katika hatua nyingine, Mwalimu alitoa shukrani kwa Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, kupokea hukumu bila kinyongo na kuahidi
kutoa ushirikiano katika ulinzi wakati wa shughuli za kuaga na
kusafirisha mwili huo.
Alisema tayari baadhi ya viongozi wa Chadema wametangulia mkoani
Geita kwa ajili ya kuonana na polisi ili kupanga namna ya kufanikisha
shughuli hiyo.
Mawazo aliuawa Novemba 14, mwaka huu mkoani Geita na watu
wasiojulikana baada ya kumvamia akiwa njiani na kumkata kwa mapanga na
shoka na kusababisha kifo chake.
Created by Gazeti la Mwananchi.
Saturday, 28 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment