Meneja Uhusiano wa Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud
MMOJA wa majeruhi watano waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Kahama kutokana na kufukiwa na kifusi cha mchanga na kukaa
siku 41 chini ya mgodi na kuokolewa, Onyiwa Kaiwao (55) amefariki dunia.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga,
Joseph Ngowi amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema kuwa chanzo
cha mauti hayo ni kutokana na majeruhi huyo kutapika akiwa amelala hali
ambayo ilifanya matapishi hayo kuingia katika njia ya hewa.
Dk Ngowi alisema Kaiwao alifariki jana saa sita mchana na kuongeza
kuwa pia alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa nimonia unaosababishwa
baridi kali hali iliyomfanya kutokuwa katika hali ya kawaida tofauti na
wenzake.
Hata hivyo, Dk Ngowi alisema majeruhi huyo pia alikuwa na matatizo
katika utumbo, na hivyo kila akienda haja kubwa alikuwa akitoa magome ya
miti waliyokuwa wakiyatumia kama chakula wakati wakiwa chini ya ardhi.
“Jana (juzi) tuliwachukua vipimo waathirika wote watano na kuonesha
kuwa hali zao ni nzuri, lakini Onyiwa alionesha kutokuwa na maendeleo
mazuri tofauti na wenzake na ghafla akiwa amelala alijitapikia hali
ambayo matapishi hayo yaliingia katika mirija ya hewa na kuziba hali
iliyosababisha kifo chake,” alisema Dk Ngowi.
Alisema hali za majeruhi wengine wanne zinaendelea vizuri, na
wanaendelea na mazoezi huku wakila wenyewe hali ambayo wamepanga kesho
kuangalia uwezekano wa kuwafanyia vipimo kwa mara nyingine tena.
Aidha, Dk Ngowi alisema endapo hali zao hazitakuwa nzuri na
kubadilika, watawahamishia katika Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya
uangalizi wa juu hali ambayo watapata mabadiliko zaidi ya afya zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shigitwa (SHIGOMIKO), Hamza
Tandiko alisema wakiwa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Nyangalata
wamekipokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwenzao na kuwataka
waliobaki kutokata tamaa Mungu atawasaidia watapata nafuu.
“Sisi kama wachimbaji hatupingani na Mwenyezi Mungu tulijitahidi
kadri ya uwezo wetu kuokoa maisha yao kwa kushirikiana na uongozi wa
Hospitali ya Wilaya, lakini kwa mapenzi ya Mungu ameamua kumchukua
Onyiwa akapumzike na hakuna mtu anaweza kuzuia kifo,” alisema Tandiko.
Wachimbaji hao wadogo watano waliokolewa kutoka katika mgodi huo wiki
iliyopita baada ya kukaa kwa siku 41 kutokana na kufukiwa na kifusi.
Mwenzao mmoja alifia mgodini wakati wakisubiri majaliwa ya kuokolewa.
Created by gazeti La HabariLeo.
Sunday, 22 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment