Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
UTARATIBU wa kugota madaraka ya urais; Rais anapokuwa madarakani kwa
vipindi viwili vya miaka mitano mitano ni suala la Kikatiba kwa mujibu
wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na
marekebisho yake kadhaa.
Ni kutokana na matakwa hayo ya Kikatiba ndio maana Novemba 5, mwaka
huu; Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alilazimika kuachia
madaraka ya urais kwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu;
kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli aliyeshinda kwa
asilimia zaidi ya 58.
Rais mstaafu Kikwete siku hiyo alikagua gwaride lililojipanga kwa
aina ya Omega ikiwa ni herufi ya mwisho ya Kigiriki ikimaanisha mwisho
wa utawala wake; Rais Magufuli yeye alikagua gwaride lenye herufi Alpha;
herufi ya kwanza ya Kigiriki yenye maana ya mwanzo wa utawala wake.
Kwa miongo mingi sasa tangu utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Nyerere mpaka hivi karibuni kwa Kikwete, tumekuwa tukishuhudia kupokewa
kwa shangwe kwa marais wapya, huku baadhi ya Watanzania wakitoa maneno
yasiyo na busara kwa marais wanaoondoka madarakani.
Tabia ya wanaobeza
Sababu mbalimbali zinatajwa kuwa chanzo cha kuanza kushamiri kwa
dhana hiyo potofu na inayopaswa kupigwa vita kwa nguvu zote na
Watanzania wote kwa vile haileti ustawi mzuri na afya kwa Taifa letu
lililojengwa kwa misingi ya kuheshimiana, kuvumiliana na kupendana.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema wanasiasa uchwara wa
upinzani, wanasiasa majeruhi wa uongozi wa Rais anayeondoka madarakani
ndani ya chama tawala na hasa wale waliopata nafasi na kushindwa
kuitumia kwa misingi ya maadili na hivyo kuondolewa katika nyadhifa zao,
ni miongoni mwa watu wanaoendekeza tabia hiyo ya kubeza marais
wanaoondoka madarakani.
Mbali ya wanasiasa, watendaji ndani ya vyombo vya habari wanaochagua
upande na baadaye upande wao kushindwa katika uchaguzi, nao wamekuwa
mstari wa mbele katika kubeza na kuwashambulia marais wanapoondoka
madarakani, kwa kushindwa kuona mazuri yaliyofanywa na badala yake
kujenga hoja zao kwa masuala yasiyo na tija kwa mustakabali wa Taifa na
Watanzania, kama njia ya kulipiza kisasi.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa nchini wanakosoa hatua hiyo ya kutoa
maneno yasiyo na heshima kwa marais wanaoondoka madarakani; wakisema si
kweli kwamba kwa kipindi cha miaka 10 wanayokuwepo madarakani, viongozi
hao wanakuwa hawajafanya mambo makubwa kwa maendeleo ya kijamii na
kiuchumi nchini.
Baba wa Taifa
Baada ya kung’atuka mwaka 1985; baadhi ya Watanzania wasio na
uzalendo na nchi na viongozi wa kitaifa walibeza baadhi ya sera za Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wakisema zimechangia kuchelewesha
maendeleo ya Watanzania, bila kuzingatia kazi kubwa iliyofanywa na
muasisi huyo wa Taifa ya kuwaunganisha Watanzania kutoka kwenye ukoloni.
Mathalani wakati watu hao wakiangazia zaidi masuala la sera kama za
Uhujumu Uchumi na sera za Ujamaa na Kujitegemea kubeza masuala muhimu na
nyeti yaliyofanywa na Rais Nyerere na serikali yake kwa Watanzania;
hawakuangalia upande wa pili wa shilingi kwamba sera hizo ndizo
zilizowezesha kujenga maadili kwa viongozi wa umma; kuleta umoja wa
kitaifa; kujenga utu na kupiga vita ubaguzi wa aina zote kuanzia ule wa
makabila, dini, rangi na hata ukanda.
Mzee Mwinyi
Tabia kama hiyo ya kukejeli viongozi wanaoondoka madarakani
iliendelea kushamiri wakati Rais wa Awamu ya Pili; Ali Hassan Mwinyi
alipoondoka madarakani mwaka 1995, ambapo baadhi ya Watanzania
walimshangilia Rais mpya wa Awamu ya Tatu; Benjamin Mkapa huku wakimbeza
Rais mstaafu Mwinyi kwamba hakuiletea maendeleo nchi.
Watu hao katika kujenga hoja zao waliegemea zaidi kwenye kasoro ndogo
ndogo kama za kuruhusu uchumi huria na kusuasua kwa makusanyo ya
Serikali, kama kigezo cha kuishambulia Serikali ya Mwinyi; bila
kuangalia upande wa pili wa kazi kubwa iliyoasisiwa na kiongozi huyo
hasa katika kuanzisha mchakato wa uchumi kuondoka mikononi mwa Serikali
na kuanza kumilikiwa na watu au sekta binafsi.
Ni wakati wa utawala wa Rais Mwinyi ndipo dhana maarufu ya ruksa
ilipoibuka na kupata umaarufu. Rais mstaafu Mwinyi alijenga serikali
yake kwa dira na mwelekeo wa kuruhusu watu binafsi kuanza kumiliki njia
kuu za uchumi na ni wakati huo ambapo ilianza kuzoeleka kuona mtu
binafsi akiwa na lundo la fedha mfukoni tofauti na wakati wa Mwalimu
Nyerere ambapo hatua hiyo ingehesabika kama uhujumu uchumi.
Mzee Mkapa
Alipoingia madarakani; Rais wa Awamu ya Tatu; Benjamin Mkapa
alipokelewa kwa shangwe kutokana na azma yake ya kuanza kurekebisha
utendaji serikalini, kusimamia uwajibikaji na makusanyo ya Serikali na
kurejesha heshima ya utendaji katika sekta ya umma.
Lakini kwa namna ile ile watu wasio na mapenzi mema na ambao ni
kawaida yao kuwabeza marais walimshambulia kiongozi huyo alipoondoka
madarakani mwaka 2005, kwamba serikali yake haikufanya lolote.
Walitumia hoja za kushamiri kwa ujambazi, kubinafsishwa kwa mashirika
ya umma, kuzipa nguvu hoja zao bila kuangalia kazi kubwa iliyofanyika
katika kuleta maendeleo ya kitaifa na hasa kazi kubwa ya kuifanya
serikali sasa kubakia na usimamizi wa ulinzi na usalama na kuachia rasmi
masuala ya biashara kwa sekta binafsi na kudhibiti rushwa na ufisadi.
Wakati wakimbeza Rais mstaafu Mkapa, watu hao walimshangilia Rais mpya
wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye naye alipoingia alichukua hatua
mbalimbali katika kupambanua dira na mwelekeo wa serikali yake.
Mzee Kikwete
Rais mstaafu Kikwete alifanya kazi kubwa katika kusimamia ujenzi wa
miundombinu, kukuza demokrasia, kukuza utawala bora, kukuza uhuru wa
mawazo na hata uhuru wa vyombo vya habari. Ni kutokana na hili ndio
maana watu walianza kuelekeza lawama kwake kwamba alikuwa mpole na
kwamba hatua yake ya kuruhusu uhuru wa watu, ilikuwa ni chanzo cha
viongozi wengi kutumia mwanya huo vibaya na hivyo kuifanya serikali yake
kukumbana na misukosuko, iliyosababisha mara kadhaa serikali yake
kubadilika kwa viongozi kukiuka misingi ya maadili ya utumishi wa umma.
Hata hivyo, wakati baadhi ya waathirika wa serikali ya Rais mstaafu
Kikwete wakibeza hayo, ripoti mbalimbali zinamtaja Rais Kikwete kuwa
kiongozi wa mfano barani Afrika kwa kukuza uhuru wa mawazo, uhuru wa
vyombo vya habari, kupambana na rushwa, kujenga usawa wa kijinsia katika
vyombo vya uamuzi, kuboresha utawala bora, kukuza demokrasia ya vyama
vingi na mambo mengine mengi.
Hata hivyo, pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na Rais mstaafu Kikwete,
baadhi ya watu walioathiriwa na utendaji wake wamegeuka kuwa wakosoaji
nambari moja wa uongozi wake na baadhi yao wakibeza masuala yote
yaliyofanywa naye katika kuliletea maendeleo Taifa letu, jambo ambalo
wadadisi wa masuala ya kisiasa wanalikemea na kulipinga vikali.
Maoni ya wadadisi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Banna,
anakosoa mtindo huo na kusema kama Taifa ni lazima tupige vita kasoro
hiyo anayosema inawapunguzia heshima viongozi wastaafu na kutia doa
Tanzania kwenye Jumuiya ya Kimataifa. Profesa Banna anasema ni kutokana
na tabia kama hiyo ndio maana Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake
aliwahi kuwakosoa wanasiasa na watu wengine kutoka katika makundi ya
kijamii, aliposema kwamba utawala wa rais unapofikia kikomo, wamekuwa
wakiacha mambo mazuri yaliyofanywa na kiongozi mstaafu na badala yake
kuchukua mambo mabaya tu.
“Hili kama Taifa ni lazima tulipige vita. Leo wapo watu wanakosoa
uongozi wa Rais mstaafu Kikwete lakini ukiwafuatilia utagundua nyuma ya
hoja hizo kuna shinikizo kutoka kwa wanasiasa wa upinzani, ama wanasiasa
wa chama tawala walioanguka wakati wa uongozi wa Kikwete au ni wana
habari waliochagua upande na kuaminisha kuwa upande wao ungeshinda
urais,” anasema Profesa Banna.
Anasema hatua ya Tanzania kuaminiwa na mataifa mbalimbali na
mashirika makubwa, ikiwemo Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) na
hivyo kupewa misaada isiyo na masharti yoyote, huku mataifa mengine ya
Dunia ya Tatu yakishindwa kunufaika na misaada hiyo ni kielelezo ya
uongozi uliotukuka wa Rais mstaafu Kikwete katika taifa hili. Profesa
Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema kazi kubwa
iliyofanywa na Rais mstaafu Kikwete katika kukuza uchumi wa Taifa
kufikia asilimia saba ya sasa na kuijengea mazingira mazuri nchi
kuelekea kwenye uchumi wa kati ifikapo na pengine kabla ya 2025, ni
uthibitisho kwamba wanaomchafua hawana hoja.
“Hata kama waliathirika na uongozi wake basi si lazima wambeze wakati
Watanzania wote ni mashahidi na wanajua kazi kubwa iliyofanywa na Rais
mstaafu. Kwa wapinzani ipo wazi ni hasira za kushindwa Uchaguzi Mkuu.
Lakini pia kwa baadhi ya wanaCCM ni wazi ni kutokana na kubanwa na
uongozi wake.
“Kama unavyojua Kikwete alibadili karibu mawaziri wake wote kutokana
na kashfa mbalimbali kama Richmond, Escrow, Operesheni Tokomeza
Ujangili, Ufisadi wa Maliasili na nyinginezo. “Hawa walioondolewa wana
hasira na wanambeza Rais mstaafu lakini ukweli unabakia kuwa amefanya
kazi nzuri na ni vema tuchukue hatua kama Taifa kukomesha suala hili
ikiwezekana kwa kuanzisha mjadala wa kitaifa wa kupinga mtindo huu
usiendelee,” anasema Semboja.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Sunday, 15 November 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment