Saturday, 14 November 2015

Tagged Under:

Makinda ang’atuka uongozi wa kisiasa

By: Unknown On: 09:26
  • Share The Gag

  • Spika wa wa zamani wa Bunge, Anne Makinda.      
    SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake, Anne Makinda ameamua kung’atuka uongozi wa kisiasa baada ya kutumikia nafasi hizo kwa miaka 40.
    Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Makinda amesema ataendelea kuwa mwanasiasa na atakuwa tayari kutoa ushauri kwa watakaoendesha shughuli hizo wakipenda, ili kuendelea kujenga demokrasia.
    Kwa mujibu wa Makinda, sehemu kubwa ya maisha yake, amefanya kazi za kisiasa ndani ya Bunge na Oktoba mwaka huu alitimiza miaka 40 ndani ya siasa baada ya kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Waziri wa Shughuli za Bunge, Mwenyekiti wa Bunge na nyinginezo.
    Amesema hata angekuwa mtumishi wa umma, angekuwa amestaafu hivyo ni vizuri kuachia wengine waendeshe shughuli hizo, kwani hata viongozi wengine wa kisiasa wa umri wake, wamestaafu akiwemo Rais Jakaya Kikwete ambaye ni rika lake naye amestaafu.
    *Kazi zake
    Akizungumzia kazi alizosimamia katika uongozi wa Bunge la 10, Makinda alisema wamefanya mabadiliko mengi, ikiwemo kujifunza kufanya kazi na vijana waliosaidia kukuza demokrasia, jambo lililosababisha katika uwasilishaji wa taarifa za kamati mawaziri wengi wawajibike.
    Alisema suala la kuondoka kwa mawaziri au Serikali kuwajibika, halikuwahi kujitokeza kama wakati wa Bunge la Kumi, ikiwemo kubadili mzunguko wa bajeti ambao umewezesha majadiliano ya wabunge, kubadili bajeti na kuweka vipaumbele vya wabunge pamoja na kuwepo kwa Sheria ya Bajeti ambayo haikuwahi kuwepo nchini.
    “Lakini pia Bunge letu tumeliandaa kuwa na E-Parliament (Mfumo wa Bunge Mtandao), ambapo kuanzia Januari kila mbunge anatarajia kuwa na tablets (aina ya kompyuta mpakato) mezani kwake, ili kupunguza makaratasi kwa wabunge,” alisema.
    Mbali na kuboresha shughuli hizo za Bunge, Makinda alisema katika maslahi ya wabunge, wamehakikisha wabunge wanatibiwa pale pale kwa kwa kutumia bima. Katika muundo, alisema wameubadili ambapo sasa Katibu wa Bunge ana naibu watatu, wa kwanza anayejishughulisha na Bunge, wa pili uendeshaji na wa tatu huduma za Bunge pamoja na idadi ya watumishi wa Bunge kuongezeka kutoka 260 hadi 500.
    Alisema pia wameandaa ofisi za wabunge mkoani Dodoma katika Jengo la Mfuko wa Hifadhi wa LAPF pamoja na ofisi za kamati. Kazi zingine walizofanya ni pamoja na kuandika Kanuni za Bunge na kuzifanyia mabadiliko ya mara kwa mara ambayo alisema Bunge la 11, lina uwezo wa kuendelea kuboresha zaidi.
    Amesema katika uongozi wake, hakukuwa na changamoto kubwa bali wabunge walikuwa wachangamfu waliofanya hata yeye kujua kanuni kwa kupitia mambo mbalimbali na kwamba lilikuwa Bunge zuri.
    *Maoni Spika ajaye
    Akizungumzia waliojitokeza kuania nafasi ya uspika, akiwemo Spika mstaafu Samuel Sitta na aliyekuwa Naibu wake, Job Ndugai, Makinda alisema wote ni viongozi wazuri na wenye uzoefu, lakini akahadharisha kuwa pamoja na uzoefu, kuna suala la aina ya watu wanaoongozwa ambao ni lazima Spika ajaye akubali jinsi walivyo.
    Amesema Spika ajaye anapaswa kukabiliana na hali halisi, atatakiwa kuwa mtulivu, kufahamu wabunge wake kwa kujifunza tabia zao mbalimbali, ili afahamu atakavyoishi nao vizuri kwa kuwavumilia na kuepuka kuwa mwepesi wa kukasirika.
    Akitoa mfano, alisema katika mabunge ya kimataifa yapo hayo na hakuna kupendelewa kwa vyama, huku akiongeza kuwa alifurahia kazi na marafiki zake na atawakumbuka sana.

    Created by Gazeti la HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment