Monday, 2 May 2016

Tagged Under:

TUCTA: Magufuli ni taa ya matumaini

By: Unknown On: 21:43
  • Share The Gag

  • Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya

    SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema Rais John Magufuli ameonesha mwanzo mzuri katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini, baada ya kutangaza kushusha Kodi ya Mshahara (PAYE) kwa asilimia mbili pamoja na kuahidi kufanyia kazi masuala mengine.
    Akihutubia Taifa juzi kwenye kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambayo kitaifa iliadhimishwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais Magufuli alitangaza kushusha PAYE kufikia asilimia tisa kutoka 11 ya sasa kuanzia mwaka wa fedha ujao wa 2016/2017.

    “Napenda kuwataarifu kuwa serikali yangu kama nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu, nimeamua kupunguza kodi ya mapato ya mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia tisa kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/2017, nikiwa na matarajio makubwa kuwa wabunge wataipitisha Bajeti yangu niliyoiwasilisha bungeni,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa na maelfu ya wafanyakazi waliofurika uwanjani hapo.

    Akizungumzia hotuba hiyo ya Rais, Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema jana kwamba Rais Magufuli ameonesha mwanzo mzuri katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi baada ya kupunguza kodi ya mshahara na pia kutangaza hatua kadhaa za kushughulikia matatizo yanayolalamikiwa na wafanyakazi hao.
    “Magufuli ni taa ya matumaini. Ameonesha mwanzo mzuri katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi. Tuna hakika kwamba ataendelea na kasi hiyo hasa baada ya kueleza jinsi ambavyo serikali yake iko tayari kushughulikia masuala mengine ambayo tulimueleza katika hotuba yetu,” alieleza Mgaya.
    Katibu Mkuu huyo wa Tucta alisema kwa msingi huo huo, shirikisho hilo litaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli katika hatua mbalimbali anazochukua katika kuongoza nchini, ikiwamo suala la kukabiliana na watumishi hewa.

    “Katika hili la watumishi hewa, tunaahidi tutamuunga mkono. Kwa sababu kiuhalisia hakuna watumishi hewa, lakini wapo watu wanaotengeneza watumishi hewa. Hawa ni wenzetu, wanaweza kuwa wanachama wetu au sio wanachama wetu. Tutamsaidia katika kuwafichua hawa,” alieleza Mgaya.

    Katika risala ya wafanyakazi nchini iliyosomwa na Katibu Mkuu huyo wa Tucta, ilisema licha ya kwamba wafanyakazi wamekuwa na kilio cha muda mrefu cha kulipwa kima cha chini cha mshahara kisichotosheleza kumudu kupanda kwa gharama za maisha, mshahara huo mdogo umekuwa pia ukitozwa kodi ambayo alieleza kuwa imekuwa ni ya mazoea kwa serikali kwa sababu ni rahisi kuikusanya.
    “Tuna imani mzigo huu tuliokuwa tumebebeshwa wafanyakazi wa kulipa kodi kubwa ya mshahara utapungua. Aidha, tunaamini serikali haitoshindwa kupunguza kodi ya mishahara kuwa tarakimu moja. “Tunashauri Ofisi ya Msajili wa Hazina ipewe nafasi kubwa katika kusimamia ipasavyo mashirika ya umma ili kuongeza na kuchangia Pato la Taifa. Aidha, tunapendekeza kodi inayokatwa kwenye malipo yatokanayo na Mikataba ya Hali Bora Kazini iangaliwe upya,” alisema Katibu Mkuu wa Tucta.
    Rais Magufuli alisema kwa kushusha PAYE, atakuwa amewapunguzia wafanyakazi mzigo mkubwa wa makato katika mishahara yao na ameamua kuanza na jambo hilo kwanza ili changamoto zilizopo za kiuchumi wazikabili.
    Alisema kwa sasa ameamua kushusha kwanza kodi hiyo, ambayo imekuwa ni mzigo mkubwa kwa wafanyakazi wengi na baadaye mambo yakiwa mazuri wataangalia namna ya kupandisha mishahara.
    Katika risala yao, Tucta walizungumzia masuala mengine ikiwamo wageni kufanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania, mifuko ya hifadhi ya jamii kutolipa fedha kwa wakati na pia kufanya uwekezaji usio na tija, uboreshaji wa mazingira ya kazi, serikali kuhamia Dodoma na wafanyakazi kuzuiwa kuunda vyama vya wafanyakazi.
    Akijibu hoja ya serikali kuhamia Dodoma, Rais Magufuli alisema tayari yeye kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wameshahamia Dodoma na hata yeye huenda Dodoma na kukaa Ikulu ya Chamwino.

    Alisisitiza nia ya serikali kuhamia Dodoma iko pale pale, hasa kwa kuwa suala hilo limeelezwa bayana katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, lakini akasema ni vyema wale wote ambao wanataka serikali kuhamia Dodoma wakaonesha mfano kwa vitendo ili na serikali nayo sasa iige mfano huo na kuhamia Dodoma.
    Kuhusu hifadhi ya jamii, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imelenga katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafaidika na mfumo wa hifadhi ya jamii nchini kuliko ilivyo sasa kwa kutaka wananchi wengi zaidi wanajiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NIHF) ili wawe na uhakika wa matibabu.
    Alisema serikali inaendelea na juhudi za kupanuia wigo wa huduma za Mfuko wa Afya Jamii (CHF) na pia kuwawezesha wafanyakazi wengi wa sekta binafsi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

    Lakini alisema wameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuachana na uwekezaji usio na tija na badala yake kuangalia uwekezaji wenye manufaa kama kuanzisha viwanda ambavyo vitaajiri watu wengi na wao kupata wanachama.
    Rais alisema ombi la Tucta juu ya kupunguza mifuko ya hifadhi ya jamii na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima wamelipokea na kuahidi kulifanyika kazi katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao 2016/2017 unaoanza Julai mosi.

    Chanzo habariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment