Waziri wa Mifugo, Uvuvi Mwigulu Nchemba.
SERIKALI imeondoa ushuru wa mazao kwenye mageti na sasa yatatozwa
ushuru yanapofika sokoni tu, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu
Nchemba amelieleza Bunge.
Kwa sasa mazao yamekuwa yakitozwa ushuru yanapofika mipaka ya kata
kwenye mageti maalumu na hata yanaporudishwa mashambani, hali ambayo
imekuwa ikilalamikiwa sana na wakulima nchini.
Mwigulu alieleza hayo wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha
2016/2017 bungeni mjini hapa jana. Katika mwaka ujao wa fedha, wizara
hiyo imeomba kuidhinishiwa Sh 275,063,518,000.
Vilevile aliwatangazia neema wakulima kwa kuwaambia sasa pembejeo za
kilimo zitapatikana kwa wingi akifafanua, “zitapatikana kama Coca- Cola
dukani.” Alisema wizara inapitia upya mfumo wa sasa wa vocha za pembejeo
kwa lengo la kupata mfumo utakaowezesha upatikanaji wa mbolea kwa
wakulima wote wanaohitaji kupitia maduka ya pembejeo kwa bei nafuu.
“Mbolea inategemewa kupatiwa ruzuku kutokea kwenye chanzo chake kabla
haijaingizwa nchini. Wizara tunapendekeza ipatiwe fedha zitokanazo na
ushuru wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi zinazowasilishwa Hazina ili
zitumike kuboresha miundombinu na upatikanaji wa ruzuku katika sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema.
Akizungumzia ugonjwa wa ebola, Mwigulu alisema mwaka wa fedha
2016/2017 Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa
Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO), watachunguza uwepo wa virusi vya
ugonjwa huo viitwavyo Filoviridae katika mbuzi na nguruwe kwenye maeneo
yanayopakana na mbuga za wanyama.
Alisema serikali itajenga kituo maalumu mkoani Dar es Salaam cha
kudhibiti ubora na usalama wa maziwa na kurasimisha wachuuzi wa maziwa
kufanya biashara endelevu. Alisema katika mwaka 2016/2017, wizara hiyo
itaandaa utaratibu wa kuanzisha upya Shirika la Uvuvi Tanzania kwa lengo
la kuwa na meli za kitaifa, zitakazokuwa zinavua bahari kuu.
Kwa upande wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Msemaji wa kambi hiyo kwa
Wizara ya Kilimo, Magdalena Sakaya alisema hadi Machi 31, mwaka huu,
wizara hiyo ilikuwa haijapokea hata shilingi moja kati ya Sh bilioni
19.4 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maendeleo.
Sakaya alisema kambi ya upinzani inaitaka serikali kuja na mpango wa
dharura wa mwaka 2016/2017, kuhakikisha kuwa kunakuwa na usafi na vifaa
bora vya kusafirisha nyama katika machinjio nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na
Maji, Dk Mary Nagu akisoma maoni ya kamati yake, aliitaka serikali
kuandaa utaratibu maalumu utakaowezesha ushirikishwaji wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kufanya doria ili kudhibiti
vitendo vya uvuvi haramu, hasa katika kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu
hasa katika kudhibiti uvuvi wa kutumia mabomu.
Chanzo HabariLeo.
Tuesday, 3 May 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment