Profesa Johannes Monyo |
MKUU wa Chuo cha Uhasibu (IAA) Njiro mkoani Arusha, Profesa Johannes Monyo amehukumiwa kifungo cha nje kwa sharti la kutofanya kosa lolote ndani ya mwaka mmoja.
Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Devotha Msofe baada ya kujiridhisha kuwa Profesa Monyo alifanya makosa ya kuajiri watumishi wanane wenye elimu ya darasa la saba bila kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma.
Hakimu Msofe alisema Profesa Monyo akiwa Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Njiro, aliwaingiza watumishi wanane kwenye ajira ya kudumu bila ya kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Mkuu Utumishi.
Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani kwa mashahidi 10 pamoja na vielelezo vinane vilivyotolewa mahakamani hapo na upande wa mshtakiwa kuwa na mashahidi wawili, mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka kuwa Profesa Monyo alifanya kosa hilo la kuajiri wafanyakazi hao wanane bila kufuata taratibu za kisheria.
“Mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa ulifanya kosa hili la kuajiri wafanyakazi wanane bila kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma hivyo mahakama hii inakutia hatiani kwa kukupa kifungo cha nje kwa sharti la kuutofanya kosa lolote katika kipindi cha mwaka mmoja,” alisema Hakimu Msofe.
Awali, Mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Adam Kilongozi alidai kuwa Juni, 2010 Profesa Monyo anatuhumiwa kuwapa ajira watumishi wanane ambao ni Pamela Maboko, Samson Mbarya, Mawazo Ndaro, Juma Nyarutu, Lilian Ngowi, Godfrey Mollel, Musa Maiki na Salim Shabani.
Kosa jingine ni Profesa Monyo kwa kutumia mamlaka yake vibaya, kuwaingiza watumishi hao wanane katika ajira, ilhali akijua elimu zao ni darasa la saba. Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo kutolewa, Profesa Monyo ameonesha kusudio la kukata rufaa kupitia kwa wakili wake, Severine Lawena.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, gazeti hili lilimhoji Mwanasheria wa Takukuru, Kilongozi, kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma au Kanuni zake inasemaje juu ya mtumishi anapohukumiwa akiwa bado yupo kazini, ambapo alisema kama mtuhumiwa amehukumiwa na akaonesha nia ya kukata rufaa, basi hukumu hiyo inaweza kufanya kazi au kutofanya kazi hadi hapo rufaa itakaposikilizwa.
Alisisitiza kuwa Takukuru wameshatuma nakala hiyo ya hukumu Tume ya Utumishi wa Umma, mwajiri wa Profesa Monyo, ili mamlaka husika zilifanyie kazi suala hilo lakini pia ni lazima mwajiri wake naye ajiridhishe na hukumu hiyo.
Chanzo habariLeo.
0 comments:
Post a Comment