Sunday, 8 May 2016

Tagged Under:

‘Sababu ya wabunge kuomba rushwa hii hapa’

By: Unknown On: 21:54
  • Share The Gag

  • Spika wa Bunge, Job Ndugai.

    SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ametaja sababu zinazochochea wabunge kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa, ni presha kutoka kwa wananchi inayotokana na kutakiwa kuchangia masuala mbalimbali katika majimbo yao.

    Spika huyo pia amewatangazia rasmi wabunge kuwa Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria utakaotenganisha uongozi na biashara.
    Aliyasema hayo wakati akizungumza katika uzinduzi wa Chama cha Wabunge wanaopambana na Rushwa (APNAC), mjini hapa. Aliwataka wabunge hao kujiepusha na vitendo vya rushwa licha ya kuwa na maslahi madogo.

    Pia aliwataka wajiandae na sheria hiyo kutokana na ukweli kuwa katika bunge hilo wabunge wengi pia ni wafanyabiashara. Presha za rushwa Alitaja sababu za wabunge wa Tanzania kujiingiza kwenye rushwa ni presha za wananchi wao kuwataka wachangie kila inapotokea msiba, sherehe, madawati, madarasa, barabara hadi ada.
    Alisema kutokana na kipato kidogo cha fedha, wabunge wengi hutafuta mbinu mbadala za kupata fedha kumudu gharama hizo. Mishahara ya wabunge na marupurupu yake kwa mwezi yanakadiriwa kufikia zaidi ya Sh milioni 11 kwa mwezi.

    Sababu nyingine ni mikopo yenye riba kubwa ambayo wabunge wengi wameichukua ikiwa ni pamoja na maslahi madogo wanayopata wabunge hao. “Kutokana na hali hii wakati mwingine humfanya kiongozi ahangaike kutafuta fedha na ndipo wengine hujiingiza katika vitendo hivi vya rushwa.
    Nawatahadharisha ninyi kama wabunge mnao wajibu wa kudhibiti rushwa na kuwa mfano katika jamii,” alisema. Spika alilia maslahi Alisema katika eneo la maslahi, ofisi ya Bunge inatambua kuwa bado maslahi wanayopata wabunge hao ikilinganishwa na kazi wanayofanya ni madogo hivyo, wanaendelea kuangalia namna ya kuyaboresha.

    Ndugai alisema wabunge wa Tanzania wana wajibu na jukumu kubwa la kudhibiti rushwa kwa kutunga sheria zinazopaswa kutumika katika kuunga mkono au kuleta miswada itakayosaidia kutokomeza rushwa. Alisema pia moja ya kazi ya wabunge ni kushauri na kusimamia Serikali.

    Alisema ni vyema pale ambapo kuna viashiria vya rushwa wakatoa ushauri huo bila kukubali kushawishiwa kwa rushwa. “Vilevile katika kupitisha bajeti za serikali, hapana budi kuhakikisha vyombo vinavyohusika na mapambano dhidi ya rushwa vimetengewa fedha za kutosha,” alisema.
    Aliwaasa wabunge kujiepusha na vishawishi vya rushwa kwa kuwa nafasi waliyonayo ni nyeti. Alisema pia kutokana na mwenendo wa umakini wa Serikali ya Awamu ya Tano, inawezekana wakawepo watu wanaoona umakini huo kama maslahi yao na kutumia njia pekee ya kuwarubuni wabunge.

    “Nawaasa msishawishike,” alisisitiza. Alisema kwa mujibu wa Jumuiya ya Vyama vya Wabunge Wanaopambana na Rushwa Afrika (GOPAC), takribani dola za Marekani bilioni 50 hutoroshwa Afrika kutokana na rushwa. “Hizi ni fedha nyingi sana za walalahoi zinazotumika kwa maslahi ya wachache,” alisema.

    Pia amehamasisha wabunge hao kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kile alichosema, katika awamu hii ya serikali ya awamu ya tano, yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo lazima aingie matatani. Sheria ya maadili “Muda si mrefu nitawaalika waje watoe semina kwenu kuhusu undani wa sheria hiyo ili wote muielewe vyema.
    Nawashauri muisome vizuri sheria hii ikija kwa sababu wengi wetu pamoja na ubunge tunafanya biashara ili tujiendeshe vizuri,” alisisitiza Ndugai. Alisema sheria hiyo ikipitishwa, haitakuwa ya kwanza Tanzania kuitekeleza kwani nchi nyingi duniani zimekuwa na mfumo unaotenganisha viongozi wake na biashara.

    “Wenzetu ni kawaida ukiingia kwenye siasa unakabidhi biashara yako mpaka pale utakapomaliza uongozi wako ndio unaruhusiwa kuendelea, naomba mjiandae kuipokea sheria hii, ni sheria nzuri na ina malengo mazuri,” alisema. Akizungumzia rushwa, alisema kila bunge lina sababu zake za wabunge kujiingiza katika vitendo vya rushwa .

    Wabunge; sheria hiyo ni mwiba Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili baada ya mkutano huo kumalizika, walisema sheria itakayotenganisha viongozi na biashara ni mwiba kwa wabunge wengi na itakapowasilishwa bungeni itazua tafrani.
    “Sikufichi, wabunge wengi sisi hapa mnavyotuona ni wafanyabiashara, ukituvua tu nafasi ya biashara hatuna kitu, hili kwa kweli kwetu ni mtihani haya tusubiri tuone,” alisema mmoja wa wabunge hao aliyekataa kutaja jina lake.

    Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, aliwataka wabunge kujiepusha kuhusishwa na rushwa akisisitiza kwamba, kutokana na nafasi yao katika jamii, wanapaswa kuwa mstari wa mbele kudhibiti tatizo hilo na kuwa mfano mbele ya jamii hiyo.
    “Niwaambie ukweli kwa nafasi hii tuliyonayo wabunge wenzetu hatutakiwi hata kutuhumiwa kwa rushwa. Sisi ndio tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kupambana kwa vitendo na walarushwa nchini mwetu,” alisema.

    Aidha alizungumzia suala la malalamiko ya adhabu kwa walarushwa kuwa ndogo na kukiri kwamba adhabu zinazotolewa kwa watu wanaothibitika kufanya vitendo vya rushwa ni ndogo ikilinganishwa na hasara iliyotokana na rushwa hiyo.
    “Nawaahidi hili tumelipokea la adhabu na tutawasilisha mapendekezo kwa ajili ya kuifanyia kazi sheria yetu ya rushwa. Naomba wabunge wenzangu mtuunge mkono kwa hili,” alisema Waziri Kairuki.

    APNAC yapongeza kupunguza rushwa Akiwasilisha mada ya kuhusu tathmini ya shughuli za APNAC katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mhadhiri wa Siasa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Davis Mwamfupe, alisema chama hicho kimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kueneza uelewa wa tatizo la rushwa hususan kwa wabunge.
    Hata hivyo, alisema changamoto kubwa iliyopo katika kutatua tatizo la rushwa, ni kutokana na mara zote rushwa kufanyika kwa siri na hufanywa na watu wenye nafasi kubwa katika jamii wakiwemo wanasiasa na wachumi hivyo kuwa vigumu kuwakamata.

    Aliwataka wabunge hao kutotumia nafasi zao ndani ya Bunge na kukemea rushwa kwa mdomo pekee bali waoneshe dhahiri kuichukia na kupambana nayo kwa vitendo. Mbunge wa Nkasi, Ally Keissy, wakati akichangia mada hiyo ya rushwa, alisema tatizo la rushwa litamalizika endapo Mahakama na vyombo vya dola vitachunguzwa kutokana na ukweli kuwa kesi nyingi za rushwa zimefunguliwa, lakini hazishindi.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment