UAMUZI wa Serikali wa kuwakata kodi kwenye kiinua mgongo chao
viongozi wa kisiasa akiwemo Rais John Magufuli, umepongezwa na wasomi na
wanasiasa, wakieleza unaleta usawa katika jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na gazeti hili, wasomi hao
walisema ilikuwa ni mazoea mabaya kuwaacha viongozi wanasiasa kutolipa
kodi wakati wanapomaliza muda wao; wakati watumishi wa kawaida ambao
vipato vyao ni vidogo walikuwa wanakatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi,
alisema uamuzi huo umeifanya serikali kuwa na chanzo kipya cha mapato,
lakini pia ni uamuzi ambao umeleta haki katika jamii. “Maamuzi haya
yalitakiwa kufanywa miaka ya nyuma, niseme tumechelewa sana maana hawa
viongozi wanahudumiwa kila kitu na kupatiwa matibabu, ki ukweli wana
maisha mazuri. Kitendo cha kuwasamehe kodi kwenye kiinua mgongo chao
haikuwa halali,” alisema Profesa Ngowi.
Alisema hatua hiyo ilikuwa inaongeza pengo la kipato kati ya wananchi
wa kawaida na viongozi wa kisiasa, kwani ilikuwa viongozi ambao wana
maisha mazuri wanaongezewa faida nyingine ya kutokatwa kodi na mtumishi
wa kawaida, ambaye anapata mshahara mdogo alikuwa analipa kodi
anapostaafu. Hata hivyo alisema matunda ya uamuzi huo wa serikali,
yataanza kupatikana baada ya miaka mitano.
“Hivyo hakuna fedha itakayoingia mwaka ujao wa fedha hadi mwaka 2020
ndipo serikali itapata kodi hiyo kutoka kwa viongozi wanasiasa
wastaafu,” alisema. Wasomi kwenye siasa Alisema uamuzi huo wa serikali,
pia unaweza kusaidia kupunguza kasi ya wasomi kuingia kwenye siasa maana
watafahamu kwamba kuanzia sasa baadhi ya vivutio vilivyokuwepo vinaanza
kuondolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kupunguza
Umasikini (Repoa), Dk Donald Mmari alisema uamuzi wa viongozi wa
kisiasa, kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao ni jambo jema kwa sababu
ni kada, ambayo kiinua mgongo chao ni kikubwa na kutokatwa kodi haki
haikuwa inatendeka.
Alisema watumishi wa umma wanapata kiinua mgongo kidogo, kutokana na
mishahara yao kuwa kidogo, lakini wamekuwa wanakatwa kodi, hivyo
wanasiasa nao kukatwa kodi huo ndio kanuni ya usawa katika ulipaji wa
kodi. “Huduma zote tunapata sawa, barabara tunatumia wote, hivyo kanuni
ya kodi ni kwamba anayepata zaidi alipe zaidi, kitendo cha kutolipa kodi
kilitokana na wanasiasa kujipendelea tu,” alisema Dk Mmari.
Aliongeza kuwa kisingizio kwamba wanasiasa hawana pensheni kama
watumishi wengine wa umma, sio jambo la kutilia maanani, kwani watumishi
wa umma ambao wanafanya kazi kwa mikataba wanapomaliza mikataba yao
wanalipwa kiinua mgongo ambacho pia kinakatwa kodi.
Alisema kama wabunge na wanasiasa wengine walioko madarakani, wana
fursa ya kupata mikopo ya kununua magari, kuna watumishi wa umma ambao
hawana fursa hiyo na hao ndio ambao wamekuwa wanalipa kodi kwa Serikali.
Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema
kilichofanywa na Serikali kuwakata kodi wanasiasa kwenye kiinua mgongo
chao, sio jambo baya kwani sababu za awali zilizokuwa zinafanya
wasikatwe au kusamehewa kodi kwa sasa hazipo tena.
Alisema miaka ya nyuma, wanasiasa waliondolewa kodi kwenye viinua
mgongo vyao kwa kuamini kuwa wakimaliza kazi zao za siasa, hawawezi
kupata kazi tena na ilikuwa ni moja ya kuvutia watu wasomi waingie
kwenye siasa isaidie kupata viongozi wa kisiasa. “Lakini kwa sasa wasomi
ni wengi na siasa imekuwa kazi kama ilivyo kazi zingine, leo hii mtu
akiacha siasa anaenda kufanya kazi nyingine.
Mfano Mzee Pinda (Mizengo Waziri mkuu mstaafu) kwani hana income
(kipato) nyingine? Jibu ni kwamba anayo,” alisema Profesa Semboja.
Aliongeza kuwa ni mazoea mabaya kwa watu ambao wanapata kipato kikubwa,
kutokatwa kodi huku anayepata kipato kidogo ndiye akatwe kodi. Alisema
wakati umefika sasa wa kuachana na mazoea hayo mabaya na kwamba sababu
za kusamehe wanasiasa wasikatwe kodi hazipo tena.
Alisema kilichofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli sio jambo
baya kwani siasa ni sawa na kazi nyingine na mwanasiasa muda wake
ukiisha anafanya kazi nyingine. Usawa kwa watumishi Mwanaharakati wa
Haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa, alisema kilichofanywa na Serikali
ni jambo jema kwa maelezo kuwa wanasiasa ni watumishi kama ilivyo
watumishi wengine na hivyo uamuzi wa Serikali ni wa kuleta usawa
miongoni mwa watumishi wote.
Olengurumwa alisema iwapo wabunge na mawaziri, watakatwa kodi
watakuwa makini kusimamia kodi hizo, zilete maendeleo na kwamba
zitasaidia pia na wanasiasa hao, kuendelea kupata mishahara yao. “Hivyo
mimi naona hiki kilichofanywa na Serikali ni kuleta usawa, wanasiasa
walipewa upendeleo sana na hata kutungiwa sheria ya kulinda maslahi yao,
sasa kama hili limeondolewa ni haki imetendeka kwa watu wote,” alisema
Olengurumwa.
Alihadharisha kuwa kodi hiyo ya wastaafu haiwezi kuleta tija kwenye
uchumi wa nchi kwa kuwa kitakachofanyika hapo ni kama serikali
imepunguziwa mzigo wa kulipa wanasiasa wastaafu. “Hapo kama mbunge
alitakiwa kulipwa Sh milioni 200 atalipwa Sh 180 kwa hiyo fedha
zinazozunguka ni zile zile, kuna haja ya serikali kuangalia kupanua wigo
kutoka kwenye mapato yanayotokana na rasilimali za nchi yetu,” alisema
mwanaharakati huyo.
Alisema kuna nchi hazina rasilimali nyingi kama ilivyo kwa Tanzania,
lakini wananchi wake wamekuwa wanafaidika na mapato ya rasilimali hizo
kidogo, hivyo akashauri kwamba umefika wakati wataalamu serikalini
wakune vichwa kuona namna serikali inavyoweza kupata mapato mengi
kutokana na hizo rasilimali.
Ma DC waridhika Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Yahaya Nawanda, alisema
suala la viongozi wa kisiasa kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao
amelipokea kwa furaha kwa sababu mtumishi yeyote wa umma anatakiwa
kulipa kodi. “Naipongeza Serikali yangu kwa kuanzisha jambo hili, maana
kulipa kodi ni jambo jema kwani inalenga kuboresha maisha ya Mtanzania,”
alisema Nawanda.
Alisema bila kulipa kodi nchi haiwezi kupata maendeleo na hivyo yeye
binafsi anaunga mkono uamuzi huo ili kupeleka mbele maendeleo ya
wananchi. “Bila kodi hakuna mishahara hii tunayolipwa na hakuna nchi
iliyoendelea bila wananchi wake kulipa kodi, hivyo wanasiasa kukatwa
kodi kwenye kiinua mgongo ni jambo jema.”
Nawanda alisema wanasiasa ambao ni viongozi wa wananchi, wanatakiwa
walipe kodi, wawe mfano kwa wananchi na kuwajengea tabia wananchi kulipa
kodi bila shuruti. Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Humphrey Polepole alisema
uamuzi wa viongozi wa kisiasa, kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao
tayari umepitishwa na Bunge na hivyo watu wanatakiwa kuutekeleza na
kuusimamia.
“Kwa taratibu za nchi yetu tulizojiwekea, Bunge ndilo linapitisha
Bajeti na kutunga sheria, jambo hili ambalo umeniuliza tayari
limepitishwa na Bunge, hivyo sisi tunatakiwa kutii na kuheshimu uamuzi
huo, kitendo chochote cha kuchallenge (kuhoji) uamuzi huo ni ukiukwaji
wa taratibu za nchi,” alisema Polepole.
Juzi Bunge limepitisha Bajeti ya Serikali huku miongoni mwa
marekebisho yaliyofanyika ni kwa viongozi wa kisiasa akiwemo Rais,
Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Wabunge kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo
chao.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliliambia Bunge kwamba
Rais Magufuli amekubali yeye kiinua mgongo chake pamoja na viongozi
wengine nacho kikatwe kodi. Hatua hiyo ya Rais Magufuli ilikuwa ni
majibu kwa wabunge, ambao walikuwa wanalalamika kwamba kwa nini viongozi
wengine wa kisiasa wameachwa katika mpango huo.
Chanzo HabariLeo.
Tuesday, 21 June 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment