JESHI la Polisi Kikosi cha viwanja vya ndege, Dar es Salaam
linamshikilia raia wa Nigeria, Bede Eke (45) kwa tuhuma za kusafirisha
unga unaosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege
Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Martin Otieno alisema mtu huyo
alikamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa safarini kwenda Lagos, Nigeria.
“Juni 26, mwaka huu majira ya saa 7:25 usiku katika eneo la ukaguzi
wa mashine ya chini, askari Polisi kwa ushirikiano na askari wa uwanja
wa ndege Terminal II walifanikiwa kumkamata Bede Eke akiwa na begi
walilolitilia shaka na katika upekuzi walibaini kuwa na unga,”alisema
Otieno.
Kamanda Otieno alisema Eke alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere (JNIA) akisafiri kwa Ndege ya Ethiopian Airline kwenda
Lagos, Nigeria kupitia Ethiopia, ambapo baada ya kutiliwa shaka katika
begi hilo waliamriwa kulifungua na ndani palikuwa na begi dogo la
mgongoni, ambalo lilishonwa vizuri na kufungwa na gundi ya nailoni.
Alisema ndani ya begi hilo dogo la mgongoni jeusi, mlikuwa na
kifurushi chenye uzito wa kilo tano na kilipofunguliwa palikuwa na unga
unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.
“Tumepeleka sampuli ya unga huo kwa mkemia mkuu wa serikali ili
kuweza kutambua ni aina gani ya dawa za kulevya, lakini bado tunaendelea
na mahojiano naye ili kubaini ni wapi amechukua unga huo,” alisema
Otieno.
Kamanda Otieno alisema kuwa kukamatwa kwa mtuhumuwa huyo kunatokana
na kuongezeka kwa udhibiti na kupata mashine za kisasa za utambuzi,
ikiwa ni pamoja na ari ya kazi. Tukio hilo limetokea wakati taifa na
dunia, inaadhimisha upigaji vita wa dawa za kulevya. Tukio hilo ni la
kwanza kwa mwaka huu katika uwanja huo.
Chanzo HabariLeo.
Monday, 27 June 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment