Tuesday, 21 June 2016

Tagged Under:

Mahakimu 5 mahakama za wilaya kutumbuliwa

By: Unknown On: 22:37
  • Share The Gag

  • Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othmani.

    MAHAKIMU watano wa mahakama za wilaya, wanakabiliwa na uwezekano wa kuadhibiwa kutokana na kile kilichoelezwa ni kushindwa kufikisha malengo ya idadi ya kesi za kuamua kwa mwaka.

    Kamati ya Maadili ya Maofisa wa Mahakama, imeshauri Tume ya Utumishi wa Mahakama, iwape adhabu ya onyo kutokana na kushindwa kufikisha malengo na kutoa sababu zisizoridhisha.
    Februari mwaka huu, mahakimu hao ambao majina yao na vituo vyao havikutajwa, walipewa siku saba na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman kutoa maelezo kwa nini wasifunguliwe mashtaka ya nidhamu au kuwajibishwa kwa kushindwa kufikia kiwango cha kuamua kesi 260, walizopaswa kuzishughulikia kwa mwaka.

    Akizungumza na gazeti hili juu ya hatua zilizochukuliwa na hatma ya maelezo hayo , Jaji Mkuu alisema ufuatiliaji wa mahakimu 507, umebaini kwamba 318 wakiwemo mahakimu 271 wa Mahakama ya Mwanzo na 71 wa wilaya, waliamua kwa kweli mashauri chini ya 100 kwa kuwa mahakama zao hazina kesi zaidi ya 100.
    Alifafanua kuwa kati ya jumla hiyo, wapo pia mahakimu 65 walioajiriwa mwishoni mwa mwaka jana, 59 waliokwenda masomoni mwaka jana katikati, 15 walipandishwa vyeo kwenda ngazi ya juu na mahakimu 10 waliachishwa kazi au kustaafu.
    “Ni mahakimu watano tu na ni wa Mahakama za Wilaya ambao walitoa sababu zisizoridhisha na wote wamefikishwa mbele ya Kamati ya Maadili ambayo imependekeza wapewe onyo na Tume ya Utumishi wa Mahakama,” alisisitiza.

    Jaji Mkuu alisema kutokana na hali hiyo, sekta ya Mahakama imepata fundisho kwamba inabidi ijipange upya kwani imedhihirika kuwa mwaka jana Mahakama imepoteza jasho la mahakimu 318 kutokana na kufanya kazi kwenye mahakama hasa za mwanzo zenye kesi chini ya 100 wakati uwezo wao ni kuamua mashauri mengi zaidi.
    “Tumeona haiwezekani kufunga mahakama zenye kesi chini ya 100 kwa mwaka na kuwahamisha mahakimu hawa kwenye vituo vingine vyenye kesi nyingi kwani hatua hii itapingana na dira yetu ya kuwapa Watanzania hasa vijijini fursa sawa ya kupata haki,” alisema.

    Jaji Chande alisema wameona ni busara kuwahamasisha mahakimu hao kujipanga kwa awamu na mpangilio ndani ya mwaka na kwa kipindi kwenye mahakama zenye kesi nyingi ndani ya kanda zao ili kupunguza idadi ya mashauri na kila mmoja kuamua kesi 260 kwa mwaka.
    Alisema endapo Mahakama itajipanga vizuri na kila hakimu kati ya hao 318 wakiamua kesi zaidi ya 100, wote kwa pamoja wana uwezo wa kuamua mashauri 31,800, hali itakayowezesha sekta hiyo kufikia lengo lake la kesi sifuri kila mwisho wa mwaka katika mahakama zote nchini.
    Akizungumzia tathmini kuhusu utendaji wa mahakama hizo, alisema mahakama za mwanzo zimeonekana kufanya vizuri kwani kati ya mahakama hizo 638, sawa na asilimia 93.5 kati ya 730 zilizopo Tanzania Bara zimemaliza malengo ya kuamua kesi sifuri zilizokuwepo mahakamani mwaka jana.

    Alisema kwa sasa mahakama hizo za mwanzo, zimebaki na kesi 15,175 zenye umri usiozidi miezi minne na kuna kesi 1,622 tu zenye umri wa zaidi ya miezi sita. Alisema Januari hadi Aprili mwaka huu, mahakimu 1,027 walio Mahakama za Mwanzo waliamua kesi 64,908, kwa kila hakimu kuamua kwa wastani mashauri 63 na wengine waliofanya bidii zaidi waliamua mashauri zaidi ya 100.
    “Tulianza kwa kupima idadi ya kesi, hivi sasa tunapiga hatua kwa kuanza kupima pia ubora wa hukumu, tutazingatia vigezo na idadi, ubora, ufasaha, muda wa uamuzi na mambo mengine muhimu. Huko ndiko tunakoelekea,” alifafanua.

    Kuhusu utendaji wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya, Jaji Mkuu alisema tathmini ya utendaji imebaini kuwa kati ya Januari hadi Aprili mwaka huu, Mahakama za Hakimu Mkazi 29 zenye mahakimu 131, ziliamua mashauri 7,752.
    Alisema mahakama za wilaya zilizopo 108 zinazoendeshwa na mahakimu 292 ziliamua mashauri 14,668 kati ya Januari hadi Aprili mwaka huu. “Pamoja na kila Mahakimu wa Mahakama hizo kuamua wastani wa kesi 50 hadi 59 kwa kipindi cha miezi minne bado jitihada kubwa zinahitajika ili kukabiliana na mashauri 21,664 yaliyobaki,” alisisitiza.

    Chanzo HabariLeo.

    0 comments:

    Post a Comment