Monday, 27 June 2016

Tagged Under:

Rungu la mawadati mikoani, wilayani laja

By: Unknown On: 01:29
  • Share The Gag

  • Msemaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Rebecca Kwandu.
    WAKUU wa mikoa wako kwenye hekaheka wakati zikiwa zimebaki siku tatu, kabla ya tarehe ya mwisho ya agizo la Rais John Magufuli, kuhakikisha tatizo la madawati linakoma nchini.
    Wakati baadhi ya wilaya na hata mikoa ‘imetamba’ kuwa katika hali nzuri ya utekelezaji, yako maeneo ambayo utekelezaji haujakamilika, huku viongozi wake wakiomba waongezewe muda wa utekelezaji.
    Gazeti hili lilifuatilia mikoa mbalimbali na kubaini wakuu wa mikoa wakiendelea na harakati za kukusanya taarifa kutoka wilayani, huku baadhi wakizitolea uvivu halmashauri zilizoshindwa kutekeleza kwa uzembe; na kusema hawatakuwa tayari kumuomba rais aongeze muda.
    Akizungumza na mwandishi jana, Msemaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Rebecca Kwandu alisema baada ya Juni 30, Waziri wa Nchi, Tamisemi, George Simbachawene atatoa taarifa juu ya hatma ya utekelezaji huo.
    “Kwa sasa sina la kusema kwa sababu bado tarehe haijafika, tunasubiri tupate kwanza tathmini ya nchi nzima kwa sababu ukweli kuna baadhi ya maeneo wamefanya vizuri wamevuka hadi lengo. “Lakini pia kuna baadhi ya maeneo wametuma barua kuwa wamepata matatizo wameshindwa kufikia lengo na wengine wakiomba kuongezewa muda,” alisema Kwandu na kusisitiza kuwa Waziri Simbachawene atatoa tamko baada ya siku iliyowekwa, kulingana na hali halisi itakavyokuwa.
    Mikoa iliyo vizuri Miongoni mwa mikoa ambayo gazeti hili limezungumza na viongozi wake ni Arusha, ambako Mkuu wa Mkoa, Felix Ntibenda alisema wako katika nafasi nzuri ya kuepuka rungu la Rais John Magufuli baada ya kukamilisha asilimia kubwa ya mahitaji ya madawati .
    Akizungumza na gazeti hili kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alisema wana uhakika kabla ya Juni 30, mwaka huu, uhaba wa madawati utakuwa historia.
    Alisema hadi Juni 23, mwaka huu mkoa huo ulikuwa umebakiza madawati 161, kukamilisha mahitaji yake ya madawati 119,765. Halmashauri zabanwa Miongoni mwa halmashauri ambazo hazijakamilisha ni wilaya na manispaa ya Sumbawanga.
    Mkuu wa wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven ameagiza wahakikishe utengenezaji wa madawati, unafanyika usiku na mchana kabla ya siku aliyoagiza rais. Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu alisema halmashauri hiyo ina idadi ya shule za msingi 55 na sekondari za umma 17.
    “Tuna uhakika wa kumaliza upungufu wa viti na meza katika shule za sekondari ifikapo Juni 30 mwaka huu,” alisisitiza.
    Kwa upande wa waliofanya vizuri ni halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, ambao walisema wana uhakika hakuna mwanafunzi atakayekaa sakafuni kwa ukosefu wa madawati ifikapo tarehe iliyotolewa na Rais Magufuli.
    Vile vile Manispaa ya Sumbawanga imefanya vizuri kwa upande wa shule za sekondari, kutokana na taarifa yake kuonesha imebakiza viti na meza 54 tu, kukamilisha mahitaji ya meza na viti 1,327 .
    Mkoani Kilimanjaro, akizungumza na mwandishi wa gazeti hili juzi, Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadiki alisema leo anakutana nao kutoka wilaya zote kwa lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa agizo la rais.

    Walioomba kuongezwa muda Wakati Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alisema hawajakamilisha utengenezaji wa madawati 4,587, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, John Mongela alisema hatakuwa tayari kuandika barua kwa rais, kuomba aongezewe muda wa utekelezaji agizo la kutengeneza madawati kutokana na uzembe.
    Mongela ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisema hayo wakati wa kupatiwa taarifa juu ya ukamilishaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari kwa wilaya ya Shinyanga.

    Alisema hatakuwa na nafasi wakati wa kuandika taarifa yake kwa rais juu ya ukamilishaji wa madawati kuomba uongezwe muda kwa viongozi walioonesha uzembe, kwani atafanya kuomba muda kwa wale walioonesha nia yenye kuleta matumaini.
    Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Hawa Ng’humbi pia ameomba uongezwe muda, wakamilishe uhaba wa madawati ndani ya mwezi mmoja wanafunzi wote wapate madawati.

    Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alisema utekelezaji wa agizo la rais, unakwenda vizuri kwani wamefikia asilimia 90 ya madawati huku mengine yakiendelea kutengenezwa.
    Ofisa Elimu wa mkoa Kigoma, Germana Mng’aho alisema kabla ya kutolewa kwa agizo la rais, mkoa huo ulikuwa na upungufu wa madawati 150,000 katika shule za msingi na sekondari .
    Alisema hadi sasa zaidi ya asilimia 90 zimetekelezwa na hadi tarehe waliyopewa, watakuwa wamemaliza.

    Wadau wameokoa jahazi Aidha, wadau mbalimbali wameonekana kuokoa jahazi kwa kuchangia ama madawati au fedha kwenye mikoa mbalimbali.
    Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Bakari Sajini alisema wadau mbalimbali, wamechangia mafanikio katika utekelezaji wa agizo hilo kutokana na kuchangia madawati kwa nyakati tofauti.
    Alisema walifanya ukaguzi wa madawati katika shule zote na kubaini wana upungufu wa madawati 4,683.
    Alisema sasa wamekamilisha madawati 4,303 na wamebakiza madawati 380.
    Kwa upande wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema anasubiri wataalamu wawasilishe taarifa mkoani kabla ya kujumuishwa na kupata tathimini kamili ya utekelezaji.

    Baada ya agizo la rais alilotoa Januari mwaka huu la kutaka kuona kila mwanafunzi anaketi kwenye madawati, Waziri Simbachawene alisema agizo hilo la rais, halina mjadala na kwamba ifikapo Juni pasiwepo mwanafunzi anayeketi sakafuni na wakurugenzi watakaoshindwa, watakuwa wameshindwa kazi na watawajibishwa.

    Habari hii imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga;, Angela Sebastian, Bukoba; Arnold Swai, Moshi; Kareny Masasy, Shinyanga; Fadhili Abdallah,Kigoma; Veronica Mheta, Arusha na Halima Mlacha.

    Chanzo habariLeo
     
     

     
     

    0 comments:

    Post a Comment