SERIKALI
imemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchukua hatua stahiki katika
shauri la kesi ya jinai namba 100 ya Jamhuri dhidi ya Isaac Emily
aliyeadhibiwa kulipa faini kwa kumtukana Rais John Magufuli mtandaoni.
Hayo
yamesemwa jana bungeni na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison
Mwakyembe wakati akitoa kauli ya serikali baada ya mwongozo ulioombwa na
wabunge wa CCM, Juma Nkamia wa Jimbo la Chemba na Livingstone Lusinde
wa Mtera, baada ya hukumu hiyo kutolewa hivi karibuni. Hata hivyo, hatua
stahiki hizo hazikuelezwa.
Alisema
nia ya maagizo hayo kwa DPP ni kulinda dhana na dhamira ya adhabu
katika mfumo wa haki jinai ambayo hutaka mhukumiwa kujutia kosa lake na
wengine kujifunza kutoka kwake.
Katika
maelezo yake, Waziri Mwakyembe alisema kwa hali ilivyo katika shauri
hilo, dhana na dhamira ya adhabu haikuweza kufikiwa kwa mwenendo wa
kuingiza siasa katika utekelezaji wa hukumu.
Alisema
serikali imejiridhisha na kilichotokea katika shauri hilo na kauli za
wabunge walioomba mwongozo kwamba masharti ya adhabu yalikuwa mepesi mno
usiolingana na shauri lenyewe.
Alisema
aliyehukumiwa analifanyia siasa suala hilo na kuigeuza adhabu rafiki
aliyopewa kuwa burudani ya kisiasa katika mitandao ya kijamii.
“Mheshimiwa
spika, nimejiridhisha na kilichotokea. Madhara ya mwelekeo huu mpya
katika haki jinai, ni kuchochea vitendo zaidi vya ukaidi kwa mamlaka za
nchi na hivyo kujenga msingi wa vurugu. Hili halikubaliki katika utawala
wa sheria. Mdharau mwiba mguu huota tende,” alisema..
Alisema
kosa kama hilo lilitokea Kenya mwaka jana ambapo mwanafunzi wa Chuo
Kikuu nchini humo, Alan Okengo (25) alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja
na kulipa faini ya dola 2,000 (Sh milioni 3.2) kwa kumtukana rais wa
nchi hiyo kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema
pamoja na umri wake na uwezo wake mdogo wa kulipa faini, adhabu ilibaki
palepale ili mkosaji ajutie kosa lake asije akarudia na jamii ijisikie
salama.
Alisema
pamoja na kutokuingilia mhimili wa mahakama na taratibu zake kitendo
cha kuwapo kwa adhabu ambayo haijutiwi inakiuka dhana na dhamira ya
adhabu.
Alisema
kwa shauri la Emily, pamoja na kutiwa hatiani wakili wake aliomba
mtuhumiwa alipe faini kwa kuwa hakusumbua mahakama na pia ni kosa lake
la kwanza na ana familia.
Alisema
wakati hakimu anamuuliza wakili wa serikali aliiachia mahakama kutoa
maamuzi ambayo ilimpatia wakili wa utetezi maombi yake.
Mwakyembe
alisema pamoja na maagizo ya serikali kwa DPP amewakumbusha waendesha
mashitaka nchini kuwa macho na waweke mbele weledi na maslahi mapana ya
taifa na kamwe wasiyumbishwe na mihemko ya kisiasa katika jamii.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment