WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki
SERIKALI imeagiza wote waliotengeneza watumishi hewa wafunguliwe
mashitaka mahakamani huku ikionya kuwa iko tayari kusimamisha kazi
maofisa utumishi wote nchi nzima wanaofikia 1,500 katika sakata hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella
Kairuki alisema hayo jana alipokuwa akichangia mjadala wa Hotuba ya
Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 bungeni
mjini Dodoma. Amesema tayari serikali imeshatoa agizo hilo la
kuwashitaki maofisa wote waliotengeneza watumishi hewa na ikibidi iko
tayari kuwasimamisha kazi maofisa utumishi 1,500 waliofundishwa kazi
hiyo na serikali.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, mpaka mwishoni mwa Mei, serikali
ilikuwa imebaini uwepo wa watumishi hewa 12, 246 waliokuwa wakitafuna Sh
bilioni 25.06 kila mwezi. Katika kuelezea athari za ufujaji huo wa
fedha za serikali, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji
alisema hata katika ulipaji wa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii,
Rais John Magufuli aliagiza uhakiki ufanyike, kabla ya kulipa kwa kuwa
penye wafanyakazi hewa, kuna malipo hewa ya wastaafu.
Alitoa mfano wa deni la Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Serikali ilikuwa
ikidaiwa Sh trilioni 2.67 lakini uhakiki wa deni hilo ulipofanyika, deni
hilo likabainika ni Sh trilioni 2.04, hatua iliyosaidia Serikali
kuepusha wizi wa karibu Sh bilioni 600 za wastaafu hewa. January na
uthubutu Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na
Muungano), January Makamba alizungumzia ahadi ya Rais ya kutoa Sh
milioni 50 kila kijiji na kufafanua kuwa Sh bilioni 59 zilizotengwa,
zitatumika kujifunza namna ya kutekeleza ahadi hiyo.
Aliwataka wabunge wa CCM kukumbuka kuwa chama hicho kilipomtangaza Dk
Magufuli kuwa ndiye mgombea urais, kilitoa taarifa duniani ya aina ya
Serikali, uongozi na mabadiliko wanayotaka Watanzania. Alisema
mabadiliko ya kweli hayawezi kutokea bila kuwepo kwa hatua kubwa na
uthubutu ndio maana serikali imethubutu kuwa na Bajeti ya Sh trilioni
29.5 na uthubutu wa kutenga asilimia 40 ya bajeti hiyo katika maendeleo.
Kwa mujibu wa January, mahali popote kwenye uthubutu, lazima kutakuwa
na watu watakaotia shaka na kuwataka wabunge wa CCM wasitilie shaka
uwezo wa serikali katika kukusanya Sh trilioni 29.5 zilizokusudiwa.
Alisema wabunge wa CCM ndio wengi katika Bunge na Ilani ya Uchaguzi
inayotekelezwa ni ya chama hicho, hivyo ni muhimu wamuunge mkono Rais
Magufuli kwani akifanikiwa Rais na Tanzania imefanikiwa.
Alikumbusha kuwa maendeleo yanahitaji kujitoa sadaka na viongozi wao
wamekubali kujitoa sadaka, hivyo wabunge, wafanyabiashara mpaka wadogo
wakiwemo bodaboda, wajitoe sadaka kwa kulipa kodi. Alitumia kauli ya
Rais John Kennedy wa Marekani aliyoitoa miaka ya mwanzo ya 1960,
alipowataka wananchi wa nchi hiyo, kutouliza nchi hiyo itawafanyia nini,
bali wajihoji wao wataifanyia nini nchi yao.
Watanzania wanune Naye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage alieleza namna Serikali ya China ilivyoridhia kutoa Sh
trilioni tano nje ya Bajeti ya Serikali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda
kwa sekta binafsi, huku ikiahidi kutoa fedha nyingine Dola za Marekani
milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo.
Alihitimisha kwa kusema ujenzi wa uchumi wa viwanda ni sawa na vita
na wakati wa vita, hakuna anayecheka hivyo Watanzania wote lazima
wanune, ili kutimiza malengo ya kuongeza pato la jumla la taifa. Aidha,
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema pato la
jumla la Taifa kwa sasa ni Dola za Marekani bilioni 55 na ili Tanzania
ifike katika uchumi wa kati, inatakiwa kuongeza uzalishaji utakaoongeza
pato la jumla la Taifa kuwa Dola za Marekani bilioni 200.
Alisema injini za kupeleka uzalishaji na uchumi katika kipato hicho,
ziko nyingi na mojawapo ni sekta ya nishati ya umeme ambayo katika
bajeti hiyo ya serikali, Wizara ya Nishati na Madini imetengewa Sh
trilioni 1.43 ambapo asilimia 94 ya hizo ni za maendeleo na kati ya
fedha hizo za maendeleo, asilimia 95 inakwenda kwenye umeme.
Katika kudhihirisha nia ya serikali katika sekta hiyo, Profesa
Muhongo alisema katika bajeti inayomaliza muda wake, wizara hiyo
imeshapata asilimia 80 ya fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu
unaoisha huku Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ikiwa imeshapata asilimia
80 ya fedha iliyotarajia. Aliwaeleza wabunge kuwa katika bajeti
waliyopitisha, usambazaji wa umeme vijijini umepangiwa Sh bilioni 534.
chanzo HabariLeo
Monday, 20 June 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment