Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro. |
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema inaendelea kumtafuta Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwa ajili ya kumhoji kuhusu mahubiri yake aliyoyatoa wiki moja iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jeshi hilo bado linaendelea kumtafuta na endapo mtu yeyote ana taarifa za alipo askofu huyo, asisite kupeleka taarifa Polisi ili akamatwe.
Kamanda Sirro alisema Askofu Gwajima hajapatikana na hawafahamu amekwenda wapi, lakini bado wanaendelea kumtafuta kwa mahojiano zaidi. “Tunaendelea kumtafuta, tunaamini tutampata ili ahojiwe, tunawaomba pia wananchi yeyote mwenye taarifa juu ya mahali alipo askofu huyo tunaomba watupe taarifa ili aweze kukamatwa,” alisema Sirro.
Askofu Gwajima anatafutwa na jeshi hilo kwa ajili ya kuhojiwa juu ya mahubiri yake aliyoyatoa Juni 11, mwaka huu kanisani kwake Ubungo Maji jijini Dar es Salaam. Katika mahubiri hayo ambayo yalisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, askofu huyo alisikika akiukosoa utendaji kazi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Pia Gwajima alisikika akimshauri Rais John Magufuli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo watakataa kumkabidhi uenyekiti na kwamba apeleke muswada bungeni, kuondoa kinga ili rais ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment