Sunday, 29 May 2016

Magufuli tumemkubali, tunamuombea GWIJI

By: Unknown On: 23:47
  • Share The Gag
  • Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Dk Barnabas Mtokambali.

    ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dk Barnabas Mtokambali amesema Mungu ameikumbuka Tanzania kwa kuipatia kiongozi mkuu wa nchi mwenye uchungu na taifa lake.
    Dk Mtokambali amemtaja Magufuli kuwa ni miongoni mwa viongozi wachache Afrika wenye malengo na nchi, ambao hutokea kwa nadra.

    Alimfananisha na viongozi kama Mwalimu Julius Nyerere, Patrice Lumumba wa Kongo na Kwame Nkrumah wa Ghana. Askofu Mtokambali alisema hayo juzi wakati wa sherehe ya kuweka wakfu jengo jipya la kanisa la TAG Nkuhungu.
    Alisisitiza kwamba kanisa linasimama na serikali iliyopo madarakani.
    “Magufuli tumemkubali, wanyang’anyi, wala rushwa, wezi hawatampenda, kanisa tunampenda, tunamkubali na tunamuombea. Ni nadra kupata rais mwenye mzigo na nchi, hutokea mara chache sana,” alisema.
    Alisema rais amekuwa na maadui wengi kutokana na kugusa maslahi ya watu. Wakati huo huo, akizungumzia kanisa hilo, alisema limefanikiwa kuchimba visima 30 na vyote vinafanya kazi .

    Alisema pia wamezindua zahanati bora katika mji wa Dodoma na sasa wana mkakati wa kufanya kiwe kituo cha afya. Akizungumzia elimu, alisema kanisa hilo lina mpango wa kujenga chuo kikuu kikubwa katika eneo la Chigongwe na wamefuata taratibu zote za serikali .
    Kwa mujibu wa askofu mkuu, wana eneo la ekari 560. Pia ekari 100 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi watakaofanya kazi chuoni hapo. Alisema changamoto kubwa iliyotokea ni baadhi ya watu kujitokeza na kudai maeneo hayo kuwa ni yao.
    Hata hivyo, alisema walishinda kesi hiyo mara mbili, lakini mpaka sasa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) haijafanya utekelezaji mpaka sasa.

    “Miaka minane sasa CDA wamebaki kimya, wamekuwa kikwazo cha ujenzi wa chuo, serikali itusaidie katika hili,” alisema. Kwa upande wake, Askofu wa TAG Kanda ya Dodoma, Steven Mahinyila alisema ujenzi huo ulianza mwaka 2011.
    Alisema ulikwama kutokana na ukosefu wa fedha na ndipo mwaka jana walipata msaada kutoka kwa kampuni ya Priority One ya Marekani, ambayo ilitoa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo.


    Waziri Ndalichako ang’ara bungeni

    By: Unknown On: 23:42
  • Share The Gag
  • BAJETI ya Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi, juzi ilipitishwa kwa namna ya kipekee tofauti na ilivyozoeleka.
    Hali hiyo inatokana na wabunge wa vyama vyote, kuungana na kumtetea Waziri wake, Profesa Joyce Ndalichako, wakitaka apewe muda aboreshe elimu.

    Wabunge wamepitisha bajeti ya Sh trilioni 1.3 huku wakisisitiza serikali iboreshe elimu nchini, ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto mbalimbali.
    Wakati Bunge likiwa limekaa kama kamati, ambako wabunge hushika mshahara wa waziri hadi wapate majibu ya kuridhisha, kwa upande wa wizara hii, waziri husika alitetewa na baadhi ya wabunge wakiwemo wa upinzani.
    Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi ) alilalamikia tatizo la vitabu shuleni, ikiwemo kukosewa kwa mitaala, jambo alilotaka waziri kuzungumzia.
    Akijibu suala hilo, Ndalichako alisema nyaraka alizonazo mbunge yeye hana, hivyo aliomba kupatiwa afanyie kazi, lakini Mbatia alikataa na kusema nyaraka hizo si za siri, kwani zipo kwenye mitandao ya elimu huku kukiwa na vitabu vinavyotumika shuleni.

    Baada ya mjadala wa muda mrefu, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Maendeleo) aliingilia suala hilo na kusema matatizo ya mitaala ni mapana.
    Alishauri suala hilo lirudishwe kwenye Kamati ya Bunge inayoshughulikia suala hilo kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Mbatia alikubaliana na ushauri wa Zitto na kurejesha shilingi, kisha kuendelea na mjadala mwingine.
    Awali, alipoanza kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Profesa Ndalichako aliwashukuru wabunge wote bila kujali tofauti za kisiasa, kwa ushauri mbalimbali waliotoa na kusema atahakikisha anafanyia kazi.
    Waziri huyo aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge na kisha kupewa uwaziri, ikiwa ni mara yake ya kwanza kusoma hotuba ya wizara hiyo, alikuwa akishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama tawala na upinzani.

    Ilipofika wakati wa kuwahoji wabunge, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Zungu alipohoji wanaoafiki waseme ‘Ndiyo’, Bunge lote liliitikia. Hakuna aliyesema ‘Hapana’.
    Aidha Bunge lilizizima kwa makofi kutoka kwa wabunge wote kwa dakika kadhaa, kabla ya kuahirishwa huku kwa umoja wao wakielekea katika kiti alichokaa Waziri Ndalichako kumpongeza. Pia kwenye majadiliano, yapo baadhi ya maeneo ambayo wabunge kwa pamoja, walikubaliana kumpa muda waziri kufanyia kazi.

    Akizungumzia mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala na mifumo mingine ya elimu, Ndalichako alisema katika kuboresha elimu, lazima kuwe na mabadiliko. Alisema katika utawala wake, watafanya mabadiliko kwa kushirikisha wadau wa elimu.
    Aliomba jamii kumuunga mkono, pale wanapofanya mabadiliko. “Wabunge wengi mmechangia kwa uchungu kuhusu ubovu wa elimu nchini, hivyo tumeanza kufanyia marekebisho ili kuboresha elimu; hivyo ni vema kutuunga mkono,” alisema.

    Chanzo HabariLeo.

    Sheria ya Dodoma kuwa Makao Makuu ‘yapikwa’

    By: Unknown On: 23:38
  • Share The Gag

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama

    SERIKALI imeanza kutengeneza sheria ya kutambulisha Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na inatarajiwa kupelekwa bungeni ili kuondoa changamoto ya migogoro baina ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na wananchi.

    Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema hayo bungeni hivi karibuni.
    Alisema kuanzishwa kwa sheria hiyo kutarahisisha katika kuhamia Dodoma pamoja na kuondoa migongano ya kisheria kati ya taasisi mbalimbali inayosimamia masuala ya ardhi mkoani Dodoma, ikiwa ni pamoja na kueleza mipaka ya CDA.

    “Nataka wananchi wa Dodoma waamini kuwa serikali ina lengo la kuhakikisha azma hii ya serikali kuhamia Dodoma inatekelezeka, ikiwa ni pamoja na kuondoa migogoro yote kwa kufuata sheria na taratibu na kunapokuwa na matatizo kwa ushirikiano wetu na wao inaisha,” alisema.
    Alisema watahakikisha migogoro yote inaisha, lakini kwa kufuata sheria ikiwa wananchi wana haki watapata na pale sheria inapowataka wao waipe haki serikali waoneshe ushirikiano.
    Waziri huyo alisema mji wa Dodoma utajengwa kisasa na kuonesha kweli ni makao makuu kama ilivyo miji mingine duniani kwa kuwa kioo cha nchi ilivyo.

    Alisema katika kuonesha nia ya serikali ya kuhamishia makao makuu Dodoma kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge watakutana na wabunge wa mkoa huo na wizara kujadiliana namna bora ya kuondoa changamoto hiyo.
    Alisema watakaa na kutathmini kwa pamoja faida ya kuhamia Dodoma kwa serikali na wizara.
    Mhagama alisema baada ya Mkurugenzi wa CDA kuthibitishwa na Rais wameanza kujipanga kwa lengo la kurudisha mahusiano kati ya mamlaka na wananchi kumaliza migogoro yote iliyokuwa ikijitokeza.
    Alisema amekwishakaa na wafanyakazi wa mamlaka hiyo na kujadili kwa pamoja na kuweka mikakati ya kusimamia mkoa wa Dodoma.

    Chanzo HabariLLeo.

    Watanzania kupata saruji ya bei nafuu

    By: Unknown On: 23:24
  • Share The Gag
  • Sehemu ya kiwanda cha saruji cha Dangote, Mtwara

    KAMPUNI ya saruji ya Dangote imetangaza bei ya saruji yake kuwa itakuwa Sh 10,000 popote, ikiwa ni punguzo.

    Imesema punguzo hilo linalenga kuongeza ushindani kwenye soko la bidhaa hiyo nchini na kuwezesha watanzania wengi kununua saruji.
    Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, SadaLadan-Baki, alisema bei ya saruji yao aina ya 32.5R itauzwa bei hiyo ya Sh 10,000 kwa mfuko wa kilo 50; na saruji ya 42.5R itauzwa Sh 10,500 kwa mfuko wa kilo 50 kutoka kiwandani mpaka popote itakapouzwa, ikiwemo jijini Dar es Salaam, ambako bidhaa hiyo inapatikana.

    Hatua hii imetajwa kuwa inafanya saruji ya Dangote kuwa ya bei nafuu kuliko nyingine, ambazo zinauzwa kati ya Sh 12,500 na Sh 14,000 jijini Dar es Salaam.
    Sada alisema hatua hiyo itasaidia maendeleo ya miundombinu na kutilia mkazo mpango wa taifa wa kukabili tatizo la makazi nchini kutokana na takwimu kuonesha hapa nchini upo uhaba wa nyumba milioni tatu.
    “Tunatambua uhitaji mkubwa wa miundo mbinu bora, na moja ya njia ya kulikabili tatizo hili ni kumfanya kila mtanzania kuweza kuwa na uwezo wa kununua rasilimali za ujenzi kwa kuweka bei mbadala kwa kila Mtanzania,” alisema Sada.
    Uongozi huo wa kampuni ulisema bei hiyo elekezi kati ya Sh 10,000 na 10,500 imelenga jijini Dar es Salaam, ambako ndiko kitovu cha biashara, kinachoangaliwa na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali.
    Hata hivyo, mkakati wao ni kuhakikisha bidhaa hiyo inasambaa nchi nzima na kwa bei ambayo itawezesha wananchi kuimudu.

    Sada alisema katika kuwezesha bei hiyo inazingatiwa, kampuni imejizatiti katika uzalishaji na usambazaji kwa kuhakikisha bidhaa hiyo inakuwapo kwa wingi sokoni, kiasi cha kutosababisha uhaba unaoweza kushawishi wafanyabiashara kupandisha bei yake.
    “Ni soko huria…lakini tutahakikisha tunasambaza mzigo kwa wingi na wasambazaji wanapata saruji kwa bei ya chini, itakayowezesha kuiuza kwa bei elekezi,” alisema baada ya kuulizwa ni namna gani watahakikisha wafanyabiashara wanazingatia bei elekezi.
    Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa kampuni, licha ya Dar es Salaam ambako lipo soko kubwa, maeneo mengine ambayo saruji ya Dangote inasambazwa, ni pamoja na Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Mbeya, Dodoma na Tanga.

    Chanzo HabariLeo.


    Serikali Yapiga Marufuku Pombe Ya Viroba ya Kwenye Mifuko Ya Plastiki

    By: Unknown On: 22:52
  • Share The Gag

  • Mifuko ya plastiki inayofungasha pombe maarufu kama ‘viroba’ imepigwa marufuku na Serikali kuanzia mwakani. 

    Sambamba na hilo Serikali pia, imepiga marufuku moja kwa moja utengenezaji, usambazaji, uingizaji nchini wa mifuko ya plastiki kuanzia mwaka huo.

    Waziri wa Nchi , Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliwaambia wanahabari jana sehemu kubwa ya mifuko hiyo inayotolewa bure imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kikubwa.

    Wakati Makamba akiyasema hayo, Februari mwaka huu Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina aliondoa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki akisema kuwa itaziweka rehani ajira za Watanzania wanaofanya kazi kwenye viwanda vinavyotengeneza mifuko hiyo.

    Pia, Mpina alisema itapunguza kasi ya uwekezaji wa viwanda vilivyowekeza katika bidhaa hiyo.

    Akizungumza katika siku ya Mazingira Afrika, Mkurugenzi wa Mazingira, Dk Julius Ningu alisema maamuzi hayo yamelenga kulinda viwanda vilivyoajiri mamia ya Watanzania, tofauti na nchi nyingine zinazotegemea wazalishaji wa nje ya nchi.

    Makamba akizungumzia uamuzi mpya wa kuzuia mifuko ya plastiki, alisema matumizi ya mifuko inayofungashia vileo na inayotumika katika matumizi mengine husambaa na kuchafua mazingira. Alisema mifuko ya plastiki inatajwa kuziba mifereji na kusababisha mafuriko na athari nyingine za mazingira.

    “Leo (Jana), tumeamua kutangaza ili kuwaanda wahusika wasiendelee kuwekeza katika mifuko hii badala yake wasubiri utaratibu mwingine utakaowekwa na Serikali,” alisema Makamba na kuongeza kuwa:

     “Asilimia kubwa ya uchafu kwenye nyanzo vya maji, mito, maziwa na fukwe za bahari ni mifuko ya plastiki.” 

    Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema Serikali inakamilisha majadiliano ya ndani na baadaye itawahusisha wadau kuhusu dhamira ya kupiga marufuku ya moja kwa moja mifuko hiyo.

    Alifafanua kwamba Serikali itatoa muda kwa walioajiriwa, kujiajiri na kuwekeza kwenye biashara ya mifuko hiyo ili kujiandaa kuacha shughuli hizo na badala yake itawezesha mazingira ya utengenezaji na upatikanaji wa vifungashio mbadala.

    “Kwa wanaotengeza mifuko hii na kuiuza katika soko la nje hatuna tatizo nao waendelee. Ila kwa soko la ndani hawataruhusiwa kufanya hivyo.Zuio hili litakuwa la kisheria siyo kwa maneno,” alisisitiza Makamba. 

    Aliongeza kuwa katika kuonyesha Serikali imedhamiria kupambana na hali hiyo wizara yake imeamua kutuma timu ya watu watano kwenda Rwanda kujifunza namna bora ya kudhibiti matumizi na kuzuia mifuko hiyo tangu mwaka 2008.

    Waziri huyo alitoa wito kwa watengenezaji, wasambazaji na waagizaji wa mifuko hiyo kujiandaa na zuio hilo na katika siku zijazo Serikali itatoa utaratibu na maelekezo ya tarehe ya kuanza zuio huku taratibu nyingine za kina zikifuata ili kuondoa mkanganyiko.

     Katika hatua nyingine, Makamba alisema maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka hayatafanyika kitaifa badala yake wizara imewaelekeza wakuu wa mikoa kufanya maadhimisho katika maeneo yao.

     “Tumewapa miongozo kuhusu utekezezaji wa shughuli hizo za maadhimisho zinazolenga kutoa hamasa ya hifadhi ya mazingira hususan nyanzo ya maji amabayo ni muhimu kwa viumbe hai,” alisema Makamba.

    Kwa mujibu wa Makamba, kauli mbiu ya mwaka huu kitaifa juu ya maadhimisho hayo ni ‘ tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu’aliwashauri na kuwataka Watanzania kutumia siku hiyo kupanda miti, kudhibiti uchomaji wa misitu 

    Ofisa Mwandamizi Mazingira wa Nemc, Arnold Kisagala alisema nusu ya mifuko ya plastiki nchini inazalishwa na kuingizwa kutoka nchi jirani ya Kenya.

    Alisema agizo la Waziri Makamba litawezekana, lakini linahitaji ushirikiano kutoka kwenye sekta zingine kwa kuwa viwanda vingi vya mifuko ya plastiki vipo Kenya.

    "NEMC tayari tulishaanza mazungumzo na wazalishaji kuhusu mifuko ya plastiki,” alisema. 


    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Saudi Arabia yachukizwa na Tangazo la Iran

    By: Unknown On: 22:51
  • Share The Gag
  •   Iran inashutumu maafisa wa Saudia kwa vifo vya mamia ya mahujaji wake
    Saudi Arabia imejibu tangazo la Iran kwamba raia wake hawataruhusiwa kwenda kuhiji Makka mwaka huu,kwa madai ya kwamba mamlaka ya Saudia imetengeneza vikwazo kwa mahujaji wa Iran kushiriki Hijja hiyo.

    Hata hivyo Waziri wa Mambo ya nje wa Saudia Adel al-Jubeir amesema kuwa waumini hao wa Kiislam kutoka nchini Iran,wanahitaji kupewa idhini pia ya kufanya maandamano wakiwa nchiniSaudia jambo ambalo halikubaliki.
    Iran inalaumu maafisa wa Saudia kwa vifo vya mamia ya mahujaji wake vilivyotokea mwakajana walipokwenda kuhiji.

    Professor Mohammad Marandi kutoka chuo kikuu cha Tehran,anasema wa hoja ya Iran, ni kutaka kujiridhisha kama Mahujaji wake watakuwa salama katika Hijja ya mwaka huu
    "Raia wa Iran hawana namna. Maoni ya Wairan ni ya hasira na jazba dhidi ya familia ya Kisaudia. Saudia imewakatalia Wairan matumizi ya Kamera,ambazo ndizo zilizotumika kuonyesha picha za maelfu ya watu waliokufa katika Hijja ya mwaka jana wakiwemo raia wa Iran. Na kwa kuwa Saudia haikulezea mazingira halisi ya vifo hivyo na baadaye ikaomba msamaha,Wairan wanaona bado mazingira hayajawa salama kwao kwa ajili ya Hijja ya mwaka''.

    Professor Marandi amesema vurugu zilizosababisha vifo katika Hijja mwaka jana hazikudhibitiwa vyema na serikali ya Saudia
    "Saudia ilionyesha bayana kutoheshimu mahujaji,familia zao na kwa miili ya waliokufa, jambo ambalo kwa Wairan halikubaliki. Hivyo Wairan wanataka kujua ni maboresho gani yatafanyika mwaka huu ili waweze kuwa salama zaidi,lakini Saudia hawataki kuweka wazi kwamba ni mabadiliko gani yaliyofanyika,na wakati huo huo viongozi wa dini nchini Saudia wanaamini kuwa Wairan si waumini kamili wa dini ya kiislamu''.

    Chanzo BBC.

    Trump aahidi kukomesha malipo ya wageni

    By: Unknown On: 22:42
  • Share The Gag
  • Donald Trump
    Mgombea kiti cha Urais kwa tiketi ya chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump, amehutubia umati wa waendesha pikipiki Jijini Washington.
    Trumph ametoa hotuba hiyo katika maadhimishoya kuwakumbuka maafisa wa polisi wa kiume na wa Kike wa Marekani.
    Amesema watu walioko Marekani kinyume na sheria, wanahudumiwa vyema kuliko maveteran wa kijeshi suala ambalo amesema halitaendelea katika utawala wake.

    Chanzo BBC.

    Walinda amani watano wauawa nchini Mali

    By: Unknown On: 22:39
  • Share The Gag
  • Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanakabiliwa na changamoto ya usalama Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali umesema kuwa walinda amani wake watano wameuawa na wengine wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi lililotokea katikati ya mji wa Mopti. Waathirika wanatokea nchini Togo.Gari lao lilipatwa na moto kabla ya kukanyaga bomu la ardhini,na kisha kulipuka.Waziri wa masuala ya kigeni nchini Mali, Abdoulaye Diop, ametuma salam za rambirambi katika mitandao ya kijamii kwa UN na nchi ya Togo.Vifo vyao vimekuja wakati dunia ikiadhimisha siku yawalinda amani.Mwaka uliopita walinda amani 129 kutoka umoja wa mataifa walipoteza maisha katika nchi 16 wanazofanyia shughuli zao.

    Chanzo BBC.

    Thursday, 26 May 2016

    Exclusive Video : Wema Sepetu Ajitabiria Kifo, Mskie Mwenyewe Hapa..

    By: Unknown On: 23:15
  • Share The Gag

  • Watu wengi hupenda mafanikio au wengi hupenda kua maarufu, mfano mzuri ni mwanadada Wema Sepetu. Ni mmoja wa waigizaji wa kike wachache wenye mashabiki wengi zaidi. Na katika hilo amefungua miradi mingi ikitumia jina lake mfano ni ile TV Show yake ya Wema In My Shoes, Lipstick za Kiss By Wema Sepetu na mwisho kabisa ni Wema Sepetu Application ambayo ameianzisha hata wiki haijaisha.

    Pamoja na watu wengi kuona mambo yanamnyookea star huyo, Wema Sepetu amekua na mawazo yakimsumbua sana kichwani. Kwani siku za karibuni amekua akiota kua siku yake ya kufa imekaribia. Mara nyingi ameota kua kafa na kazikwa.
    Tumebahatika kupata video Exclusive ya Wema Sepetu akielezea ndoto hizo. Unaweza mskiliza hapa chini......
    Credit; UDAKU SPECIAL  

    Spika Job Ndugai (Mb) Afanya Mabadiliko Mengine ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge.

    By: Unknown On: 23:13
  • Share The Gag
  • Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai (Mb) amefanya mabadiliko mengine ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ili kuzingatia maombi ya baadhi ya Wabunge pamoja na mahitaji mapya yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa shughuli za Kamati za Bunge.

    Kwa mujibu wa taarifa yake, mabadiliko hayo yamefanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 116(3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili 2016 ambapo yamehusisha maeneo manne ikiwemo; Kuhamishwa kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati, Kualikwa kwa baadhi ya wajumbe katika Kamati ya Bajeti, Baadhi ya Wajumbe wa kamati ya Haki, Maadili, na Madaraka ya Bunge kuondolewa pamoja na Uteuzi wa wajumbe wapya katika kamati ya Haki, Maadili, na Madaraka ya Bunge.
     
    Mabadiliko hayo ya wajumbe kwenye kamati yanaanza mara moja ambapo orodha ya wajumbe waliobadilishwa kamati na nafasi zao ni kama ifuatavyo; Wajumbe wanaohamishwa Kamati ni pamoja na Mhe. Ezekiel Magoyo Maige, (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Nishati na Madini na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Allan Joseph Kiula (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Omary Tebweta Mgumba (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Sheria Ndigi na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Rhoda Rdward Kunchela (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Masuala ya UKIMWI na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC.

    Wengine ni Mhe. Joseph George Kakunda (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya PIC na kwa sasa anahamia Kamati ya PAC, Mhe. Ahmed Ally Salum (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya PAC na kwa sasa anahamia Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Neema William Mgaya (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na kwa sasa anahamia Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Mhe. Salma Mohamed Mwassa (Mb) ambaye alikuwa katika Kamati ya Bajeti na kwa sasa anahamia Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

    Taarifa inaeleza kuwa, Wajumbe waalikwa katika Kamati ni pamoja na Mhe. Andrew John Chenge (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya Sheria Ndogo, Mhe. Joseph Roman Selasini (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya LAAC, Mhe. Dkt. Dalali Peter Kafumu (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Mhe. Japhet Ngalilonga Hasunga (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya PAC, Mhe. Albert Obama Ntabaliba (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya PIC pamoja na Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb) ambaye yupo katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

    Aidha, Walioondolewa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ni pamoja na Mhe. Dkt. Haji Hussein Mponda (Mb) pamoja na Mhe. Najma Murtaza Giga, (Mb).

    Wanaoteuliwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka Ya Bunge ni pamoja na Mhe. Asha Abdalla Juma (Mb). Mhe. Emmanuel Mwakasaka (Mb) pamoja na Mhe. Augustino Manyanda Masele (Mb).


    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Mr II Sugu Kuhojiwa na CloudsTV Kwa Mara ya Kwanza Toka Amalize Tofauti

    By: Unknown On: 23:09
  • Share The Gag

  • Joseph Mbilinyi ameanza ku-trend kwenye mitandao ya kijamii kupitia tangazo linaloonyesha atahojiwa na CloudsTV Ijumaa May 27 2016, ameanza kutrend hata kabla Interview yenye haijaonyeshwa na hii ni kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ya kuwa hii ni Interview yake ya CloudsTV ya kwanza toka amalize tofauti zake na CMG.

    Mbunge huyu wa Mbeya mjini ambaye ni mmiliki wa single mpya ya Freedom aliipost hii picha kwenye page yake ya Instagram na kuonyesha wazi ameshaachana na tofauti zilizokuwepo na kwa roho safi maisha yanaendelea bila beef : ‘Rapper/MP/ CEO / AUTHOR / BUSINESSMAN /INVESTOR ni kesho asubuhi Freedom to all media, freedom from beefs’

    Credit; UDAKU SPECIAL

    Katibu Mkuu Kiongozi Afanya Ziara Hospitali Ya Rufaa Ya Mkoa Wa Kinondoni Mwananyamala Dar Es Salaam

    By: Unknown On: 23:07
  • Share The Gag
  • SERIKALI imesema itaanza kutumia mbinu mpya kuwadhibiti madaktari na wauguzi wanaoiba dawa za serikali na kisha kuziuza kwenye maduka ya watu binafsi.

    Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi alipoenda kukabidhi magodoro 50 katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dar es Salaam Mwananyala yaliyotolewa na umoja wa makanisa ya Kipentekoste nchini.

    Kijazi alisema mbinu hiyo itasaidia kuwabaini kiurahisi watumishi hao kwani itaendeshwa kwa siri ambapo kila kitengo katika wizara ya afya kutakuwa na mwakilishi atakayesaidia kutoa taarifa pindi atakapoona jambo hilo.

    “Mimi niwatake wenye tamaa waache mara moja haiwezekani dawa serikali inunue kwaajili ya kuwapatia wananchi bure mtu mmoja kwa manufaa yake azipeleke kwa wafanyabiasha kuuza wananchi wakose dawa na kuanza kuhangaika”alisema Kijazi.

    Pia amewataka wauguzi kuhakikisha kwamba malalamiko yanayotolewa na wananchi yanafanyiwa kazi mara moja na kuongeza serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kumnyanyasa mgonjwa.

    Alisema wagonjwa wamekuwa wakitoa malalamiko mengi juu ya huduma zinazotolewa katika hospitali ya Mwananyamala hivyo amewataka watendaji kubadilika ili kuepuka malalamiko yasiyo ya msingi.

    Alisema ni lazima watoa huduma za afya wakazingatia nidhamu na weledi katika utendaji wa kazi kwani hawakulazimishwa kusomea taaluma hiyo na kuongeza kuwa fani zipo nyingi hivyo ambaye anaona hawezi kufanya yanayotakiwa aachie wengine.

    Pamoja na hayo amezitaka hospitali zote kuanzisha dawati la malalamiko ili wanaohudumiwa wapate pakusemea pindi wanapofanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwa ni pamoja na kucheleweshewa huduma au kuombwa fedha ili kuwahishiwa huduma ili hali ikiwa ni haki yao.

    Hata hivyo ametaka madawati hayo kuwa wazi masaa 24 ili wananchi wapate muda mwingi wakujieleza na sio kusubiri kuelezea hisia zao pale wanapoona viongozi wakitembelea vituo hivyo.

    Kijazi alitembelea wodi mbalimbali hospitalini hapo ikiwamo wodi ya wazazi, Wanaume, Watoto, Wanawake na watoto njiti ambapo alipata kujionea baadhi ya wagonjwa wakilala zaidi ya mmoja kwenye kitanda kimoja kutokana na kukosekana kwa vitanda.

    Naye Mganga mkuu msaidizi katika hospitali hiyo Delila Moshi alieleza matatizo yanayoikabili hospitali hiyo kuwa ni pamoja na madeni ambapo inadaiwa stahiki za watumishi Sh. milioni 500 ambazo ni fedha za likizo kwa wafanyakazi, Sare za kazi, Nyumba na posho za masaa ya ziada.

    Moshi alisema hospitali hiyo pia ina ukosefu wa vifaa vya kisasa kama CT Scan hali inayosababisha wagonjwa kupewa rufaa ya kwenda muhimbili kwaajili ya vipimo zaidi, Ukosefu wa chumba cha uangalizi wa wagonjwa mahututi (ICU) na Daktari bingwa wa mifupa na wagonjwa wa dharura.

    Tatizo lingine ni wingi wa wagonjwa wa msamaha ambapo kwa kuanzia januari hadi desemba mwaka jana zaidi ya bilioni 2 zilitumika huku kwa mwezi wakitoa matibabu ya zaidi ya milioni 100 bure.



    ==

    Credit; Mpekuzi Blog

    Shilingi Bilioni 3 na Mali za Bilioni 10 zataifishwa na TRA Kutoka kwa Wakwepa Kodi Bandari Kavu ya Azam

    By: Unknown On: 23:01
  • Share The Gag


  • Mamlaka ya kukusanya kodi TRA kupitia madalali wa Yono Auction Mart wamekusanya mali za bilioni 3 pamoja na kutaifisha mali za bilioni 10 kutoka kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 329 kupitia bandari kavu ya Azam bila kulipa kodi na bado wanaendelea na msako bara na visiwani.

    Madalali hao wamesema watu walipe kodi na watoe risiti za elekroniki la sivyo mali zitakamatwa.
     

    Credit; UDAKU SPECIAL 

    Klabu ya Yanga kuchagua uongozi

    By: Unknown On: 22:58
  • Share The Gag
  • Washabiki wa watoto wa Jangwani
    Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetangaza leo Mei 27, 2016 kuanza kwa mchakato wa kuchukua fomu za kugombea uongozi katika Klabu ya Young Africans ya Dar es Salaam inayotarajia kufanya uchaguzi tarehe 25 Juni mwaka huu.
    Nafasi zinazogombewa ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wanane wa Kamati ya Utendaji.
    Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Aloyce Komba fomu zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Mwisho wa kuchukua fomu ni tarehe 31 Mei, 2016.

    Chanzo BBC.

    Rais Magufuli Atoa Mchango wa Milioni 10 Kusaidia Matibabu ya Mwafunzi Aliyepata Upofu

    By: Unknown On: 22:57
  • Share The Gag

  • Rais John Magufuli ametoa mchango wa Sh. milioni 10 kwa ajili kusaidia matibabu ya mwanafunzi Bernadetha Msigwa aliyepata upofu hivi karibuni.

    Msichana huyo anayesoma mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, ni miongoni wa wasichana ambao tatizo lake limeibuliwa kupitia kampeni ya Kipepeo, iliyoanzishwa na kampuni ya Clouds Media, Mei Mosi mwaka huu.

    Kupitia matangazo yanayorushwa na kampuni hiyo, Rais Magufuli baada ya kusikia tatizo la Msigwa, ambaye pia picha yake imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, akiwaomba Watanzania wamsaidie mchango wa fedha ili aweze kutibiwa. aliguswa na kuamua kutoa mchango huo.

    Meneja wa kipindi cha 360 kinachorushwa kila siku za wiki asubuhi na televisheni ya Clouds, Hudson Kamoga alisema baada ya Rais kuona tangazo hilo, lililorushwa muda mfupi kabla ya kuanza uchambuzi wa magazeti, alimpigia simu.

    “… Alisema ameguswa na stori ya Bernadetha, hivyo yeye na familia yake watachangia Sh10 milioni ili kumsadia,” alisema Kamoga.

    Kamoga ambaye aliwahi kupigiwa simu na Rais Magufuli akiwa katika ya kipindi hicho na kuwasifu yeye na wenzake wanaokiendesha, alisema baada ya muda mfupi, Rais alimwagiza msaidizi wake apaleke mchango huo.

    “Zilipita kama dakika 30 hivi au 45, akawa amemtuma mtu alete zile hela,” alisema Kamoga.

    Mbali na Rais Magufuli, Kamoga alisema viongozi wengine walioguswa na tatizo la Msigwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ambaye alikuwa mgeni kwenye kipindi cha 360 jana asubuhi, alichangia Sh2 milioni.

    Pia, Manaibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Anthony Mavunde Dk Abdallah Posi kila mmoja alichangia Sh1 milioni na Mkurugenzi wa Kampuni ya TSN, Farough Baghozah alichangia Sh3 milioni.

    Kamoga alisema mwitikio wa Watanzania umekuwa mkubwa na hadi jana, michango iliyokuwa imetolewa ilikuwa zaidi ya Sh30 milioni anazohitaji Msigwa kwa ajili ya matibabu.

    Kamoga alieleza kuwa msichana huyo alianza kupata maumivu makali ya kichwa mwaka huu na baada ya muda, alipoteza uwezo wa kuona.

    “Hakuzaliwa kipofu. Amepata tatizo mwaka huu, wakiwa chuo mwaka wa tatu,” alisema Kamoga.

    Alisema aliomba msaada kwao hivyo kupitia kampeni ya kipepeo, tatizo lake limefahamika na wengi na Watanzania wamemchangia ili aweze kutibiwa na kuona tena.

    Credit; UDAKU SPECIAL 

    Sekondari Kongwe za Umma Kurejeshewa Makali Yake

    By: Unknown On: 22:34
  • Share The Gag
  • Serikali imeeleza mkakati wa kuzirudisha shule 33 maarufu katika ubora wake ili ziweze kufanya vizuri kama ilivyokuwa zamani.

    Mkakati huo ulielezwa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni. 
    Alisema shule hizo zilipokuwa nzuri zikitoa elimu bora, zilizalisha vipaji vingi, akiwamo yeye aliyesoma katika mojawapo.Alisema katika awamu ya kwanza, shule 33 zitakarabatiwa.

    Alizitaja shule hizo kuwa ni Ihungo, Ilboru, Kilakala, Mwenge, Msalato, Mzumbe, Ngaza, Pugu, Same, Tabora Boys na Tabora Girls.

    Nyingine ni Azania, Jangwani, Kantalamba, Mpwapwa, Tosamaganga, Malangali, Milambo, Nangwa, Kibiti, Minaki, Ifakara, Songea Boys, Ndanda, Kigoma, Kibaha na shule za ufundi za Bwiru Boys, Ifunda, Iyunga, Moshi, Mtwara, Musoma na Tanga.


    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Dada wa Bilionea Msuya Auawa Kinyama Dar

    By: Unknown On: 22:29
  • Share The Gag
  • Mtumishi wa Wizara ya Fedha, Aneth Msuya (30) ambaye ni mdogo wa Bilionea Erasto Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi 22 KIA, ameuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake eneo la Kigamboni jijini Dar Es Salaam.

    Mmoja wa ndugu wa familia hiyo, Shujaa Khamis, jana alithibitisha kuuawa kwa Aneth, lakini alikataa kuingia kwa undani.

    “Ni kweli wamemchinja usiku wa kuamkia leo (jana) na hapa nipo kwenye msiba hapa nyumbani (Mererani) kwa baba. Tumeambiwa wamechukua Tv tu,” alisema.

    Hata hivyo, Khamis alikataa kueleza lolote kama wana mashaka na mauaji hayo zaidi ya kuliomba Jeshi la Polisi nchini, kuchunguza kiini cha mauaji hayo na kuwasaka waliohusika.

    Habari nyingine kutoka Wizara ya Fedha, ziliwakariri baadhi ya watumishi wakisema wamepata taarifa za msiba huo, lakini hawajapewa taarifa rasmi.

    “Tuna taarifa tunazisikia sikia kuwa ameauawa, lakini jana (juzi) tulikuwa naye kazini ila leo (jana) ndiyo tunasikia amechinjwa na watu wasiojulikana. Imetusikitisha sana,” alisema mmoja wa watumishi hao ambaye hakutaja jina kwa kuwa si msemaji.

    Kamanda wa mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Andrew Satta alipofutwa jana kuthibitisha taarifa za mauaji hayo alisema yuko kwenye kikao.


    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Silaa Adai Wafuasi wa Chadema walitishia Kuchoma Nyumba yake

    By: Unknown On: 00:00
  • Share The Gag

  • ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Ukonga, Jerry Silaa (CCM) amedai kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walimtishia kuchoma moto nyumba yake wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana.

    Silaa alieleza hayo jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati akitoa ushahidi wa kesi ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo, Mwita Waitara (Chadema).

    Alitoa ushahidi huo kwa njia ya kiapo baada ya Jaji Fatuma Msengi kutupilia mbali pingamizi la upande wa walalamikiwa waliokuwa wanapinga kupokewa kwa kiapo hicho kwa kuwa kina mapungufu kisheria.

    Katika kiapo hicho, Silaa anaeleza kuwa, Oktoba 27 mwaka jana katika kituo cha kujumlishia kura cha Pugu Sekondari, kulikuwa na idadi kubwa ya wapiga kura wa Chadema wakiwa wamesimama mita 20 kutokea usawa wa kituo hicho.

    Alidai kuwa wafuasi hao walianza kuwatishia Mawakala na Msimamizi wa Kituo, jambo lililosababisha Polisi washindwe kufanya kitu zaidi ya kuwaonya, ndipo mjibu maombi wa pili na wenzake wakasema hawatopokea matokeo na watachoma moto nyumba yake pamoja na kituo hicho.

    Silaa ambaye aliwahi kuwa, Meya wa Manispaa ya Ilala, alidai hadi Oktoba 27, baadhi ya vituo vilikuwa havijakusanya matokeo jambo lililosababisha aandike barua kwenda kwa Msimamizi wa Kituo kuomba mchakato wa kuhesabu kura urudiwe.

    Credit; UDAKU SPECIAL

    Wednesday, 25 May 2016

    Rais Magufuli na Mkewe Waguswa na Stori ya Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Aliyepofuka Macho..Waamua Kumchangia Mil 10 Akatibiwe

    By: Unknown On: 23:57
  • Share The Gag


  • Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DktJohn Pombe Magufuli, Mkewe Mama Janeth Magufuli na familia yake kuahidi kuchangia Milioni 10 kwaajili ya matibabu ya #Kipepeo Bernadeta Msigwa mwakilishi kutoka ofisi ya Rais Bw. Ngusa Samike amefika katika ofisi za CloudsMediaGroup na kukabidhi fedha hizo. Vilevile Mheshimiwa Rais ametoa ujumbe kwa Kipepeo Bernadeta kuwa amtumainie Mungu kwani ndiye muweza wa kila kitu. Katika upande mwingine Naibu wa Waziri wa Wizara ya Kazi, Vijana na Ajira Mh. Anthony Mavunde amechangia Shilingi Milioni 1.
    Kama umeguswa na unahitaji kuchangia au unataka maelezo zaidi kuhusu jinsi ya kumsaidia piga namba 0742848729. Pia unaweza kuangalia story yake kamili kwenye account hii ya Instagram@BernadetaMsigwa.
    Asante sana Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
    Credit; UDAKU SPECIAL 

    Video : Lulu Michael Akubali Kua Anavaa Matambala ya Kuongeza Makalio

    By: Unknown On: 23:55
  • Share The Gag



  • Siku za hivi karibuni kumetokea mabifu mengi sana ya wasanii wetu wa kike hapa Bongo. Mabifu makubwa ambayo yamemake headline sana ni ya ya Shilole na Vanessa Mdee na upande wa pili ni Lulu na video queen Giggy Money.

    Giggy Money siku za karibuni amekua akitofautiana na wasanii wengi na kwa sasa kaamua kulinukisha na kuanzisha bifu na Lulu. Giggy amekua akijitamba kua anamzidi maisha mazuri Lulu hasa katika upande wamavazi na kuvaa matambala ili aongeze tako.

    Katika kauli moja Giggy alisikika akisema kua Lulu ni bingwa wa kuvaa nguo za matangazo. Baada ya Lulu kutuhumiwa hayo aliamua kufunguka kwa ufupi na kujibu tuhuma hizo.

    Unaweza mskiliza kwa kutazama video yake hapa chini.

    Credit; UDAKU SPECIAL 

    Video: Chid Benz Adaiwa Kutoroka Sober House

    By: Unknown On: 23:52
  • Share The Gag

  • Wakati wadau wa muziki wakifahamu kuwa Msanii wa Muziki wa Hip Hop Bongo, Rashid Makwilo ‘Chid Benz’ yuko katika kituo cha kusaidia waathirika wa madawa ya kulevya ‘sober house’ kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, inadaiwa jamaa alishatoroka kitambo na sasa yuko kitaa.

    Taarifa iliyotua kwenye meza ya dawati hili ilidai kuwa, Chid alitoroka kituoni hapo baada ya kushindwa kuhimili mazingira yalikuwepo hivyo akaona bora arudi mtaani kwa staili ya liwalo na liwe.

    Baada ya kupata taarifa hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita waandishi wetu walitinga Bagamoyo na kukutana na meneja wa kituo hicho, Tumaini Majura ambaye alithibitisha kuondoka kwa Chid akiwa bado anaendelea kupatiwa matibabu. Sehemu ya mahojiano kati ya Risasi na meneja huyo ni hii;
    Chid-Beenz_fullRisasi: Kwani Chid Benz ameishi hapa kwa muda gani?
    Tumaini: Ni siku 28 lakini alitakiwa kukaa kwa muda wa angalau miezi mitatu ili kurudi katika hali yake ya kawaida.

    Risasi: Ilikuwaje sasa mpaka akaondoka kabla hajawa sawa?
    Tumaini: Nafikiri ni uamuzi wake binafsi maana siku moja meneja wake (Babu Tale) alikuja kumjulia hali, alipotaka kuondoka aling’ang’ania kuondoka naye. Sisi pamoja na Tale tulimsihi sana kubaki lakini alikataa.

    Risasi: Hali ilikuwaje kwa meneja wake wakati Chid anang’ang’ania juu ya jambo hilo?
    Tumaini: Kiukweli hakuwa akitaka aondoke maana mara kwa mara alikuwa anamsihi kuwa mvumilivu ili amalize angalau miezi mitatu na ampeleke kwenye shoo za muziki ndani na nje ya nchi, lakini Chid hakujali hayo. Kwa hiyo siwezi kusema alifurahia juu ya jambo hilo.
    Risasi: Maisha yake ya kawaida yalikuwaje na wenzake?

    Tumaini: Hayakuwa mabaya sana japo alikuwa mzito kushiriki kwenye ishu za usafi na vitu vingine. Muda mwingi alipenda kupumzika na kuandika mistari. Lakini kuna kipindi alikuwa akijaribu kuhamasisha wenzake wagomee kitu fulani. Sisi tulikuwa tunamchukulia kama mtu wa kawaida aliyekuwa anahitaji msaada kutoka kwa viongozi.

    Baada ya mahojiano hayo, waandishi wetu waliamua kumtafuta Chid Benz, alipopatikana alikataa kuzungumzia suala hilo huku akisisitiza kuwa lolote kuhusu yeye atafutwe Babu Tale.

    Alipopatikana, Babu Tale alisema: “Sitaki kusikiliza wala kuzungumza lokote kuhusu Chid, muda ukifika nitaongea ila kwa sasa niacheni tu.”


    Angali Video Hapa:


    Chanzo:Global Publishers

    Credit; UDAKU SPECIAL

    CCM Waituhumu Chadema Arusha Kugawa Miradi Kwa Kupendelea Maeneo Waliyoshinda

    By: Unknown On: 23:42
  • Share The Gag
  • CCM Mkoa wa Arusha, imeziomba halmashauri tano kati ya saba zinazoongozwa na Chadema, kugawa miradi ya maendeleo kwa usawa katika maeneo yao ili kuunga mkono msimamo wa Rais John Magufuli wa kuhudumia wananchi bila ubaguzi wa itikadi za vyama.

    Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Laizer alitoa kauli hiyo jana katika mkutano na viongozi wa chama hicho na Serikali katika kata za Lolksale na Lemoot wilayani Monduli, wakati wa ziara yake ya kuhamasisha utekelezaji wa ilani ya CCM na kukiimarisha chama hicho. 

    Alisema katika halmashauri zinazoongozwa na upinzani alikopita amegundua kuwapo kwa utoaji wa miradi usio na uwiano, kwa kubagua baadhi ya kata zinazoongozwa na madiwani wa chama tawala, hali inayoweza kuzua malumbano.

    Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Calist Lazaro alisema malalamiko hayo ya CCM hayana msingi kwa kuwa madiwani wa chama hicho katika halmashauri zote wanajua wajibu wao na hakuna upendeleo wowote.

    Lazaro ambaye pia ni Meya wa Jiji la Arusha, alisema CCM haitengwi kwani haina uongozi katika kata nyingi. Alisema kati ya kata 24 CCM imeshinda moja, hivyo wanapoona kazi zinafanyika kwenye kata hizo wanadhani ni upendeleo.

    Madai ya Laizer 
    Mwenyekiti huyo wa CCM alisema viongozi wa Chadema wanaoendekeza siasa hadi sasa baada ya uchaguzi kumalizika, hawatendi haki kwa kuwa kuchagua au kuchaguliwa ni hiari ya kila mtu na kamwe mwananchi hapaswi kuhukumiwa kwa uamuzi aliofanya kidemokrasia.

    “Kwa nini wao viongozi wa chini wanaendekeza ubaguzi wakati kiongozi mkuu wa nchi ambaye ni Rais anaendelea kusisitiza kutoa huduma kwa wananchi pasipo na ubaguzi?” alihoji na kuongeza:

    “Kama Rais Magufuli angeamua kuzinyima fedha baadhi ya halmashauri zinazoongozwa na vyama vya upinzani, kungekuwa na madhara makubwa hivyo wapinzani wajirekebishe.”

    Laizer aliwataka wananchi wa kata na halmashauri hizo zinazokabiliwa na matatizo hayo, kutokuwa wanyonge kwa kuwa wanaye baba ambaye ndiye Rais anayeonyesha hana ubaguzi na wala si muumini wa masuala ya vyama vya siasa, baada ya yeye kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

    Mwenyekiti huyo anaendelea na ziara wilayani Monduli ikiwa ni wilaya yake ya nne, baada ya kupita katika wilaya za Meru, Arumeru na Karatu kwa kazi hiyo ya uhamasishaji wa utekelezaji wa ilani ya chama chake.


    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Tozo za Daraja la Nyerere kupitiwa

    By: Unknown On: 23:39
  • Share The Gag

  • Daraja la Nyerere.

    SERIKALI inatarajia kufanya mapitio ya viwango vya tozo, zinazotumika kwa vyombo vya usafiri vinavyopita kwenye daraja la Nyerere lililoko Kigamboni jijini Dar es Salaam. Hatua hiyo imekuja kutokana na maoni na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa daraja hilo juu ya ukubwa wa viwango hivyo, vilivyoanza kutumika Aprili 16 mwaka huu.

    Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (anayeshughulikia Ujenzi), Joseph Nyamhanga, alisema tangu waanze makusanyo, wamepokea ushauri na maoni na kisha watafanya mapitio ya viwango.
    “Kwa sasa bado ni mapema sana, hatuna hata mwezi mmoja toka tuanze kupokea tozo, tunaendelea kupokea ushauri na baada ya mwezi mmoja tutakaa na kufanya mapitio tena kuangalia viwango hivyo,” alisema Nyamhanga.

    Nyamhanga alisema Serikali itafanya tathmini kuona kama kweli viwango vinavyotumika sasa ni mzigo kwa watumiaji wa daraja na ikionekana malalamiko ni mengi na inahitajika kupunguza, itafanya hivyo.
    “Ushauri wangu kwa wananchi wanaotumia daraja hilo ni kwamba wavute subira wakati tunaangalia hali ikoje, lakini waelewe duniani kote barabara za kulipia na hata madaraja yapo, hii ni mfumo ambao upo duniani kote,” alisema Nyamhanga.
    Aidha alisema Wizara pia itaangalia namna ya kuweka mfumo ambao utawanufaisha zaidi watumiaji wa daraja hilo wa mara kwa mara kuwezesha kuwapo utaratibu wa kulipia tiketi za msimu zitakazotoa nafuu.
    Awali, wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya watumiaji wa daraja, hususani madereva wa daladala, walilalamikia utaratibu uliopo wa kulipia kila wanapopita katika daraja na kusema inawagharimu zaidi kuliko mapato yao kwenye biashara hiyo.

    “Kwa siku moja tunajikuta tunaingia gharama kubwa mno kwa sababu sisi tunapita hapa darajani mpaka mara 14 kwa siku na kila tukipita tunatakiwa kulipa Sh 7,000, hii siyo biashara kabisa,” alisema Maro Lyoki ambaye ni kondakta wa daladala.
    Dereva wa daladala, Jacob Michael alisema fedha ambayo inapatikana kwa siku katika biashara hiyo haitoshi kulipia kuvuka katika daraja hilo na fedha ya kumpa mwenye gari. Aliomba serikali kusikiliza kilio chao cha kupunguza viwango hivyo linufaishe watu wengi.

    Kwa upande wa waendesha pikipiki za biashara maarufu kama bodaboda, baadhi ya waliozungumza na gazeti hili, walisema wamelazimika kuongeza nauli kutoka Sh 2,000 hadi Sh 3,000 kutoka darajani hadi Kituo cha Uhasibu kwa ajili ya kufidia gharama za daraja.
    Viwango vya sasa Katika daraja hilo, watembea kwa miguu wanapita bure, wenye baiskeli wanalipa Sh 300, pikipiki Sh 600, mikoteteni, guta, bajaj na magari madogo yanatozwa Sh 1,500, magari aina ya ‘pick up’ Station Wagon na yanayozidi tani mbili ni Sh 2,000.

    Mabasi yanayobeba abiria wasiozidi 15 (mini bus) yanatozwa Sh 3,000, mabasi yanayobeba abiria kuanzia 15 hadi 29 Sh 5,000 huku mabasi yanayobeba abiria zaidi ya 29 yanatozwa Sh 7,000.
    Ttrekta na magari yenye tani mbili hadi saba, yanalipa Sh 7,000, yenye tani saba hadi 15 wanalipa Sh 10,000, tani 15 mpaka 20 wanalipa Sh 15,000 na yenye tani 20 mpaka 30 yatalipia Sh 20,000.
    Matrekta yenye matrela, magari makubwa yenye uzito wa tani saba hadi 15 yanatozwa Sh 10,000 wakati magari yenye uzito wa tani 15 hadi 20 yanatozwa Sh 15,000. Magari yote ya serikali na taasisi za umma yanatakiwa kulipa tozo kama ilivyobainishwa isipokuwa yale yenye namba za jeshi (Magereza - MT, Polisi - PT, JWTZ, Zimamoto) na magari ya wagonjwa.

    Hivi karibuni, baadhi ya wabunge wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, walishauri viwango hivyo vya tozo, viangaliwe upya hususani kwa daladala zinazopita.
    Pia walishauri serikali itumie mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji mapato kwa watu wanaopita darajani hapo. Miongoni mwa waliotaka kuangalia upya viwango ni Mbunge wa Mvomero, Suleiman Sadick Murrad (CCM) aliyesema Sh 7,000 zinazotozwa kwa daladala zinawaumiza.

    Alitaka mapato ya watumiaji hao, yazingatiwe badala ya kuwakatisha tamaa kutumia daraja hilo. Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Mageleri alisema viwango hivyo ni vikubwa. Alisema daraja lilipozinduliwa, wananchi waliona ni mkombozi wao, wataondokana na adha ya vivuko iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu. “Baada ya kutangazwa viwango hivyo imekuwa adha kubwa,” alisema.

    Chanzo HabariLeo.

    Wema Sepetu: Ipo Siku na Mimi Nitaitwa Mama

    By: Unknown On: 23:38
  • Share The Gag
  • Msanii wa filamu nchini Wema Sepetu ambaye siku za karibuni ilisemekana alipata ujauzito na kisha baadaye ujauzito huo kuharibika amefunguka na kuonyesha bado hajakata tamaa na anaamini ipo siku na yeye atapata mtoto kama watu wengine wanavyopata

    Kupitia Account yake ya Instagram Wema Sepetu alipost picha akiwa na mama yake mzazi na kuweka maneno yalisomeka kuwa 'iko siku na mimi nitaitwa Mama', jambo ambalo liliibua hisia za mashabiki zake na wengine kuanza kumfariji kuwa Mungu yupo na anasikia kilio chake na wengine wakiendelea kumtia moyo kuwa asijali kweli upo wakati na yeye atakuwa mama na kupata mtoto.

    "Muombe Mungu Wema Sepetu hata sisi wanawake wenzako tunaumia sana kuona unatukanwa kisa mtoto, tunakuombea Mungu akujualie mtoto wako usisemezane nao hao watu wanakuongelea vibaya" Lovenes France


    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Kampuni 52 zajitosa kusambaza umeme

    By: Unknown On: 23:34
  • Share The Gag
  • Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.

    KAMPUNI 52 zimetuma maombi kuwekeza kwenye sekta ya umeme nchini. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo juzi, alipozungumza na Watanzania waishio Zambia katika mkutano uliofanyika ubalozi wa Tanzania jijini Lusaka.
    “Haya maombi yamekwishapokelewa na wenye makampuni wamekwishahojiwa, kuangalia uwezo walionao katika suala zima la uwekezaji wanaotaka kuufanya, na tukiwapata wenye uwezo na wenye nia ya dhati watapatiwa miradi ya kuiendesha,” alisema.

    Aliwataka watanzania hao waishio Zambia, watumie fursa ya uwepo wao kutafuta marafiki ambao wanaweza kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali nchini. Alisema serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu wakati wananchi wanahitaji kupatiwa huduma muhimu.
    “Serikali peke yake haiwezi kufanya kazi ya uwekezaji kwa hiyo tunahitaji kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo na ndiyo maana kule kwenye mkutano nimewaeleza washiriki kwamba milango ya uwekezaji Tanzania iko wazi,” alisema.

    Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika, kutawezesha wananchi wengi zaidi kujiingiza katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuinua uchumi wa nchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
    Alisema malengo ya Serikali ya awamu ya tano ni kuona kuwa nchi inakuwa na mitambo mingi ya kuzalisha umeme na umeme wote unaozalishwa na mitambo hiyo inaunganishwa na gridi ya taifa kuondokana na tatizo la mgao wa umeme nchini.
    Alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati vikiwemo gesi asilia, makaa ya mawe, madini ya urani, maji, upepo, nishati ya joto kutoka ardhini na nishati inayotokana na vinyesi vya mifugo, ambayo alisema vinatumika kwa watu wachache (siyo kitaifa).

    Alisema kupatikana kwa gesi asilia nchini kumeleta neema, ambapo mabomba ya gesi yamekwishajengwa kutoka Mtwara hadi Kinyerezi na kutoka Kilwa- Songosongo hadi Dar es Salaam. “Sasa hivi kuna utafiti unaendelea juu ya uwezekano wa kusambaza gesi ya kupikia majumbani.
    Tumeanza pale Mikocheni (DSM) na sasa hivi wanafanya utafiti mwingine kule Mtwara ili wananchi waweze kutumia gesi hii kupikia badala ya mkaa,” alisema. Akielezea kuhusu uwekezaji kwenye makaa ya mawe, Waziri Mkuu alisema serikali imelenga kutumia makaa ya mawe ili kuendeshea mitambo ya kwenye viwanda vikubwa, badala ya kutumia umeme au mafuta ya dizeli kama inavyofanyika sasa.

    “Baadhi ya wenye viwanda wanabadilisha mifumo ya kuendeshea mashine zao ili iweze kuendana na teknolojia ya makaa ya mawe pindi tu uchimbaji ukishika kasi,” alisema. Akifafanua kuhusu juhudi za serikali katika kusambaza nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), vijiji zaidi ya 3,000, kati ya vijiji 12,000 vilivyopo nchini, vimefikiwa na nishati ya umeme.
    “Tulianza na REA awamu ya kwanza, awamu ya pili na sasa tunaenda awamu ya tatu. Hata mkipiga simu kwa ndugu zenu vijijini, mtakuta katika kila kata kuna vijiji kati ya vinne hadi vitano ambavyo vimefikiwa na nishati ya umeme kupitia mradi wa REA,” alisema. Waziri Mkuu alirejea nchini jana.

    Chanzo HabariLeo


    Rais Magufuli Mgeni Rasmi Mkutano Wa CRB

    By: Unknown On: 23:30
  • Share The Gag
  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa mashauriano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Nchini (CRB) leo tarehe 26 Mei, 2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

    Mkutano huo wa mwaka wa mashauriano na wadau wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi unatarajiwa kuhudhuriwa na  zaidi ya Makandarasi na wadau wa Sekta ya Ujenzi wapatao 1000 na utafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 26 Mei, 2016 hadi tarehe 27 Mei 20l6.

    Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Juhudi za Makusudi za Kukuza Uwezo wa Makandarasi Wazalendo kwa Maendeleo Endelevu ya Kiuchumi; Changamoto na Mustakabali Wake’.

    Lengo la mkutano huu ni kuwakutanisha wadau wa Bodi ya Usajili Makandarasi na Sekta ya Ujenzi ili kujadili changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo Makandarasi Wazalendo.

    Imetolewa; 
    Eng. Joseph M. Nyamhanga
    Katibu Mkuu (Ujenzi)
    Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano



    ==

    Credit; Mpekuzi Blog