Veronica Romwald na Allen Msapi (GHI), Dar es Salaam
MASHINE ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ijulikanayo kama Magnetic
Reasonance Imaging (MRI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
imeharibika tena baada ya kufanya kazi kwa siku mbili, tangu
ilipofanyiwa matengenezo na Kampuni ya Philips.
Mashine hiyo ilifanyiwa matengenezo kutokana na shinikizo la Rais Dk.
John Magufuli aliyefanya ziara ya kushtukiza hospitalini hapo na
kuamuru zifanyiwe marekebisho haraka.
Katika ziara yake hiyo, Dk Magufuli alishangaa kuona wagonjwa wamekaa
hospitalini hapo kwa zaidi ya miezi miwili bila kutibiwa, kutokana na
mashine hiyo kuwa mbovu.
MRI ni mashine inayotumia sumaku kupiga picha badala ya mionzi.
Wataalamu wa masuala ya afya wanasema ni mashine ambayo inapiga picha
zenye ubora zaidi kuliko zilizopigwa na mashine ya CT Scan.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel
Aligaesha, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa, huduma za
uchunguzi zinazofanywa na mashine hiyo zimesitishwa hadi hapo
itakapotangazwa tena.
“Mapema wiki iliyopita tuliwatangazia wananchi kwamba huduma za MRI
zimeanza kutolewa baada ya mashine hiyo kutengenezwa. Katika taarifa
hiyo tuliwaeleza kuwa matengenezo ya kifaa kingine cha CT- Scan yalikuwa
yakiendelea.
“Hata hivyo baada ya mashine ya MRI kufanya kazi Novemba 11 na 12,
mwaka huu ilionekana kuna hitilafu ya kiufundi ambayo inahitaji
matengenezo zaidi hali iliyotulazimu kusimamisha kufanya kazi kuanzia
Novemba 13 mchana,” alisema.
Alisema uongozi wa hospitali hiyo umeshawasiliana na kampuni ya
Philips ambayo ina mkataba wa kuzifanyia matengenezo mashine hizo ili
kurekebisha hitilafu zilizojitokeza.
Created
Saturday, 7 January 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment