WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameitaka kampuni ya TANCOAL Energy inayochimba
makaa ya mawe kwenye mgodi wa Ngaka itimize masharti ya mkataba
iliouingia na Serikali mwaka 2008.
Kampuni
ya TANCOAL iliundwa Aprili 3, 2008 na kampuni tanzu ya Atomic Resources
Limited ambayo wakati huo ilikuwa ikijulikana kama Pacific Corporation
East Africa (PCEA) na kwa sasa inaitwa Intra Energy (T) Limited ambayo
hisa zake ni asilimia 70 na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lenye
asilimia 30 ya hisa.
Ametoa
kauli hiyo Ijumaa, Januari 6, 2017 mara baada ya kutembelea mgodi huo
na kukagua shughuli za uzalishaji. Mgodi wa Ngaka uko wilaya ya Mbinga,
mkoani Ruvuma na unamilikiwa na kampuni ya TANCOAL kwa ubia baina ya
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na kampuni ya Intra Energy
Corporation ya Australia.
Kwa
mujibu wa mkataba huo, ilikubaliwa kwamba mbali ya kuzalisha makaa ya
mawe, kampuni hiyo ilipaswa kuzalisha umeme wa megawati 400 kutokana na
makaa hayo. TANCOAL ina migodi miwili; Mbalawala na Mbuyura ambao
umetengwa mahsusi kwa ajili ya kuzalisha umeme.
“Kwenye
mkataba tulikubaliana kuwa mtazalisha umeme lakini hadi hadi leo
hamjaanza mnadai kuwa TANESCO wanawachelewesha. Nitafuatilia nione kama
ni wao au la ili tujue ukweli,” alisema.
Kwa
mujibu wa mikataba huo, TANCOAL ilipaswa kugharamia dola za Marekani
milioni 14.49 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja ili kuwezesha
malori makubwa na madogo yaweze kufika mgodini na kusomba makaa hayo.
“Mlisema
mngetengeneza barabara lakini hadi sasa bado hamjafanya hivyo na ndiyo
maana malori yanaishia kule. Yangefika hapa moja kwa moja, mngeweza
kubaini kwa urahisi mahitaji ya makaa ya mawe ni kiasi gani,” alisema
Waziri Mkuu.
Hivi
sasa, malori ya kutoka mgodini yanashusha makaa yaliyochimbwa kwenye
eneo lililokodishwa na TANCOAL la Amani Makolo ambalo liko umbali wa
km.55 kutoka mgodini na malori makubwa yanapakia makaa hayo kutoka
kwenye eneo hilo jambo ambalo linazidisha gharama za usafirishaji.
Kwa
mujibu wa mkataba huo, TANCOAL ilipaswa kuwekeza mtaji wa Dola za
Marekani milioni 82 lakini hadi sasa imewekeza kiasi cha dola milioni 14
ambazo ni sawa na asilimia 12 tu ya ahadi iliyotolewa.
“Makubaliano
yalikuwa ninyi mtawekeza Dola za Marekani milioni 81.69 lakini hadi
sasa mmetumia dola za Marekani milioni 14, hamjafikia hata nusu,”
alisema Waziri Mkuu.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Dk.
Samuel Nyantahe afuatilie kwa makini mambo yanayoendelea ndani ya
shirika hilo. “Wewe unaendesha vikao lakini haya ndiyo mambo
yanayoendelea kwenye taasisi unayoiongoza,” alisema.
Alimtaka
afuatilie pia uwasilishaji wa mkataba huo kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ili vipengele vinavyoibana NDC kiuendeshaji na kupata gawio
viweze kuangaliwa upya.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa kampuni ya TANCOAL kwa
kuwashirikisha wajasiriamali wadogo kupata teknolojia ambayo itasaidia
kupunguza tatizo la ukataji miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.
Alisema
mgodi huo umeanza kuwanufaisha wenyeji kwani ameona kazi nzuri
inayofanywa na kikundi cha akinamama cha Mbalawala (mbalawala Women
Group) ambacho kinatumia vumbi la makaa hayo (ambayo ni mabaki)
kutengeneza mkaa wa kupikia majumbani (briquettes).
“Hii
teknolojia ikisambazwa kwenye shule, mahospitali na kwenye magereza
itasaidia kupunguza matumizi makubwa ya kuni yanayofanywa na taasisi
hizi,” alisema.
Meneja
wa kikundi hicho, Bibi Leah Kayombo alisema wanatumia chengachenga na
vumbi la makaa hayo kwa kuchanganya na kemikali nyingine ili kupunguza
joto halisi la makaa hayo, jambo linalowezesha mkaa huo kutumika
majumbani bila kuharibu masufuria.
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment