Saturday, 7 January 2017

Tagged Under:

Dk Malewa alifumua jeshi la magereza

By: Unknown On: 23:17
  • Share The Gag
  • KAIMU Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk Juma Malewa

    KAIMU Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Dk Juma Malewa amefanya mabadiliko ya uongozi kwa baadhi ya wakuu wa magereza wa mikoa na vituo mbalimbali hapa nchini.
    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa jeshi hilo, Lucas Mboje, mabadiliko hayo yalianza jana na ni ya kawaida na yanalenga kuboresha utendaji kazi na ufanisi wa jeshi la magereza.

    Katika mabadiliko hayo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Katos Rugainunura amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza sehemu ya Utawala.
    Nafasi yake inakaimiwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mzee Nyamka aliyekuwa Mkuu wa Utawala Magereza Mkoani Morogoro.
    Aidha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Antonino Kilumbi aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma amehamishwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mkuu wa Kikosi cha Ujenzi. Nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Julius Sang’udi aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya.

    Aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Magereza Anderson Kamtiaro anakwenda kuwa Ofisa Mnadhimu Magereza Mkoani Arusha na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza, Hassan Mkwiche ambaye alikuwa ni Mkuu wa Gereza Kuu la Karanga lililopo Moshi.
    Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Same, Kamishna Msaidizi wa Magereza Evarist Katego anakwenda kuwa Mkuu wa Gereza Kuu la Karanga na aliyekuwa Boharia Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, George Kiria amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Uhasibu .

    Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Uwesu Ngarama amehamishiwa Makao Makuu kuwa Boharia Mkuu wa Jeshi. Nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Ofisa Mipango wa Jeshi, Athuman Kitiku.
    Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoani Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Magereza Musa Kaswaka anakwenda Makao Makuu Kitengo cha Ukaguzi.

    Nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza, Ismail Mlawa aliyekuwa Mkuu wa Kiwanda cha Samani Gereza Kuu Ukonga.
    Taarifa hiyo ilisema aliyekuwa Ofisa Mdhibiti wa Fedha wa Jeshi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Gideon Nkana anakwenda kuwa Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga, Dar es Salaam na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza, Chacha Jakson.
    Wengine ni aliyekuwa Ofisa Mnadhimu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kijida Mwakingi anakaimu nafasi ya Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Magereza Abdalah Misanga anatoka Gereza la Mgumu kwenda kuwa Mkuu wa Gereza la Msalato mkoani Dodoma.

    Kamishna Msaidizi wa Magereza John Itambu anatoka Gereza la Kilosa kwenda kuwa Mkuu wa Kiwanda cha Samani cha Gereza Kuu la Ukonga. Kamishna Msaidizi wa Magereza Erasmus Kundy anatoka Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga kwenda Makao Makuu Kitengo cha Habari, wakati Kamishna Msaidizi wa Magereza Julius Ntambala aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi Makao Makuu, anabakia Makao Makuu Kitengo cha Ujenzi kuwa Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo.
    Kamishna Msaidizi wa Magereza Sylivester Mrema anatoka Gereza la Idete kwenda Gereza la Ubena kuwa Mkuu wa Gereza. Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ubena Kamishna Msaidizi wa Magereza Shaba Zephania anakwenda Magereza Mkoa wa Pwani kuwa Ofisa Mnadhimu.

    Kamishna Msaidizi wa Magereza Solomon Urio anatoka Makao Makuu kwenda Magereza Mkoa wa Dar es Salaam kuwa Ofisa Mnadhimu.
    Kamishna Jenerali Malewa aliteuliwa mwezi Desemba mwaka jana, baada ya Rais John Magufuli kuridhia ombi la kusitisha mkataba na kustaafu kwa Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali John Minja kuanzia Desemba 2, mwaka jana.

    Rais Magufuli alitangaza pia kuteua Kamishna wa Magereza, Dk Juma Malewa kuwa Kaimu Mkuu wa Jeshi la Magereza hadi hapo uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Magereza, utakapofanyika.
    Kustaafu kwa Minja kulikuja siku chache, baada ya Rais Magufuli kufanya ziara katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam Novemba 29, mwaka jana, ambako alitumia nafasi hiyo kupiga marufuku uuzwaji wa sare za majeshi nchini na watu binafsi.

    Alitaka wote wanaofanya biashara hiyo, kukabidhi mara moja kwa majeshi husika.
    Rais Magufuli alipiga marufuku hiyo kufuatia maelezo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza, kuwa wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi, kinyume cha taratibu za majeshi nchini.
    Rais alitaka pia vyombo vya ulinzi na usalama, kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za majeshi nchini. Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya.

    Chanzo HabariLeo.


    0 comments:

    Post a Comment