Makamu wa Raisi Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nane wa majaji ulioandaliwa na Chama Cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), unaofanyika
kila baada ya miaka miwili. Mkutano wa mwaka huu uliokuwa na kauli mbiu
isemayo ‘Kuongoza njia kufikia hitaji la upatikaji wa haki kwa wote na kwa wakati.
SUALA la rushwa ya ngono limeendelea kuwa tishio nchini hadi kusababisha wanawake wengi kujiengua katika nafasi zao.
Hayo yamebainishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati
akifungua Mkutano wa Nane wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA),
uliofanyika Dar es Salaam jana.
Samia alisema ni jambo la kuvunja moyo, kuona kwamba katika Karne ya
21 suala la rushwa ya ngono, linaendelea na kusababisha wanawake wengi
kujiengua katika nafasi zao.
Makamu wa Rais alionya juu ya vitendo hivyo vya rushwa ya ngono,
vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wenye madaraka na kusema tabia hiyo
ni mbaya na lazima ikomeshwe mara moja katika jamii.
“Matumaini, matarajio na ndoto za wanawake, zimekuwa zikikatishwa na
watu wachache ambao ni hatarishi, hivyo tunahitaji kufanya kazi
kuhakikisha kwamba tunawasaidia kwa hali na mali kwa sababu wahanga hao
wanaweza kuwa mama yako, dada, mke na binti yako,’’ alisema Makamu wa
Rais.
Alisema kuwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono, huzuia na kukwamisha
juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii na za kiserikali ipasavyo,
ikiwemo elimu, ajira na haki kwa ajili ya ustawi wa wanawake.
Makamu wa Rais aliwaagiza majaji na mahakimu wanawake kote nchini,
kupambana ipasavyo na kukabili vitendo vya unyanyasaji kijinsia na
rushwa ya ngono ili kusaidia wanawake kupata haki zao za msingi bila
kubaguliwa katika jamii.
Alisisitiza kuwa atahakikisha kwamba wanawake na watoto, wanapatiwa
haki zao kwa uhuru bila ya ubaguzi wala vitendo vya ukatili wa kijinsia
dhidi yao.
Samia aliongeza kuwa kuondoa vikwazo vya kisheria kuhusu ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake ni miongoni mwa maeneo makubwa
sita katika kuondoa pengo kubwa la kiuchumi.
Alifafanua kuwa serikali inahamasisha kushiriki kutekeleza sheria za
kimataifa katika kupambana na unyanyasaji wa kijinsia, rushwa ya ngono
na umiliki wa mali dhidi ya wanawake. Samia aliwahimiza majaji hao kutoa
hukumu kwa wakati katika kesi wanazoendesha ikiwa ni pamoja na kufuata
maadili na kanuni zilizowekwa.
Aidha, aliwataka kuhakikisha kwamba wanatoa bure elimu ya haki za
binadamu na ujuzi kwa maofisa wa mahakama, watunga sera na waathirika wa
ukatili wa kijinsia. Akitoa takwimu za ushiriki wa wanawake katika
nafasi mbalimbali, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema
asilimia 44 ya majaji waliopo katika mahakama ni wanawake huku Mahakama
Kuu pekee ikiwa na asilimia 47.9 ya wanawake.
Alisema Bunge lina asilimia 46.6 ya wanawake wakati katika nchi
jirani ikiwemo Kenya, wana idadi ndogo ya majaji wanawake ambayo ni
asilimia 3.3. Jaji Othman alisema kuwa wasajili wa mahakama waliopo,
asilimia 34 ni wanawake na kwamba nafasi ya uongozi hususan kwa mahakimu
wafawidhi wa mahakama za mwanzo na kati, imeongezeka.
‘’ Malengo yetu kama mahakama ni kuongeza idadi ya wanawake katika
mahakama zetu zote, kwani ndio mahitaji na matakwa ya sheria. Pia
niipongeze TAWJA ambayo imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika mahakama
kwa kutoa elimu kuhusu masuala ya kisheria kwa maofisa wa mahakama na
wengine wenye uhitaji,’’ alisema Jaji Othman.
Aidha, alisema kuwa kuongeza idadi ya mahakama za mwanzo na za kati
ni ishara ya kuongeza huduma za kisheria pamoja na utoaji wa elimu,
itakayosaidia kuiboresha mahakama pia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji Imani Aboud alisema kuwa
mkutano huo umekuwa ukifanyika kila mwaka na lengo ni kuzungumzia
masuala mbalimbali, ikiwemo mafanikio, changamoto na malengo yao ya
baadae.
Alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na
rushwa ya ngono, ambayo licha ya mwanamke kuwa na haki ya kupata kazi,
huombwa rushwa hiyo ili kumrahisishia upatikanaji wake.
‘’Tumejipanga kufanya kazi kwa mujibu wa sheria pamoja na kutoa elimu
kuhusu sheria zilizopo na kuwasaidia wanawake na jamii kwa ujumla, kazi
hii itafanyika kwa kadri serikali ya awamu hii inavyotaka,’’ alisema
Jaji Aboud.
Chanzo HabariLeo.
Saturday, 7 January 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment