Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu mustakabali wa uzinduzi wa
mkutano wao wa kampeni unaotarajiwa kufanyika agost 29 Dar es alaam.
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umesema utafanya mkutano wake wa
ufunguzi wa kampeni za urais katika Viwanja vya Jangwani Dar es Salaam
licha ya kuambiwa uwanja huo tayari ulikuwa umelipiwa.
Wakati Ukawa ukisema hatua hiyo ni hujuma dhidi yake na vyama vya
upinzani vinavyounda umoja huo, Halmashauri ya Manispaa Ilala imeweka
wazi kilichosababisha Umoja huo kukosa viwanja hivyo katika siku hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya malalamiko ya Chadema
chini ya mwavuli wa Ukawa, Ofisa Utamaduni wa Manispaa ya Ilala, Claud
Mpelembwe, alisema maombi ya kutumia uwanja huo yaliyowasilishwa na
chama hicho Jumatatu wiki hii, hayakufanikiwa kutokana na kukuta uwanja
huo ukiwa umelipiwa na chama kingine.
Mpelembwe alieleza kusikitishwa na kitendo cha Chadema kusambaza
nakala ya barua waliyoiandikia, kwenye mitandao na kutoa picha mbaya
kwamba wamezuiliwa kufanya uzinduzi wao.
“Kwanza tumesikitika sana, Manispaa na hata mimi binafsi,
nimehuzunishwa na hawa Chadema ni wateja wetu wazuri, tunafanya kazi nao
nyingi tu na hata wakati wa kuunda Ukawa walikuja kuulizia nafasi kwa
tarehe walizotaka kufanyia mkutano wao Jangwani na walipata kwa kuwa
hakuna mtu mwingine aliyeulipia,” alisema Mpelembwa.
Aliongeza, “… sasa wenzao Chama Cha Mapinduzi (CCM), walishaulipia
uwanja huo kwa tarehe hiyo, wao Chadema walipaswa baada ya majibu ya
barua yetu, wangerudi kuomba au kuulizia tarehe zilizo wazi”.
Alisema, awali Chadema walipeleka maombi ya kuzindua kampeni zao
wizarani wakiomba kutumia Uwanja wa Taifa, maombi ambayo yalikataliwa
kwa sababu zilizotajwa na kwamba wenzao, walipeleka maombi yao mapema
kwa manispaa kuomba matumizi ya uwanja huo.
Alisema Agosti 21, mwaka huu, CCM waliuliza uwepo wa nafasi ya
kutumia uwanja wa Jangwani na ndipo walipeleka maombi kuomba kuutumia
kwa maandalizi ya kuzindua kampeni zao kuanzia Agosti 21 hadi 23.
“Hakuna asiyejua utaratibu wa matumizi ya viwanja vya wazi na hata
kumbi za shehere au mikutano, unauliza uwepo wa nafasi kwanza kwa tarehe
utakazo kama ziko wazi, ndipo unafanya malipo na kuwekewa
ukumbi,”alisema Mpelembwa.
Alisema CCM baada ya kulipia ukumbi huo kwa tarehe tajwa, waliuliza
pia kama ipo nafasi katika uwanja huo kwa Agosti 28 hadi 30 na pia
Oktoba 22 hadi 24 mwaka huu, wakajibiwa kuwa zipo nao wakalipia.
“Sasa Chadema wao walileta maombi Agosti 24, na tuliwajibu uwanja
umelipiwa na mtu mwingine, na tuliwashauri watafute eneo jingine na
kwamba wanaweza kuutumia uwanja huo kuanzia Septemba mosi (wiki ijayo)
hadi Oktoba 21, kwa sababu hakuna aliyeulipia,” alisema Mpelembwa.
Ofisa huyo wa manispaa alisisitiza kwamba, baada ya wao kujibiwa
hivyo, walipaswa kurudi kwa Mkurugenzi wa Manispaa kuomba tarehe
nyingine jambo ambalo hawakufanya; badala yake, wamekwenda kusambaza
barua hiyo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
“Nilishangazwa sana, baada ya kuona barua hiyo kwenye mitandao ya
kijamii, na mimi ndiye ninayesimamia viwanja hivyo na huwa ninafanya
kazi na Chadema, sasa walipaswa kurudi kwetu kuulizia tarehe nyingine,
ila hawakufanya hivyo,” alilalamika Mpelembwa.
Alitaka umma kuelewa utaratibu wa matumizi ya maeneo ya wazi kwamba
yanatolewa baada ya maombi ya tarehe husika kukubaliwa iwapo hakuna mtu
mwingine aliyeomba awali kutumia eneo hilo.
Ukawa walalama
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti mwenza wa umoja
unaoundwa na vyama vya upinzani- Ukawa, James Mbatia, alisisitiza kwamba
mkutano wao utafanyika kama ulivyopangwa. Hata hivyo hakueleza ni wapi
utafanyikia.
Mbatia alisema suala hilo (la kukosa uwanja), wamemwachia Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva kwa kuwa yeye ndiye
mwamuzi na si mamlaka nyingine. Alisema endapo Mwenyekiti huyo wa NEC
hatachukua hatua, wataendelea na mambo yao kwa mujibu wa ratiba zao kwa
kuwa ni haki yao kisheria.
Alisema hawaoni sababu ya kumfuata kiongozi yeyote kwa ajili ya
kuomba kibali kwa kuwa hawana imani kutokana na tofauti zao za itikadi
za kisiasa.
“Sisi sio wakimbizi ndani ya nchi Tanzania. Sisi ni raia halali wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sisi tuna haki zote za kufanya kampeni
hapa kwa misingi ya taratibu na sheria na ndio tukasema hatutakubali
lazima kampeni zetu ziendelee hatutazuiliwa na mtu yeyote ni haki yetu,”
alisema Mbatia.
Aidha aliwataka wafuasi wa vyama hivyo na wananchi kwa ujumla kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki ambacho wanaendelea kutafuta ufumbuzi wa
suala hili .
Aliwataka kutokuwa na jazba waangalie mustakabali wa nchi kwani vyama
vya siasa vinaweza kusambaratika muda wowote lakini nchi ya Tanzania
itaendelea kubaki palepale.
Habari hii imeandikwa na Ikunda Eric, Fadhil
Akida
Thursday, 27 August 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment