Mgombea
urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akihutubia mkutano wa hadhara
katika Viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya jana. (Na Mpigapicha
Wetu).
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amesema nchi inapopata neema, wabaya nao huingia.
Akizungumza na wananchi katika maeneo ya Makongorosi na Chunya katika
mkoa mpya wa Songwe juzi, Dk Magufulia alifafanua kuwa Tanzania ina
rasilimali nyingi kuanzia madini, hifadhi za taifa na gesi, ambazo
zinatakiwa zitumiwe kwa manufaa ya wote.
Aliwaonya wananchi kuwa makini na wagombea wanaotoa fedha,
akikumbushia mchakato wa kumpata mgombea ndani ya CCM, ulivyogubikwa na
baadhi ya wagombea kumwaga fedha.
Alisema mgombea anayetoa fedha, maana yake anawanunua wapiga kura na
kuonya kuwa kama akipata madaraka kwa kununua watu, iko siku atawauza.
“Mimi nilijitokeza kimyakimya, nikatafuta wadhamini kimyakimya na
kurejesha fomu kimyakimya… Sikutaka kutoa fedha kwa kuwa ni dhambi kwa
Mungu,” alisema Dk Magufuli.
*Congo
Akifafanua kauli ya wabaya kuivizia neema ya nchi, Dk Magufuli
aliwataka Watanzania kutazama mfano wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo. Kwa mujibu wa Dk Magufuli, nchi hiyo jirani ina kila aina ya
rasilimali zenye thamani kubwa duniani, lakini mpaka sasa ina mtandao wa
barabara za lami wenye urefu wa kilometa 1,500 tu.
Hali hiyo ya DRC ni tofauti na Tanzania ambapo Dk Magufuli alisema
kwa sasa imefanikiwa kujenga karibu kilometa 20,000 za barabara. Pamoja
na mafanikio hayo, Dk Magufuli alisema bado Watanzania wamekuwa wakikosa
huduma muhimu wakati Serikali ina fedha za kutosha.
Alisema Watanzania wamefikia mahali pa kuichukia Serikali yao, huku
wakisema ni ya mafisadi na kuwasihi wananchi wasitoe hukumu ya jumla,
kwa kuwa wabadhirifu ni wachache.
Dk Magufuli alisema Watanzania sasa wanahitaji mabadiliko yenye tija,
kama yaliyotokea nchini China ambayo sasa ni nchi ya dunia ya kwanza na
si mabadiliko yasiyo na tija kama yaliyotokea nchini Libya.
Akifafanua kauli hiyo, Dk Magufuli alisema China inayoongozwa na
chama cha kikomunisti, baada ya kupata uzoefu, ilifanya mabadiliko kwa
kutumia chama hicho hicho na leo hata Marekani inaishangaa.
Lakini Libya kwa mujibu wa Dk Magufuli, ilikuwa na Rais Muammar
Gadafi ambaye alitumia vizuri rasilimali za nchi hiyo hasa mafuta,
kunufaisha jamii kiasi cha kufikia hatua ya kuwapa fedha na nyumba
vijana waliokuwa wakioa.
Alisema Walibya walipata raha wakati wa Gadafi, lakini wakalewa neema
na amani, wakamuua na baada ya hapo wamejikuta wakivurugana, huku
wengine wakikimbia nchi yao na wengine wakitamani Gadafi arudi lakini
ndio hawawezi kumrudisha.
*Zambi
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mbeya na Rungwe, Godfrey Zambi,
alisema chama hicho kimempata Magufuli kuwa mgombea wa urais ambaye ni
mwadilifu kiasi kwamba hata wapinzani hawawezi kumyooshea vidole.
Zambi alisema baada ya kupatikana Dk Magufuli, baadhi ya watu, hasa
wapinzani walitarajia kutokee mpasuko, badala yake sasa CCM imeimarika
na wako pamoja zaidi.
*Lukuvi
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Mjumbe wa
Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, William Lukuvi, alisema ndani ya
Serikali kuna magugu mengi na Dk Magufuli, ndiye tingatinga la kung’oa
magugu hayo.
Lukuvi alisema Dk Magufuli amekuja kusafisha maovu yote serikalini na
katika jamii ya Watanzania, kwa kuwa kuna kero nyingi, ambazo kwa
uchapakazi wake atazitatua.
Kwa mujibu wa Lukuvi, ndani ya CCM walijiangalia na kujipima kutafuta
mtu anayeweza kurejesha imani ya watu katika Serikali, kusimamia
nidhamu ya matumizi ya Serikali na kutenda haki, wakamuona Dk Magufuli.
Akizungumzia uadilifu wake, Dk Magufuli alitoa mfano wa Wizara ya
Ujenzi anayoiongoza, kwamba mwaka jana bajeti yake ilikuwa zaidi ya Sh
trilioni 1.2 na fedha za Mfuko wa Barabara zaidi ya Sh bilioni 600.
Pamoja na kupata fedha hizo katika Wizara, Dk Magufuli alisema
hakuwahi kula hata senti tano huku akiongeza kuwa hajawahi kutuhumiwa
kwa wizi, ufisadi wala ujambazi.
Akielezea zaidi historia ya utendaji wake serikalini, Dk Magufuli
alisema ametumikia serikalini kwa miaka 20 na wakati wote huo, hakuwahi
kufukuzwa kazi kwa kuwa hakuwahi kudhulumu mtu wala nchi.
“Niliwaheshimu Watanzania na kumuogopa Mungu, sikutaka kufanya
dhuluma kwa watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu na baada ya miaka 20
sasa, nadhani natosha kuwa rais, nataka nilete mabadiliko bora,”
alisema.
Alisema anataka siku moja akifa na kwenda Mbinguni, akiulizwa alifanya nini, aseme amewatatulia Watanzania kero zao.
Creaded by gazeti leo
Saturday, 29 August 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment