Uchapakazi
Mgombea Urais kupitia CCM, Dk John Magufuli akiwahutubia wakazi wa
Tunduma mkoani Songwe wakati wa ziara ya kampeni zake jana. (Picha na
AdamuuNDAN
MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli
amesema katika uongozi wake katika sekta ya ujenzi, alijikuta akifukuza
kazi makandarasi 3,200 walioonesha uzembe kazini.
Dk Magufuli amesema hayo jana katika miji na vijiji mbalimbali vya
Mkoa wa Songwe na kuongeza kuwa anachukia michakato na kupiga kalenda
shughuli mbalimbali za Serikali.
Aidha katika mikutano mbalimbali aliyoifanya mkoani Rukwa juzi,
mgombea huyo wa CCM amesema siku zote ni mkweli na katika dhambi ambayo
hajawahi kuifanya, ni kudanganya.
“Nitaunda Baraza la Mawaziri litakalojibu hoja na nitahakikisha
linafanya kazi. Hapa kwangu masuala ya mchakato hapana wala njoo kesho
hapana,” alisema.
Alisema waziri atakayeleta masuala ya michakato, ajichakate mwenyewe
kwa kuacha kazi ili wenye uwezo wa kufanya kazi wachukue nafasi hiyo.
Mgombea huyo wa CCM, alisema Watanzania wamechoka kudhulumiwa haki
zao na mafisadi, na sasa wanataka mabadiliko kuondokana na dhuluma hiyo.
Akizungumza katika mikutano hiyo na barabarani alipokuwa
akisimamishwa na wananchi, Dk Magufuli alisema matakwa ya wananchi kwa
sasa ni mabadiliko bora na si bora mabadiliko. Akielezea historia ya
utendaji wake serikalini, alisema ametumikia serikalini kwa miaka 20 na
wakati wote huo, hakuwahi kufukuzwa kazi kwa kuwa hakuwahi kudhulumu
mtu.
Alisema anataka siku moja akifa na kwenda Mbinguni, akiulizwa
alifanya nini, aseme amewatatulia Watanzania kero zao, hataki kuambiwa
amedhulumu mtu.
Dk Magufuli alisema kama ameweza kusimamia ujenzi wa karibu Kilometa
17,000 za barabara za lami, ambapo Kilometa moja sawa na zaidi ya Sh
bilioni moja, hatashindwa kutatua kero zingine za maji, umeme, dawa
hospitalini.
Akielezea mbinu ya utekelezaji wa ahadi zake, Dk Magufuli aliwataka
wananchi kumchagulia wabunge wengi kutoka CCM, apate nafasi ya kuteua
mawaziri wazuri kutoka kwa wabunge hao kwa ajili ya utekelezaji wa ahadi
hizo.
Akielezea ni namna gani atatatua kero ambazo pengine hazipo katika
Ilani ya Uchaguzi, Dk Magufuli alisema yeye atasimamia Serikali tajiri
kwa kuwa fedha zipo na kwamba tatizo la kutopatikana kwake ni matumizi
mabaya ya baadhi ya watu ndani ya Serikali.
Mgombea huyo alisema ana hakika watu ambao wamekuwa wakijinufaisha na
fedha za umma na kusababisha kero, ikiwemo ya ukosefu wa dawa, maji,
umeme, ujenzi wa barabara na kero nyingine zitakazoletwa na wabunge na
madiwani, atawashughulikia lakini na wao hawatampa kura kutokana na
kuhofia alichoita ‘moto’ wake.
Dk Magufuli aliwataka Watanzania kwa ujumla wao, hasa wanaoathirika
na ubadhirifu huo na rushwa, kumpigia kura kwa wingi ili ashinde na
akawashughulikie wabadhirifu, walarushwa na mafisadi wanaotumia vibaya
fedha hizo.
created by gazeti leo
Thursday, 27 August 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment