Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kushirikiana na
muungano wa vyama vingine vitatu vinavyounda umoja uliobatizwa jina la
Ukawa, leo kinatarajiwa kuzindua kampeni zake katika viwanja vya
Jangwani jijini Dar es Salaam.
Chama hicho kimetamba kufanya ufunguzi wa kampeni wa kihistoria.
Hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho kuruhusiwa na Mkurugenzi wa
Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, kutumia uwanja huo ambao awali
manispaa hiyo ilikuwa imetoa kibali kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kufanya tamasha lake.
Mapema, Mkurugenzi huyo alisema, manispaa yake ilikuwa imetoa kibali
kwa CCM kutumia uwanja huo kwa ajili ya tamasha walilopanga kufanya,
ambapo hata hivyo baada ya majadiliano kati ya manispaa hiyo na Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) walikubaliana mkutano wa Chadema ufanyike leo
kama ilivyopangwa.
Alisema pia walizungumza na viongozi wa CCM ili kuwaomba wawaachie
Chadema uwanja huo ili wafanye ufunguzi wa kampeni zao ambapo chama
hicho kilikubali kufanya hivyo.
Mgombea wa Urais wa chama hicho ni Edward Lowassa anayewakilisha
mwamvuli wa Ukawa anaoungwa mkono na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Lowassa jana alikutana na kuzungumza na makundi mbalimbali ya
wafanyabiashara, waendesha bodaboda, mama lishe, wasanii na makundi
mengine ambapo aliwataka kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika
ufunguzi wa kampeni hizo.
Aliyaambia makundi hayo kuwa matatizo yao anayafahamu hivyo wasiwe na
wasiwasi kwani anawaahidi kuyashughulia atakapopata ridhaa yao.
Aidha, alisisitiza suala la amani ya nchi ambapo alisema, amani
iliyopo kila mmoja ana wajibu wa kuilinda kwani endapo itatoweka
watakaopata shida ni watu wote na hasa akinamama. “Yapo mambo mengi
yanayotokea, vikwazo vya hapa na pale lakini nawaambia nchi yetu ina
amani sana na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda amani iliyopo,” alisema
Lowassa.
Alisema hakujiunga na Chadema kwa ajali bali kwa lengo la kuhakikisha
analeta mabadiliko na kuahidi kuwa endapo atapata nafasi atakwenda kwa
kasi kuhakikisha analeta mabadiliko hayo. Akizungumzia kuhusu elimu
alisema itakuwa ni moja ya jukumu lake la msingi kwani elimu ni ‘kila
kitu’ katika kuleta maendeleo ya nchi.
“Elimu itakuwa ni bure kwani wenzetu (nchi nyingine) wamewezaje na
sisi tushindwe? Nchi kama Marekani wamewezaje? Kipaumbele changu cha
kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu,” alisema.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa chama hicho, Haji Duni alisema,
atahakikisha Lowassa anatimiza ahadi yake ya kutoa elimu bure kuanzia
msingi hadi vyuo vikuu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, uzinduzi wa kampeni
hizo utakuwa ni wa kipekee kwani wamejipanga kuhakikisha mazingira ya
viwanja hivyo yanakuwa mazuri kwa kila mwananchi atayefika kwenye
kampeni hizo.
Created by gazeti leo
Saturday, 29 August 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment