Dar es Salaam. Askofu Dk
Fredrick Shoo amechaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
(KKKT), akichukua nafasi ya Dk Alex Malasusa aliyemaliza kipindi chake
cha miaka minane.
Dk Shoo, ambaye pia ni askofu
wa Dayosisi ya Kaskazini, alichaguliwa juzi usiku katika siku ya tatu
na ya mwisho ya mkutano mkuu wa 19 wa kanisa hilo uliofanyika Chuo Kikuu
cha Tumaini (Tuma) jijini Arusha baada ya kuwashinda maaskofu wenzake
wawili, katika uchaguzi uliokuwa na kila aina ya ushindani.
Waliokuwa
wakichuana kuwania nafasi hiyo baada ya kupendekezwa na Halmashauri Kuu
ya KKKT ni Askofu Dk Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki,
Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare na Dk Shoo.
Mwenyekiti
wa uchaguzi huo, Dk Malasusa, ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya
Mashariki na Pwani, alimtangaza Dk Shoo kuwa mkuu wa kanisa hilo kwa
kipindi cha miaka minne baada ya kupata kura 153, huku Dk Munga akipata
kura 67, ikiwa ni baada ya uchaguzi huo kurudiwa mara tatu kutokana na
mshindi kutopata zaidi ya theluthi mbili ya kura zote.
Kanuni
za uchaguzi za KKKT zinaeleza kuwa mshindi atapatikana kwa kupata kura
zisizopungua theluthi mbili ya kura zote zilizopigwa, iwapo mshindi
hatapatikana katika duru la kwanza, majina mawili yaliyopata kura nyingi
ndiyo yatakayopigiwa tena kura.
Iwapo theluthi mbili haitapatikana katika duru la pili, kura ya wingi au uchache itatumika kwa duru la tatu ili kumpata mshindi.
Katika kuhakikisha mshindi anapatikana, mkutano huo ulilazimika kutumia hatua ya wingi wa kura na Dk Shoo kuibuka mshindi.
Katika
awamu ya kwanza, Askofu Mjema alipata kura 53, Dk Munga kura 81 na Dk
Shoo kura 86, idadi ambayo haikufika theluthi mbili ya kura zote
kulingana na kanuni za kanisa hilo jambo lililosababisha uchaguzi
kurudiwa mara ya pili.
Dk Malasusa alitangaza matokeo
ya awamu ya pili ya kura zilizopigwa ambapo Askofu Munga alipata kura 94
na Dk Shoo kura 124. Kura moja ikiharibika.
Kabla ya
kuanza kwa mkutano huo wajumbe wa Halmashauri Kuu walipitisha majina
matatu ya maaskofu waliowania nafasi hiyo na kuyapeleka kwenye mkutano
huo ili yapigiwe kura.
Wajumbe wa mkutano huo mara
baada ya kupewa karatasi za kupigia kura walikwenda katika vyumba maalum
kwa ajili ya kumchagua askofu wanayemtaka, mara baada ya kuchagua
walitakiwa kurejea ukumbini na kutumbukiza karatasi hizo katika vifaa
vilivyoandaliwa kuhifadhia kura hizo.
Kauli ya Dk Shoo
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Dk Shoo alimshukuru Mungu huku akionyesha mshangao wa kuchaguliwa kwake.
“Sijui
nimepataje nafasi hii, ni nguvu ya Mungu tu kwa kweli. Kwa ushirikiano
wa waumumini wote nitaweza kufanya kazi hii, naomba mniombee,” alisema.
Alichokisema Malasusa
Akizungumza
katika ibada ya kufunga mkutano huo uliomalizika saa 6:00 usiku, Dk
Malasusa alisema anamuachia madaraka Dk Shoo katika hali ya amani na
utulivu, huku akiwapongeza viongozi na maaskofu wote wa kanisa hilo.
Awali
kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, mkutano huo ulimchagua Alice Mtui wa
Dayosisi ya Konde kuwa mwandishi wa kanisa hilo kwa kipindi cha miaka
minne.
Alice alipigiwa kura 201 na wajumbe wa mkutano huo, huku kura za hapana zikiwa 17 na kura moja ikiharibika.
Created by mwananchi
Created by mwananchi
0 comments:
Post a Comment