Mbali na wastaafu hao, Rais Kikwete ambaye jana alikiri kuwa yuko karibuni kuanza kuitwa mzee, naye amezungumzia namna alivyokabiliana na changamoto za uongozi wake, huku akizungumzia anachojutia katika miaka kumi ya uongozi wake. Haya yamo kwenye Ripoti ya Benki ya Dunia ambayo inaelezea kwa mara ya kwanza kufanikiwa kwa uchumi wa Tanzania na changamoto zake ikiwemo kuyumba kwake kwa zaidi ya miaka 50, tangu wakati wa Uhuru mwaka 1961 mpaka mwaka huu na kutoa jibu la kukua, kuanguka na kuibuka kwa uchumi wa viwanda Tanzania.
Mafanikio ya Mwalimu Katika ripoti ya kihistoria ya miaka 50 ya ushirikiano wa Tanzania na Benki ya Dunia iliyotolewa hivi karibuni, washauri wa mwanzo wa Mwalimu Nyerere na watendaji wa sekta muhimu akiwemo Profesa Simon Mbilinyi na Ibrahimu Kaduma, wamekaririwa wakizungumzia uongozi wa Mwalimu Nyerere ulivyokuwa. Ripoti hiyo inaweka bayana kuwa Mwalimu Nyerere aliongoza nchi iliyokuwa katika mfumo wa Kijamaa, ambao ulisimamia Serikali kuwa mpangaji na msimamizi mkuu wa shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Serikali ilimiliki njia kuu za uchumi na shughuli karibu zote za uzalishaji, huku sekta binafsi ikishiriki kwa kiwango cha chini katika mipango ya uchumi, na utekelezaji shughuli za uzalishaji. “Azimio la Arusha la mwaka 1967, liliweka kanuni za awali za namna mfumo huo wa uchumi utakavyosimamiwa na kutekelezwa. Ulikuwa kwa sehemu kubwa ukihusisha uwekezaji, umiliki na ukuaji wa ndani na Nyerere alifanikiwa kuwa msimamizi mkuu,” aimeeleza ripoti hiyo. Mafanikio ya mfumo huo, yametajwa kuwa yalikuwa mazuri kwa kufuata Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano, ambao ulifanyiwa mapitio na marekebisho kadhaa kwa wakati huo.
“Ingawa hakuna hata nchi moja iliyokuwa ikipata Uhuru, iliyoiga mfumo huo wa uchumi, Rais Nyerere alikuwa nyota ya kisiasa. Alisifiwa kwa uongozi thabiti kutoka kwa Watanzania wenyewe na mataifa ya Afrika yaliyokuwa yakipambana na ukoloni. “Alipata sifa kwa kuonesha uthubutu wa kubuni na kutekeleza mfumo wa Kiafrika wa kujitegemea katika maendeleo. Ulikuwa uongozi wa msomi wa kiafrika wa kijamaa, uliokubalika siyo tu kwa Watanzania wenyewe, lakini duniani kote,” imeeleza ripoti hiyo. Ripoti hiyo imeweka bayana kuwa mfumo huo wa Mwalimu Nyerere, ulitoa mwamko mkubwa mpaka katika sehemu kubwa ya nchi za Ulaya, ambapo katika miaka ya mwisho ya 1960, vijana wengi walionesha kuvutiwa na kuiga na uongozi wa Mwalimu Nyerere.
Kati ya miaka ya 1960 na 1970, ripoti hiyo imeeleza kuwa kukubalika kwa Tanzania, kulienda sambamba na kupokea ufadhili kutoka nchi wahisani, ambapo pia Rais Nyerere alikuwa kivutio katika nchi nyingi za Ulaya, hasa Sweden, Norway, Denmark na Uholanzi. Wahisani wavutiwa Profesa Mbilinyi, ambaye wakati huo alikuwa Mshauri wa Mwalimu Nyerere, amekaririwa na ripoti hiyo akisema ufadhili huo pia ulisaidia kuongoza nchi kwa mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea, ambapo Benki ya Dunia nayo ilidhamini nchi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na nishati, elimu na viwanda hasa vya sigara, sukari, nguo na vinu vya kusaga mahindi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata Benki ya Dunia ilivutiwa na mfumo wa Mwalimu Nyerere, kwani Rais wa Benki ya Dunia wa kati ya mwaka 1968 na 1981, Robert McNamara na kiongozi huyo wa Tanzania, walikuwa karibu na ushiriki wa benki hiyo katika miradi ya Tanzania ukawa mkubwa. “McNamara alifanya kazi nzuri sana, baadhi ya mambo ambayo (Tanzania ilihitaji), yalifanikiwa kwa sababu yake,” amekaririwa Kaduma akisema, ambaye alikuwa Mkurugenzi katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Kifedha na Kitaalamu katika Wizara ya Fedha kati ya Mwaka 1967 na 1969.
Kaduma amekaririwa akifafanua kuwa McNamara pia alikuwa muumini wa mfumo wa uchumi na maendeleo, ambao Serikali ndiyo mpangaji na mwendeshaji mkubwa wa sekta za uzalishaji zinazochangia ukuaji wa uchumi na kusimamia mgawanyo wa pato la Taifa na huduma za kijamii. “Tanzania imekuwa stahimilivu na umoja leo kutokana na sera za Mwalimu Nyerere. Sera zake zililenga kuleta usawa na haki. Hazikuhusu ujamaa pekee, zilihusu ukuaji wa uchumi katika hali ya usawa.
“Angalia sasa kuna ukuaji wa uchumi lakini si katika hali ya usawa unaoonekana tangu (wakati wa sera za uchumi huria) na ubinafsishaji katika miaka ya 1990, naona katika hili kuna kushindwa kwa sera ambako huwezi kukuhusisha na Mwalimu Nyerere,” amesema Kaduma katika ripoti hiyo. Kaduma amesisitiza katika ripoti hiyo kuwa, Mwalimu Nyerere alikuwa na maono, hakufikiria kesho peke yake, alitazama miaka mia mbele; “Nafikiri falsafa yake ilikuwa bora kwa nchi za Kiafrika na zilizokuwa zikiendelea kwa wakati huo.”
Mgongano viwandani Hata hivyo, kiongozi mwingine wa wakati wa Mwalimu Nyerere, Sir Andy Chande, akizungumzia uongozi wake alipokuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usagishaji (NMC), amesema katika sera hizo za ukuaji katika usawa, alijikuta akibishana na Waziri wa Kilimo, pale Serikali ilipoingilia bei ya mchele. “Nilikuwa na matatizo na Waziri wa Kilimo, ambaye aliagiza bei ya mchele ishuke ghafla katika soko la rejareja. Katika maduka, bei ya mchele ikawa ndogo kuliko gharama za uzalishaji na usafirishaji mpaka katika duka husika.
“Niliomba kukutana na Rais, tukakutana katika Ukumbi wa Baraza la Mawaziri na kulikuwa na kama watu 20, watumishi wa NMC, watumishi wa Wizara ya Kilimo na Katibu Mkuu. “Nilimwambia Rais, huna madaraka ya kunielekeza namna ya kuendesha shirika hili kama vile ni la misaada. Sheria ya Bunge imeagiza liongozwe kibiashara, lakini kama unataka niliongoze kama la misaada, tafadhali niambie. “Wenzangu walidhani angekasirika na pengine angenitupa katika Gereza la Ukonga. Lakini alikuwa mwelewa sana na akasema “hapana, hakuna kitu kama hicho” akaamua kuchukua suala hilo mikononi mwake na mambo yakabadilika,” amesema Chande.
Alifafanua kuwa alijua kuwa Waziri wa Kilimo ni mwanasiasa ambaye angependa sifa kutokana na kutoka katika jimbo na maslahi mengine ya kisiasa, hivyo asingekubaliana na kupandisha bei ya mchele. Kwa mujibu wa Chande, ingawa Nyerere hakukasirika, Katibu Mkuu alikasirika, akamsubiri Chande katika maegesho ya magari na kumwambia “unatumia matusi gani kwa Rais namna hiyo?” Chande alisema, alimjibu kuwa amesema ukweli na kama anataka aongoze yeye shirika hilo, lakini baadae akatafuta suluhu na Katibu huyo na mwishowe Waziri akaridhika kupandisha bei taratibu, mpaka ifike katika bei ya soko.
“Nilikuwa na uhusiano mzuri sana na Mwalimu Nyerere na kizuri ni kwamba, ukiwa mkweli kwake hatakuchukulia vibaya,” alisema Chande. Vita ya Kagera yavuruga Aliyekuwa gavana wa Benki Kuu (BoT) kati ya 1966 na 1974 na Waziri wa Fedha kati ya 1977 na 1980, Edwin Mtei, yeye anasema alianza kutofautiana na Mwalimu Nyerere wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1977. “Nilielezea mawazo yangu, kuhusu athari za Azimio hilo na hasa katika kupotea mitaji (baada ya kutaifisha njii kuu za uchumi)… Pia nilipinga baadhi ya hatua kama ya vijiji vya ujamaa ya mwaka 1971 na 1973, ambayo ilikuwa na athari mbaya ya haraka katika ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa chakula,” amesema.
Pamoja na maoni hayo, Mtei amesema alikubali kuwa Waziri wa Fedha mwaka 1977, kwa kuwa aliamini bado ana mawazo ya kuendelea kejenga uchumi wa nchi, na angeyatumia vizuri akiwa ndani ya Serikali kuliko nje. Wakati huo kwa mujibu wa Mtei mazao ya biashara yalikuwa na bei nzuri katika soko la kimataifa hasa kahawa, akiba ya fedha za kigeni ilikuwepo ya kutosha na hivyo alikuwa na imani kuwa uchumi ungeendelea kukuwa katika hali nzuri. Ndoto hiyo ya kuendeleza uchumi kwa mujibu wa Mtei, ilififishwa na Rais Idi Amini wa Uganda, alipoamuru jeshi lake livamie Tanzania, akajikuta akishiriki kutumia rasilimali zote za nchi, kufukuza jeshi la Amini mwaka 1978 mpaka 1979.
“Kuelekeza nguvu zote katika vita, maana yake kuunyonya rasilimali zetu mpaka kuuchosha uchumi na kutelekeza miradi ya maendeleo ya kuboresha miundombinu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi. “Tulitumia fedha nyingi za maendeleo katika vita karibu Dola za Marekani 500,000 kwa siku kwa mwaka mzima. “Shilingi ya Tanzania ilipoteza thamani kubwa kutokana na mfumuko wa bei uliosababishwa na uamuzi wa kutumia mikopo mikubwa kutoka katika mabenki na katika hazina za mashirika yaliyokuwa yakiyumba,” amesema Mtei.
Vikwazo wahisani Baada ya vita, Mtei amesema alianza kutafuta washirika wa maendeleo wasaidie kurejesha uchumi katika hali yake baada ya kufanya hesabu kwa wakati huo na kubaini kuwa nchi ilihitaji Dola za Marekani milioni 375 kwa haraka. “Lakini washirika wa maendeleo wakasisitiza, lazima tufikie makubaliano na Shirikila la Fedha Duniani (IMF) kwanza,” amesema. Kutokana na mazingira hayo, alisema alilazimika kwenda IMF jijini Washington Marekani kufanya majadiliano nayo, kutafuta mkopo, ingawa Mwalimu Nyerere hakupenda wazo la kutafuta mikopo, wala wazo la kuruhusu Shilingi ipate thamani kutokana na nguvu ya soko, wala kuruhusu ubinafsishaji wa mashirika yaliyokuwa katika hali mbaya.
Hata hivyo, alipofika IMF, akatakiwa kupunguza thamani ya shilingi ambayo ilikuwa ikipangwa na Serikali na kuiruhusu ishindane katika soko huru la fedha, na kufanya mabadiliko katika mashirika ya uma. Kwa mujibu wa Mtei, alijaribu kujadiliana na IMF kupunguza masharti yao hasa katika kupunguza thamani ya Shilingi, ili wabakie na masharti ya kufanya mabadiliko katika mashirika ya umma, ili yafanye kazi vizuri. “Niliporudi nyumbani na mtazamo huo, Rais alikuwa muwazi kabisa kuwa hakubaliani na suala lolote la kupunguza thamani ya Shilingi na mapito ya mashirika ya umma, atayafanya lakini kwa muda wake.
“Aliweka wazi kuwa hawezi kupokea amri kutoka Washington, Marekani, nikaona amekuwa akishauriwa vibaya na watu wasiojua hali halisi. Nikaamua kujiuzulu. Hata hivyo, Rais Nyerere aliendelea kuniheshimu pamoja na tofauti zetu,” amesema Mtei. Akizungumzia hali hiyo, Profesa Mbilinyi ambaye alikuwa mshauri wa Mwalimu Nyerere, amesema katika ripoti hiyo kuwa ilikuwa vigumu kumshauri kuhusu kupunguza thamani ya fedha, kwa kuwa Mwalimu alikuwa akipingana na IMF na Benki ya Dunia.
“Bosi alikuwa akitaka ushauri na majibu ya maswali yake kutoka kwetu, lakini ukitoa ushauri unaoendana na Benki ya Dunia, atakujibu “toka hapa” lakini mwishowe aliamua kuzungumza mwenyewe na Benki ya Dunia,” amesema Profesa Mbilinyi katika ripoti hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo katika miaka ya mwanzo ya 1980, hali ya uchumi ikawa mbaya na baadhi ya watu, wakaanza kuona sera za Ujamaa na Kujitegemea zimeshindwa kuleta maendeleo, na ulikuwa wakati wa kujaribu mfumo mwingine.
Profesa Mbilinyi amesema katika masharti ya IMF, Mwalimu Nyerere alikuwa tayari kukubali mabadiliko ya sera za kilimo, ili sera za Tanzania za kilimo ziwe za kibiashara zaidi, ili wakulima wawe matajiri badala ya ombaomba. “Mwalimu alisema IMF na Benki ya Dunia wakikubali hilo, atakwenda kuwashukuru lakini baadae alichoka kujadili mabadiliko ya sera, akatuambia anaona muda umefika akapumzike Butiama,” amesema Profesa Mbilinyi.
Mzee Mwinyi Akizungumzia alivyopokea kiti cha urais katika ripoti hiyo, Rais wa Awamu wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, amesema alipokea madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitokea Zanzibar, ambako alikuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 1984 mpaka 1985. “Nilikuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambako nilianzisha mchakato wa kuruhusu uchumi wa soko huria.
“Ingawa kupokea kwangu madaraka hakukuonekana kama kulifuata utaratibu wa kawaida, lakini viatu nilivyotakiwa kuvaa kwa miaka kumi, nililazimika kuvivaa kwa kuwa nilikuwa na uzoefu wa kufanya mabadiliko ya kiuchumi kwenda uchumi wa soko huria. “Sijutii lolote katika hatua yoyote niliyochukua ya kubadilisha uchumi kwenda wa soko huria katika uongozi wangu, kwa kuwa ndio ulikuwa mwanzo wa sekta binafsi katika nchi,” amesema Rais Mwinyi.
Rais Mwinyi amesema wakati huo Serikali ilikuwa na mashirika mengi ya umma yaliyokuwa hayafanyi kazi huku yakitaka kulipiwa gharama zao za uendeshaji kutoka katika mfuko wa Serikali, Hazina. “Serikali yangu ilitaka kuhakikisha mashirika yanayoshindwa kujiendesha, hayasafishi fedha kidogo za bajeti iliyopo nchini,” amesema Rais Mwinyi. Mwaka 1986, Mwinyi alimteua Cleopa Msuya kuwa Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango, ambaye alikwenda Washington kuendeleza majadiliano na IMF.
Akizungumza katika ripoti hiyo, Msuya amesema baada ya kurejea kutoka IMF, Mwinyi aliitisha kikao cha Baraza la Mawaziri na kukubali kutekeleza masharti ya Shirika hilo la Fedha Duniani, na kumtaka Waziri huyo wa Fedha kuandaa Bajeti ya Mabadiliko ya Uchumi. Kukosa usingizi “Tulizungumza katika Baraza la Mawaziri kuhusu tulichokubaliana IMF na kila mmoja akasewa sawa! Nenda kaandae Bajeti ya Serikali itakayoendana na makubaliano hayo,” amesema Msuya katika ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa Msuya, siku tatu baada ta kikao hicho cha Baraza la Mawaziri, Rais Mwinyi alimpigia simu na kumwambia “Sipati usingizi kutokana na haya makubaliano uliyokuja nayo, tunaweza kukutana tena tujadili upya katika Baraza la Mawaziri?”. Msuya amesema katika ripoti hiyo kuwa alikubaliana na Rais Mwinyi na bada ya siku mbili zingine, wakakutana tena katika Baraza la Mawaziri na siku moja kabla ya kusomwa kwa Bajeti hiyo, Rais Mwinyi akaitisha tena kikao.
“Katika kikao hicho nilimwambia Rais Mwinyi, kama kuna hata mmoja wetu ambaye hatakubaliana na Bajeti niliyoiandaa kutokana na masharti tuliyokubaliana kutoka IMF, nitajiuzulu ili ateue yeyote ambaye angemtaka na Rais Mwinyi akajibu hapana,” amesimulia Msuya. Katika kikao hicho cha Baraza la Mawaziri, Msuya amesema kuwa Rais Mwinyi aliwaambia kuwa ameshindwa kupata usingizi, kwa kuwa amekuwa na wasiwasi na kesho yake ni Siku ya Bajeti, lakini bado hawajiamini kama wanaweza kutangaza masharti waliyokubaliana na IMF au la.
Kwa mujibu wa Msuya, siku hiyo Rais Mwinyi aliwataka mawaziri wote wazungumze kutoka katika mioyo yao na kila mmoja aseme kama anakubaliana na masharti hayo au hakubaliani nayo ili wapate muafaka kama waendelee na masharti hayo, au waachane nayo. Mawaziri wapingana Msuya amesema kulikuwa na mawaziri wachache, akiwemo Waziri wa Viwanda ambaye hakukubaliana na masharti hayo, kwa kuwa wakati huo kulikuwa na maandamano katika nchi za Jamaica na Morocco kupinga masharti ya IMF, ambapo waziri huyo alionya kuwa maandamano hayo yangeweza kuibuka Tanzania.
Kwa mujibu wa Msuya, Rais Mwinyi alimkumbusha waziri huyo kuwa viwanda vichache vilivyosalia baada ya vingi kufungwa, vilikuwa vikifanya kazi kwa chini ya asilimia 25 ya uwezo wake. “Rais Mwinyi alisema hata viwanda kama vya vinywaji baridi, bia na vya nguo vilikuwa vikifanya kazi katika uwezo wa chini kabisa na hatukuwa hata na fedha za kununua vipuri, wala za kuagiza malighafi wala bidhaa nyingine muhimu kutoka nje ya nchi.
“Aliendelea kusema kuwa wasiwasi haukuwa huo wa viwanda kufanya kazi katika uwezo wao wa chini kabisa, bali kulikuwa na uwezekano kuwa vilikuwa vikitarajiwa kufungwa kabisa,” amesimulia Msuya. Wakati huo kwa mujibu wa Msuya, nchi nyingi za kiafrika zilikuwa zikikabiliana na hatua ngumu lakini za lazima za kubadilisha uchumi wao, ikiwemo mwaka 1982, Rais Nimeiri wa Sudan, alipotakiwa kuondoa ruzuku katika sukari, mafuta ya petroli na mkate.
Kwa mujibu wa Msuya, Rais huyo wa Sudan alilalamika IMF kuwa akifanya hivyo, kungetokea vurugu na maandamano nchini humo, lakini alivyosisitizwa, akakubali kuondoa ruzuku katika sukari na mafuta ya petroli tu. Msuya amesema katika ripoti hiyo kuwa, IMF ilihoji kwa nini hataki kuondoa ruzuku katika mkate, Rais huyo akaamua kuepuka vurugu kwa kupunguza ukubwa wa mkate, ndipo IMF ikakubali kumsaidia.
Profesa Mbinyi, ambaye pia alipata nafasi ya kuwa mshauri wa Rais Mwinyi katika ripoti hiyo amesema, “Ilikuwa ngumu kuwa mshauri wa Mwalimu Nyerere, kwa kuwa alikuwa na msimamo thabiti dhidi ya IMF, lakini ilikuwa kazi nyepesi kidogo kwa Rais Mwinyi. “Rais Mwinyi alikuwa na fikra huria, ilikuwa rahisi kwetu kubuni sera na kusimamia programu kwa kuwa alikuwa huru kuchanganya kanuni za kijamaa na za kibepari, ilimradi nchi isonge mbele,” alisema.
Mkapa Akizungumza katika ripoti hiyo namna alivyopokea madaraka kutoka kwa Rais Mwinyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amesema alikuta uchumi haukui, viwanda na mashirika yakifanya kazi chini ya uwezo wake, huku yakitaka fedha kutoka katika Mfuko wa Serikali, Hazina. “Kulikuwa na changamoto ya kubadilisha mwelekeo wa uchumi, namna ya kusaidia mashirika ya umma na binafsi yapate faida au ziada, namna gani ya kuruhusu mashirika mapya ya binafsi na ya umma kuanzishwa na kukua na kuwa na nguvu za kiuchumi. “Tulikuwa tukijiuliza je, tufungue fursa kwa sekta binafsi? Tutaweza vipi kuendesha mapato ya Serikali.
Namna ya kubana maeneo ambayo mapato ya Serikali yalikuwa yakivuja, namna ya kuongeza wigo wa kodi kwa kuwa pengo la bajeti lilikuwa kubwa kuliko uwezo. “Hakuna nchi inayoendelea bila deni, lakini deni letu lilikuwa kubwa kiasi kwamba likasababisha hasira kwa Benki ya Dunia, ambayo ilianza kupoteza matumaini ya kuboresha uwezo wetu wa ndani, kubadilisha mbinu zetu, kubadilisha umiliki wa uchumi wetu na kuweka misingi ya kufungua fursa mpya za kiuchumi, ikiwemo katika sekta ya madini,” amesema Mkapa.
Mkapa amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, kukaibuka changamoto nyingine ya kasi ya mabadiliko ambapo hata watumishi wa umma hawakuwa na kasi ya kukubali mabadiliko. Amesema alikutana na sekta binafsi na mikutano na viongozi wa wizara mbalimbali, ambapo alishauri watumishi na viongozi wa sekta binafsi kila mmoja kuzungumza kwa uhuru kuhusu changamoto wanayoiona bila kuogopa. “Mfano mzuri ni Waziri wa Elimu, Joseph Mungai, alikuwa mbunifu, aliweza kujadili na kushirikiana katika mabadiliko na Serikali Kuu, Serikali za Mitaa mpaka na viongozi wa vijiji.
“Baadae Benki ya Dunia, ikakubali kutusaidia katika elimu ya msingi, si tu katika udahili wa wanafunzi, bali katika mazingira ya kujifunza na kufundishia, malipo ya walimu, vifaa vitabu na vingine,” alisema. Akizungumzia mchakato wa kubadilisha umiliki wa uchumi, kutoka wa Serikali mpaka kwa sekta binafsi, Mkapa amesema ulifanyika vizuri, isipokuwa udhaifu ulikuwepo katika usimamizi wa mikataba na makubaliano.
“Nadhani ndio sababu mpaka leo kuna malalamiko kwamba tulikosea kukubali katika ubinafsishaji. Lakini hatukuwa na njia ya kuendelea kushikilia mashirika hayo na hakukuwa na suala la kurudi nyuma katika mabadiliko ya sera,” amesema. Akifafanua kuhusu madai kuwa mashirika na viwanda vingi viliuzwa kwa watu wa nje, Mkapa amesema kulikuwa na Watanzania wachache waliokuwa na uwezo wa kununua mashirika na viwanda vikubwa, lakini kwa wingi, Watanzania wengi ndio walinunua mashirika na viwanda hivyo.
“Hatukushindwa kabisa katika ubinafsishaji, lakini tulikwenda taratibu sana na hata mashirika ambayo hayakubinafsishwa, yapo yaliyokufa na mengine hayajakuwa. Kwa hiyo sera ilikuwa sahihi, lakini ufuatiliaji na utekelezaji vilichelewa,” amesema Mkapa katika ripoti hiyo. Kikwete Akizungumza katika ripoti hiyo Rais Kikwete ambaye uongozi wake umepata mafanikio katika ukusanyaji wa mapatio, ujenzi wa miundombinu ya barabara, sekta ya elimu kuanzia ya sekondari mpaka elimu ya juu, usambazaji umeme vijijini, bado ameelezea kuwa na majuto katika uongozi wake.
Akisimulia majuto yake, Rais Kikwete alikumbusha alivyoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini mwaka 1988, ambapo alianza kutembelea maeneo ya sekta hiyo kupata uzoefu. “Nilipokuwa nakwenda Mara (Mgodi wa North Mara), nikapita Butiama kumsalimia Mwalimu Nyerere akanipongeza na kusema “unafanya vyema kupata uzoefu wa sekta ya madini”. Rais Kikwete amesema moja ya jambo ambalo hawezi kusahau katika ziara hiyo ni pale Mwalimu Nyerere alipomwambia “Sikiliza Jakaya, sisi wakati wetu tulijaribu katika sekta ya kilimo na tukadhani kilimo kingekuwa sekta ya kutokea katika kukuza uchumi wetu, lakini kikaniangusha.
“Sasa unafanya kazi katika sekta ya madini, tafadhali jitahidi kwa nguvu zako zote ili sekta ya madini iwe sekta ya kututoa katika kukuza uchumi wetu,” alikumbushia wosia huo. Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kama kuna kitu anajuta wakati anaondoka madarakani, bado ni kilimo kwa kuwa hakiko katika hatua ambayo angependa kukiacha na kwa kuwa wamejitahidi kupunguza umasikini katika sekta hiyo inayoajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania, lakini umasikini bado uko juu.
Created by gazeti leo
0 comments:
Post a Comment