Dar es Salaam. Baba wa familia
iliyoteketea kwa moto ndani ya nyumba walimokuwa wamelala, jijini Dar es
Salaam, Masoud Mattar Masoud (59) amesema kama angeona miili ya familia
yake, naye angekufa.
Masoud alipoteza ndugu tisa baada ya nyumba yake kuteketea kwa moto, unaosadikiwa ulitokana na jiko la gesi.
Katika
tukio hilo lililotokea eneo la Buguruni Malapa, usiku wa kuamkia juzi,
jumla ya watu tisa walifariki dunia kwa kuungua moto ndani ya nyumba
hiyo namba 40, baada ya juhudi za wananchi kuwaokoa kushindikana.
Walioteketea
katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Samira Juma Ibrahim (42)
maarufu kwa jina la mama Aisha na watoto wake wanne; wavulana watatu na
msichana mmoja. Watoto hao ni Ahmed Masoud (15), aliyekuwa mwanafunzi wa
kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Msimbazi na Aisha Masoud
(13), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi
Alfurqan.
Watoto wengine wa familia hiyo ni Abdillah
Masoud (10), ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika
Shule ya Msingi Alfurqan, pamoja na Ashraf Masoud (5).
Mbali
na watoto wa familia hiyo, wengine waliofariki katika tuki hilo ni mama
yake Samira, yaani bibi wa familia hiyo, Bimdogo Masoud (72); mtoto wa
dada yake Samira, Wadhati Saleh (27) na mtoto wake Fahir Fesal (mwaka
mmoja na nusu) pamoja Samira Haroun (17).
Wadhati
ambaye alikuwa akiishi Magomeni, alikuwa mgeni katika nyumba hiyo na
alifika nyumbani hapo asubuhi ya siku ya tukio hilo yeye na mtoto wake
pamoja na Samira ambaye ni binti aliyekuwa akiishi naye.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema baada ya kusikia kelele za vilio, waliizunguka
nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwaokoa, lakini ilishindikana baada ya
milango kutofunguka na moto kuwa mkali kiasi cha kushindwa kuingia.
“Katika
namna ya kujaribu kujiokoa, Ahmed alijaribu hata kurusha nje funguo ili
waweze kufunguliwa mlango, lakini ilishindikana. Hivyo alirudi chumbani
wakashikana pamoja kusubiri kifo,” alisema Suleiman Bashraf (45),
ambaye ni kaka wa Samira.
Bashraf, anayeishi Mikocheni
na ambaye anasema alifika eneo la tukio wakati dada yake na watoto wake
wakiwa wameshafariki, alibainisha kuwa baba wa familia hiyo, alikuwa
kazini wakati wa tukio hilo
Jana katika mahojiano na
Mwananchi akiwa Kigogo CCM yaliko matanga kwa ndugu wa mkewe Masoud,
ambaye ni baba wa familia hiyo iliyoteketea alisema, “Ninaushukru
uongozi wa msikiti wa Gulam kunizuia kufika eneo la tukio na pengine
hata mimi ningekufa palepale.”
“Siku ya tukio mimi
sikuwapo nyumbani, nilikuwa kazini na kwamba nilipata taarifa za tukio
hilo kutoka Pemba kwa mjomba,” anaeleza.
Masoud ambaye
ni mfanyakazi wa kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Kontena (TICTS)
inayofanya kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, anasema anapokuwa zamu
ya usiku huwa anaondoka nyumbani saa 10 jioni na kupitia msikitini
kufanya ibada na baada ya hapo anakwenda kazini.
Masimulizi
Masoud,
huku akibubujikwa machozi kwa huzuni na kujifuta mara kwa mara
anasimulia: “Siku ya tukio hilo kulikuwa na ugeni nyumbani kwangu kwani
kulikuwa na mtoto wa dada wa mke wangu aitwaye Wadhati Saleh, huwa ana
kawaida ya kuja karibu kila wiki kumsalimia bibi yake. Wadhati alifika
asubuhi ya siku hiyo akiwa na mtoto wake pamoja na binti mmoja aliyekuwa
akiishi naye aitwaye Samira.
“Mtu pekee ambaye hakuwapo nyumbani wakati naondoka kwenda kazini alikuwa Ahmed ambaye alikuwa shuleni.
“Kwa
kawaida wakati ninapoondoka nyumbani mara nyingi huwa nataniana na mke
wangu. Yeye huwa ananitania kuwa mbona unaondoka mapema hivyo nami huwa
namjibu kuwa napitia msikitini kwanza. Hata siku hiyo wakati naondoka
mke wangu ambaye alikuwa amekaa nje na mtoto wa dada yake (Samira)
alinitania kama kawaida yake ‘mbona mapema hivi’, nami kama kawaida
nilimjibu kuwa ‘napitia msikitini’.
Basi mtoto wa
Wadhati alinifuata, nikamchukua na nikamrudisha kwa mama yake halafu
nikamuaga kuwa ningerudi kumchukua. Niliagana na familia yangu na
nikaiacha ikiwa yenye furaha. Niliondoka hadi msikitini ambako nilifanya
ibada kama kawaida na baada ya ibada nilikwenda kituoni ambako
nilipanda daladala na kwenda kazini. Kule kazini nilizima simu na
kuiweka kwenye chaji. Majira ya saa 10 alfajiri nilikwenda msikitini kwa
ajili ya ibada ya alfajiri na kwamba baada ya kutoka msikitini,
nilirudi kuchukua simu.
Nilipoiwasha tu nilisikia milio
kuashiria kuwa kuna simu nilikuwa nimepigiwa lakini sikupatikana. Punde
kidogo nilipigiwa simu na mjomba wangu Suleiman Salim, kutoka Pemba.
Aliniuliza kuwa niko wapi maana napigiwa simu sipatikani, nami nikamjibu
kuwa niko kazini na simu yangu niliizima nikaiweka kwenye chaji. Kisha
aliniambia niende haraka nyumbani kuna moto.
Aliponiambia
hivyo niliomba gari kazini likanipeleka nyumbani. Wakati tukiwa njiani
nilipigiwa tena simu nyingine na mkwe wangu, Ali Saidi, mume wa mtoto wa
dada. Alinitaka pia niende haraka nyumbani. Nilimuuliza kama kuna
usalama lakini yeye akasisitiza tu kuwa niende haraka.
Nilihisi
kuna tatizo kubwa na pale pale akili yangu ikaanza kuchanganyikiwa.
Nilipofika katika msikiti wa Masjid Gulam, nikasimamishwa na maimamu na
waumini wengine waliokuwapo pale msikitini, wakaniambia nisiende huko
nyumbani.
Walifungua mlango wa gari wakanishusha na
wakanichukua na kunipeleka hadi msikitini. Huko wakaniambia nipumzike
humo kwanza huku wakinitaka niwe mstahimilivu. Imam Said na waumini
wengine walinizunguka. Nikawaambia wanieleze nini kinaendelea kwa kuwa
mimi ni mtu mzima, lakini waliendelea kunipa maneno ya kunifariji.
Ndipo
wakaniambia kuwa hawakutoa hata mtu mmoja katika ajali hiyo. Nadhani
wakati ule waliponizuia kwenda kule nyumbani kwangu ndio wakati Polisi
walikuwa wakizipakia maiti kwenye gari kuzipeleka hospitalini. Hali
yangu ilibadilika sana na pengine kama ningeziona maiti nami ningekufa
palepale.
Nilikaa msikitini humo hadi asubuhi kwenye
saa nne kasoro hivi nilipochukuliwa kupelekwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) ambako miili ya marehemu ilikuwa imehifadhiwa kwa ajili
ya taratibu za mazishi. Hata huko Muhimbili sikuruhusiwa kuiona miili
ile na hata mimi sikutaka kuiona kwani nilikuwa nikiteseka sana kutokana
na matatizo ya shinikizo la damu.
Mke wangu alikuwa
ndiyo dira yangu. Alikuwa mdogo lakini kaniongoza na kanistahimili kwa
mambo mengi. Mke wangu alikuwa kiongozi wangu mambo mengi yeye ndiye
alikuwa akiyafanya.
Maalim Seif awasili
Wakati
mahojiano yakiendelea alifika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoendeshwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK), Seif Sharrif Hamad.
Maalim Seif
aliwasili msibani hapo saa 5.46 asubuhi na akatoa salamu za rambirambi
akiwataka wafiwa kumtumaini Mungu na kuwaombea dua waliofariki. “Huyu
(Masoud) siku yake ilikuwa haijafika ndiyo maana wakati haya yakitokea
hakuwapo. Lakini hawa siku yao ilikuwa imefika. Hivyo tuwaombee dua kwa
Mwenyezi Mungu.Created by Gazeti la Mwananchi
Toa maoni yako