MKAZI
wa wilayani Chato mkoani Geita, Rose Joseph (32) aliyekuwa na
maambukizi ya virusi vya Ukimwi na mtoto wake mwenye umri wa miaka kati
ya minne na mitano, wamekutwa mlimani wakiwa wamekufa katika mazingira
ya kutatanisha katika kijiji cha Nafuba kilichoko ndani ya Ziwa Victoria
wilayani Bunda mkoani Mara.
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Nafuba, Zakaria Kachimu alisema tukio hilo
liligundulika juzi saa 9:00 mchana katika eneo la mlima huo, baada ya
wananchi waliopita katika eneo hilo kuona kwanza mwili wa mwanamke huyo.
Alisema baadaye wananchi walifanikiwa kumtafuta mtoto wake na kumkuta pia akiwa amekufa katika eneo lingine.
Kachimu
alisema mwanamke huyo alifika kisiwani hapo Julai 25, mwaka huu, akiwa
na mtoto mdogo wa kiume aitwaye Kababu, akiwa anatafuta kazi ya
kuhudumia kwenye mgahawa.
Alisema
kuwa kulingana na afya ya mwanamke huyo kudhoofika, kila sehemu
alikokwenda kutafuta ajira hiyo alikataliwa. Baada ya kukosa ajira hiyo
mwanamke huyo alikwenda kwa jamaa yake ambaye pia ni mwanamke aliyeko
kisiwani hapo na kuishi nyumbani hapo.
Baadaye
mwanamke huyo alikwenda kutibiwa katika zahanati moja iliyoko kisiwani
hapo na ikagundulika kuwa ana mambukizi ya virusi vya Ukimwi na kuambiwa
aende katika Kituo cha Afya Kisorya kwa ajili ya kujiunga kwa kupewa
dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi (ARVs).
Hata hivyo ilielezwa kuwa mwanamke huyo hakwenda kwenye kituo hicho kama alivyoshauriwa na mganga wa zahanati hiyo.
Aidha,
Ofisa Mtendaji huyo alisema siku ya tukio wananchi waliopita katika
eneo hilo walikuta mwili wa mwanamke huyo katika mlima huo na kuamua
kutoa taarifa, ambapo tena walianza kutafuta mtoto wake na kukuta pia
akiwa amekufa katika eneo lingine.
Alisema kuwa chanzo cha vifo hivyo ni cha kutatanisha na kwamba huenda mtoto huyo alikufa kwa njaa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo. Alisema upelelezi unafanyika kujua chanzo cha vifo hivyo.
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment