Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akihutubia. |
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Tano, itapambana kwa nguvu zote na vitendo vya ufisadi kwenye fedha, zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Amesema serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii kwa kuendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi, kudhibiti matumizi yasiyo lazima na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa kodi ili fedha zinazokusanywa, zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.
Alisema hayo jana wakati akifunga maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima ya Nanenane kitaifa katika Uwanja wa Ngongo mkoani Lindi kwa niaba ya Rais John Magufuli.
Katika hotuba yake kwa mamia ya wananchi waliofurika katika viwanja hivyo, Makamu wa Rais alisema azma ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo itatimia, iwapo tu vitendo vya ufisadi katika fedha zinazoelekezwa kwenye maendeleo utakoma.
Alisema pia hayo yatawezekana endapo wananchi wataunga mkono jitihada za serikali katika kulipa kodi kwa wakati, kudai risiti, kufanya kazi kwa bidii na kukemea vitendo vya rushwa kama hatua ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tuna dhamira ya dhati ya kuendelea kuwatumikia na kuwaboreshea huduma zote za kijamii pamoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla bila kujali mikoa mnayotoka, jinsia, dini au itikadi za vyama vyenu.”
Kuhusu uimarishaji wa shughuli za kilimo nchini, Samia alisema maadhimisho ya Nanenane ni moja ya juhudi za serikali za kuboresha shughuli za kiuchumi katika taifa, ambapo asilimia 75 ya wananchi wanajihusisha na shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi kote nchini.
Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuzipa kipaumbele sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na kuongeza bajeti katika sekta hizo ili ziweze kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la taifa na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Aliwaeleza wananchi kuwa serikali imeweka mikakati na mipango inayolenga kusaidia uimarishaji wa shughuli za kilimo kote nchini kwa kuongeza matrekta makubwa na madogo kutoka 7,491 mwaka 2005/2006 hadi 16,478 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hivyo kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 70 hadi asilimia 12.
Alifafanua kuwa serikali imeongeza idadi ya maofisa ugani katika kilimo kutoka 3,379 mwaka 2005 hadi 2006 hadi 8,756 mwaka 2015/2016 na serikali pia imefufua mashamba ya mbegu kwa kuhusisha sekta binafsi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kuzalisha mbegu bora za mazao ya chakula nchini.
Matarajio ya wananchi
Akizungumzia matarajio ya wananchi, Samia alisema serikali inajua wananchi wana matarajio makubwa ya uongozi wao hivyo itahakikisha inaboresha huduma na uchumi wa Watanzania wote.
“ Tunajua mna matarajio makubwa na uongozi wa awamu ya tano, basi niwaahidi kuwa serikali yenu itahakikisha inaimarisha huduma na uchumi kwa usawa bila kuwa na upendeleo wa mikoa mnayotoka, itikadi ya dini na siasa,” alisema.
Aidha alisema ni vyema uongozi wa mikoa hiyo kuhakikisha wanaendeleza mashamba katika mikoa yao wayatumie kuwaelimisha wananchi njia bora za kilimo. Pia aliwataka wananchi kusaidia juhudi za serikali katika kuleta maendeleo kwa kulipa kodi, kupambana na rushwa na wafanyakazi wazembe na wavivu.
“Ningependa kuwaomba wananchi kuiunga mkono mikakati ya serikali ambayo ina lengo la kuwaletea mabadiliko chanya. Watanzania wote mnatakiwa kulipa kodi kama inavyotakiwa ili kufanikisha malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2020, alisema.
Kwa upande wa ufugaji, Samia alisema serikali inaboresha wataalamu wa mifugo ambapo wenye elimu ya Diploma wameongezeka kutoka 2,451 mwaka 2015 hadi 2,500 mwaka huu, wakati wale wenye Cheti wameongezeka kutoka 1,034 mwaka 2015 hadi 1,466 mwaka 2016 huku 1,471 wakihitimu Shahada mwezi Juni mwaka huu.
Alisema mpaka Juni mwaka huu kulikuwa na upungufu wa wataalamu 8,725 nchi nzima.
Kwa upande wa uvuvi, Samia alisema idadi ya mabwawa imeongezeka kutoka 21,300 mwaka 2014/2015 hadi 22,500 mwaka 2015/2016.
Alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha ifikapo 2020, ajira kwa vijana inaongezeka hadi kufikia asilimia 40 na kuwataka vijana kuchangamkia fursa za ajira zinazojitokeza.
Atembelea banda la TSN
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais aliipongeza Kampuni ya magazeti ya Serikali ya Tanzania Standard Newspapers Limited (TSN) kwa kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi kupitia magazeti yake, likiwamo gazeti mtandao.
TSN ni wachapishaji wa magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili, SpotiLeo na gazeti mtandao linalopatikana kwa anwani ya www. dailynews.co.tz na www.habarileo. co.tz.
Alitoa pongezi hizo baada ya kutembelea banda la TSN kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini katika viwanja vya Ngongo mjini Lindi. Pia alivutiwa jinsi TSN inavyoendesha gazeti mtandao na kuahidi kuwa atajiunga na huduma ya gazeti mtandao haraka iwezekanavyo.
“Hongereni kwa kazi nzuri mnayofanya nami nitajiunga na magazeti mtandao ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo,” alisema huku akitaka kujua kama huduma hiyo ni ile ya kupata ukurasa wa mbele na nyuma pekee.
Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa TSN, Prosper Mallya alimwambia Makamu wa Rais kuwa magazeti mtandao yana kurasa zote kama ilivyo kwa magazeti ya kawaida, lakini yanauzwa kwa nusu bei.
“Daily News mtandao inauzwa kwa Sh 500, HabariLeo kwa Sh 400 na SpotiLeo inauzwa kwa Sh 250, bei ambazo ni nusu ya bei za magazeti ya kawaida,” alisema.
Mratibu wa Toleo Maalumu katika Magazeti ya TSN, Dativa Minja alimwambia Makamu wa Rais kuwa TSN imekuwa ikiandika habari, makala mbalimbali na uchambuzi katika masuala ya kilimo, ufugaji na uvuvi na kuwa wakulima wananufaika kwa kusoma magazeti hayo.
Chanzo HabariLeo.
0 comments:
Post a Comment