SIKU 10 tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Kenya, imeelezwa kuwa
nchi hiyo ndiyo inayoongoza kwa kufanya uchaguzi ghali zaidi barani
Afrika.
Aidha, kwa duniani imeshika nafasi ya pili, ikitanguliwa na Papua New
Guinea inayotajwa kuwa kinara duniani, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali
vya habari. Wakati Papua NewGuinea ikitajwa kumgharimu kila mpigakura
Dola za Marekani 63 (Sh 132,300 za Tanzania), Kenya imetajwa kumgharimu
kila raia wake dola 25.4 (Sh 53,340) ili kulipia gharama za kila kura
katika mchakato huo wa kidemokrasia.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Kenya, Kamau Thugge
katika taarifa yake kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, mwaka huu,
makadirio ya fedha za uchaguzi yalikuwa Shilingi za Kenya bilioni 49.9,
sawa na dola za Marekani milioni 499 (Sh trilioni 1.04 za Tanzania). “Ni
gharama za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika uchaguzi.
Gharama za moja kwa moja ni Shilingi za Kenya bilioni 33.3 (Dola
milioni 333, sawa na Sh za Tanzania bilioni 700). Kwa mujibu wa
mchanganuo uliokuwa umetolewa, dola milioni 429 zilitakiwa kwenda Tume
Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), huku kiasi kingine kikisambazwa kwa
ajili ya mahakama, taasisi za usalama na msajili wa vyama vya siasa.
Hii ina maana kwamba, kwa dola 25.4 kwa kila mpigakura kati ya
Wakenya milioni 19.6 waliojiandikisha, imetia fora kwa kufanya uchaguzi
ghali zaidi katika Bara la Afrika. Inaelezwa kuwa, mwaka 2013 Kenya
ilitumia Sh bilioni 26 za nchi hiyo, sawa na Dola za Marekani milioni
260 (Sh bilioni 540) kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliomweka madarakani kwa
mara ya kwanza Uhuru Kenyatta.
Kiasi hicho ni takribani mara mbili ya uchaguzi wa mwaka huu.
Uchaguzi Mkuu wa Kenya mwaka huu pia umevutia idadi kubwa ya wagombea,
ambapo kulikuwa na wagombea 16,259 wakiwania nafasi mbalimbali 1,882
huku katika kiti cha urais kilichowaniwa na wagombea wanane, Uhuru
Kenyatta (55) alirejea madarakani baada ya kuvuna asilimia 54 ya kura
milioni 15.6 zilizopigwa, akimbwaga kwa mara nyingine mshindani wake,
Raila Odinga aliyepata asilimia 44.4 ya kura zote.
Hata hivyo, Raila aliyewania urais kwa tiketi ya Muungano wa Vyama
vya Upinzani (NASA), ikiwa ni mara yake ya nne kuisaka Ikulu ya Kenya,
lakini bila mafanikio, amegomea matokeo ya uchaguzi huo akidai haukuwa
huru na wa haki, licha ya waangalizi wa kimataifa kuusifia uchaguzi huo
kuwa haukuwa na dosari. Raila mwenye umri wa miaka 72, amekwenda
mahakamani kupinga rasmi matokeo ya uchaguzi huo.
Katika Afrika Mashariki, Rwanda ambayo pia imefanya uchaguzi wake
mkuu mapema mwezi huu uliomrejesha Rais Paul Kagame madarakani, hivyo
kuendelea kuongoza kwa muhula wa tatu, imeelezwa gharama zake za
uchaguzi kuwa zimemgharimu kila mpigakura Dola ya Marekani 1.05 (sawa na
Sh 2,205 za Tanzania). Ilikuwa na wapigakura waliojiandikisha milioni
6.8.
Katika mwaka 2010, inakadiriwa kila mpigakura wa Rwanda aliigharimu
nchi yake dola 1.71 (Sawa za Shilingi za Tanzania 3,591). Gharama za
Uchaguzi Mkuu wa Uganda wa mwaka jana, 2016 zinaonesha zilikuwa sawa na
Dola 4 za Marekani (Shilingi za Tanzania 8,400), wakati Uchaguzi Mkuu wa
Tanzania wa mwaka 2015 uliomweka madarakani Rais mchapakazi na `kioo’
cha nchi nyingi, Dk John Magufuli ulimgharimu kila mpigakura dola 5.16
(Shilingi za Tanzania 10,836).
Uchaguzi wa Ghana wa mwaka jana umetajwa ndiyo uliokuwa na gharama za
chini zaidi barani Afrika, kwa wastani wa dola 0.70 (Sh 1,050 za
Tanzania), wakati kiwango cha chini duniani ni wastani wa dola 5 (Sh
10,500 za Tanzania). Nigeria, taifa lenye watu milioni 186 ambalo lina
wapigakura takribani milioni 70, mwaka 2015 lilitajwa kutumia dola
milioni 603 (Sh za Tanzania trilioni 1.26), sawa na dola 8.61 (Sh
18,081) kwa kila mpigakura.
Tume ya Uchaguzi Tanzania Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Ramadhan Kailima amesema kuna mambo ambayo Tanzania inaweza
kujifunza kwa namna ambavyo uchaguzi nchini Kenya umefanyika. Aidha,
ameipongeza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) kwa
kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 8, mwaka huu na
Rais Kenyatta kurejea madarakani akiwabwaga washindani wake saba,
akiwemo wa karibu, Odinga.
“Tume imefanya mambo mazuri sana na wamekuwa mfano hata kuna taasisi
zimesema hivyo ikiwemo AU (Umoja wa Afrika) na EU (Jumuiya ya Ulaya),
hivyo nina kila sababu ya kumpongeza mtendaji mwenzangu,” alisema
Kailima. Alisema utaratibu waliotumia hauna tofauti na utaratibu
uliotumika nchini katika uchaguzi mkuu uliopita, lakini kuna baadhi ya
mambo yanapaswa kuigwa kutoka kwao. “Mfano matumizi makubwa ya
teknolojia, utoaji wa elimu ya mpigakura ambapo wao wameanza kipindi cha
maandalizi ya kuboresha daftari la kupigia kura, lakini sisi tutafanya
kwa mwaka mzima, kufanya midahalo baina ya Tume na wananchi ili wapate
nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa,” alisema Kailima.
Chanzo habariLeo
Monday, 21 August 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment