Monday, 21 August 2017

Tagged Under:

Wakuu wa SADC wampongeza Rais Magufuli

By: Unknown On: 11:20
  • Share The Gag
  • WAKUU wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wamempongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati akiwa mwenyekiti Asasi ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ya jumuiya hiyo.
    Walitoa pongezi hizo jana wakati wakihitimisha Mkutano wao wa 37 mjini Pretoria, Afrika Kusini. Akizungumzia mambo muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa 37 wa SADC, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alimwakilisha Rais Magufuli katika mkutano huo, alisema pamoja na mambo mengine, SADC imetambua na kuthamini mchango wa Tanzania katika kipindi cha uongozi wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama iliyokuwa chini ya Rais Magufuli.
    Alisema Tanzania imeshakuwa mwenyekiti wa asasi hiyo mara tatu kwa nyakati tofauti, ambapo mara ya kwanza ilikuwa kipindi cha 2006/2007, mara ya pili 2012/2013 na mara ya tatu kipindi cha Agosti 2016 hadi Agosti 2017. Tanzania imemaliza kipindi chake cha Uenyekiti wa Asasi ya SADC Agosti 19, 2017 wakati wa mkutano huo wa 37. Tanzania ilipokea kijiti cha uongozi huo kutoka Msumbiji wakati wa Mkutano wa 36, uliofanyika Swaziland Agosti 30, 2016.
    Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana wakati wa Uenyekiti wa Tanzania katika asasi hiyo ni kusimamia uchaguzi wa Bunge nchini Seychelles, uliofanyika Septemba, 2016. Aidha katika kipindi hicho, Tanzania ilisaidia kurejesha hali ya amani na utulivu nchini Lesotho, ambayo kwa muda mrefu tangu 2014 imekuwa kwenye mgogoro wa kisiasa; pamoja na kushughulikia matatizo ya uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
    Wakati huo huo, Mkutano huo wa 37 wa SADC ulimuongezea muda mwingine Mtanzania, Dk Stergomena Taxi kuendelea na wadhifa aliokuwa nao wa Katibu Mtendaji wa SADC kwa kipindi cha miaka minne mingine, ambapo atatumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2021. Dk Taxi alithibitishwa jana na Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali na kuapishwa rasmi kushika nafasi hiyo.

    Chanzo HabariLeo

    0 comments:

    Post a Comment