Tuesday, 1 December 2015

Fedha za Uhuru kupanua barabara

By: Unknown On: 01:57
  • Share The Gag
  • RAIS John Magufuli ameamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharimia shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru Desemba 9, mwaka huu, kutumika kupanua barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam, yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
    Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa kwa vyombo vya habari jana, ilisema tayari fedha hizo, kiasi cha Sh bilioni nne, zimepelekwa kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, linalopaswa kuanza mara moja.
    Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alitaka ujenzi wa barabara hiyo uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika barabara hiyo.
    Kujengwa kwa njia hizo, kutaifanya barabara ya Morocco hadi Mwenge kuwa na njia tano. Rais Magufuli hivi karibuni alitangaza kufuta maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru, ambayo huadhimishwa kwa kufanyika kwa gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama kwenye Uwanja wa Uhuru.
    Badala yake, mwaka huu maadhimisho hayo yafanyike kwa watu kufanya kazi za usafi katika maeneo yao ya kazi na majumbani. Akiwa katika kampeni za uchaguzi mkuu, Rais Magufuli aliahidi kumaliza tatizo la foleni za barabarani akichaguliwa kuwa Rais, akisema utatuzi wa tatizo hilo ulibidi usubiri kukamilika kwa mpango kabambe wa kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami ili kufungua njia kuu za nchi.
    Alisema mpango uliopo ni kuanza kujengwa kwa barabara za juu (fly over) kwa kasi kwa kuanzia eneo la Tazara, ambapo mkataba umeshasainiwa ili kuanza ujenzi.
    “Suala la foleni za Dar es Salaam wala si tatizo kubwa. Tusingeanza kujenga barabara za juu tukaacha mikoani hakuna barabara za uhakika za lami, tungeshangaza ulimwengu. Sasa tunaanza ujenzi wa fly over kwa kasi kubwa.
    “Kuanzia Januari mwakani (2016) tutaanza ujenzi wa barabara ya lami ya njia sita kutoka Dar es Salaam - Mlandizi hadi Morogoro kwa gharama ya shilingi trilioni 2.3, ambayo pia itasaidia kupunguza foleni Dar kwa vile magari yataweza kuingia na kutoka kwa urahisi kuliko sasa,” aliahidi Rais Magufuli alipoomba kura kwa wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam.
    Aidha, chini ya mkakati huo, Rais Magufuli alisema hatua zimeanza kuchukuliwa ili barabara inayopita baharini katika eneo la Daraja la Selander, yenye urefu wa kilometa 7.4, ianze kujengwa haraka iwezekanavyo kutokana na kukamilika kwa hatua za mkataba wa ujenzi.
    Kuanza kutekelezwa kwa ahadi hiyo ya kushughulikia kero za foleni katika Jiji la Dar es Salaam, kunadhihirisha azma ya dhati ya Rais Magufuli kutekeleza masuala mbalimbali aliyoahidi wakati wa kampeni kwa kasi kubwa, ambayo haikutarajiwa.
    Tayari Rais ameanza kushughulikia upunguzaji wa matumizi serikalini kwa kupiga marufuku safari za nje zisizo za lazima kwa watendaji wa serikali, kusimamia makusanyo ya kodi za serikali, kuboresha huduma za afya na kusimamia utoaji wa elimu bure kuanzia Januari mwakani.
    Juzi Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitoa Waraka wa Serikali Namba 5, wa mwaka 2015, kuwakumbusha watendaji wa sekta ya elimu kuhakikisha kuwa wanasimamia utekelezaji wa utoaji wa elimu bure kwa shule zote za umma na kufutwa kwa michango yote kuanzia Januari, mwakani.
    Katika hatua nyingine, Rais Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, Ikulu, Dar es Salaam.
    Katika mazungumzo hayo, Profesa Lipumba alimpongeza Dk Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kwa kutoa hotuba nzuri ya uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyokonga nyoyo za Watanzania. Kwa upande wake, Rais Magufuli alimpongeza Profesa Lipumba kwa msimamo wake thabiti wa kupinga ufisadi na amemtakia heri katika shughuli zake.

    Created by Gazeti la HabariLeo.

    Shambulio bandia laleta maafa Kenya

    By: Unknown On: 01:48
  • Share The Gag

  • Image caption Polisi wa Kenya

    Mwanamke mmoja amefariki na zaidi ya wanafunzi 20 kujeruhiwa katika oparesheni ya kuiga shambulio la kigaidi ilioendeshwa
    nchni kenya, katika chuo kikuu cha Strathmore.
    Oparesheni hii ilipangwa na chuo hicho pamoja maafisa wa polisi bila kuarifu wanafunzi na wafanyakazi, ili kubaini ikiwa chuo hicho kiko tayari kukabiliana na tukio la kigaidi.
    Kauli rasmi kutoka chuo kikuu cha strathmore, imedhibitisha kwamba mfanyakazi mmoja amefariki kutokana na majeraha aliyopata baada ya kuruka kutoka ghorofa ya tatu
    Wanafunzi zaidi ya ishirini wamejeruhiwa wanne kati yao wakiwa hali mahututi baada ya mkanyagano
    mkanyangano huo ulisababishwa na mkakati wa usalama uliokuwa ukiendeshwa chuoni humo na vikosi vya usalama
    Wengi waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitalini jijini Nairobi akiwemo mhadhiri aliyeruka kutoka ghorofa ya nne
    waliumia miguu na mikono katika harakati za kuruka kupitia madirisha na milango wakati wa tukio hilo.
    Mkakati huo ulipaswa kuangazia maandalizi ya wanafunzi na watu wengine endapo tukio la kigaidia linaweza tokea.
    Hata hivyo usimamizi wa chuo hicho umeelezea kusikitishwa na jinsi tukio hilo lilivyozuka na kusababisha majeraha huku ukiahidi kuwalipia gharama za hospitali za wote waliojeruhiwa.
    Tukio hili linajiri miezi kadhaa baada ya wapiganaji wa al shabaab kutekeleza shambulio la kigaidi mwezi aprili katika chuo kikuu cha Garrissa, na kusababisha vifo vya wanafunzi mia moja arobaini na saba.

    Created by BBC Swahili.

    Kasi ya Magufuli, Majaliwa imeipa uhai CCM – January

    By: Unknown On: 01:46
  • Share The Gag
  • MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, January Makamba amesema kasi ya utendaji inayooneshwa na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, imekipa uhai mpya chama chao na kwamba wanaCCM sasa wanatakiwa kutembea kifua mbele.
    Akizungumza jana na gazeti hili Dar es Salaam, January alisema wakati wa kampeni CCM iliahidi itawaletea Watanzania mabadiliko na jambo hilo ndilo hasa linalofanywa na Magufuli na Majaliwa.
    “WanaCCM sasa wanatakiwa kutembea kifua mbele na kuwapongeza Magufuli na Majaliwa kwa kutoa matamko ya kuwaunga mkono kwa hatua wanazochukua. Wakati wa kampeni tuliahidi mabadiliko ya kweli. Na sasa tunaanza kuyaona,” alisema January na kuongeza:
    “Tusikae kimya. Hii ni vita kali na naamini Watanzania wote wanamuunga mkono, lakini kwa kuwa anatekeleza ahadi ya CCM sisi tunapaswa kuwa mstari wa mbele kwa kumuunga mkono kwa maneno na matendo.
    “Tulipigana kufa na kupona ili tushinde na baadhi yetu tunaendelea kupokea vitisho na matusi kwa sababu ya kampeni kwa vile kwa wapinzani ushindani haujamalizika baada ya kumalizika kwa kampeni. Mbunge huyo wa Bumbuli mkoani Tanga na Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema kama mwana CCM na MNEC anajisikia fahari kwa vitendo vinavyofanywa na Magufuli kwa vile vimekipa chama pumzi na uhai mpya, akikumbusha maneno yaliyokuwa yakitumika na wapinzani kwamba chama hicho sasa kimeishiwa pumzi.
    “Lazima CCM ihakikishe Magufuli na Majaliwa wanafanikiwa katika uongozi wao. Hapo ndiyo nguvu iliyotumika katika kampeni itakuwa na maana. Kazi anayofanya Rais inakiletea chama pumzi na uhai mpya.
    “Kwa mwendo huu, hakutakuwa na kazi ngumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kama ilivyokuwa mwaka huu. Inawezekana wapo wanaCCM watakaoguswa na utendaji huu wa Rais, lakini hiyo ni gharama ndogo sana ya kulipa kwenye kuitafuta Tanzania ambayo kila mwananchi anaililia,” alisema.

    Created by Gazeti la habariLeo.

    Rais Magufuli Atangaza Kupunguza Wafanyakazi Katika Mshirika Ya Umma Ambayo ni Mzigo kwa Serikali

    By: Unknown On: 01:36
  • Share The Gag

  • Mamia ya wafanyakazi katika mashirika na taasisi mbalimbali za umma zinazoendeshwa kwa hasara likiwamo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wako hatarini kufutwa kazi kufuatia amri ya serikali  ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji katika taasisi hizo.

    Mashirika hayo yameelezwa licha ya kuwa na watumishi wengi, lakini bado uzalishaji na utendaji wake umekuwa hauna tija kwa taifa.



    Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msajili wa  Hazina,  Laurence Mafuru,  katika kikao na wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma.

    “Kuna kampuni ambazo zimepewa mtaji na serikali, lakini zinashindwa kuzalisha. Zinaandika barua kuomba msaada Serikali Kuu. Kama unaona (mkuu wa taasisi) una wafanyakazi wengi na huzalishi kwa namna inayotarajiwa, ni vyema upunguze watu,” alisema Mafuru.

    Kadhalika, licha ya kutoa maelekezo hayo, Mafuru alizitaja taasisi kadhaa zinazoendeshwa kwa hasara au kuzalisha chini ya kiwango kinachotarajiwa kuwa ni Tanesco, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Shirika la Ndege (ATCL), Kampuni ya Simu Tanzania ( TTCL) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).

    Maafuru alizitaja taasisi na mashirika mengine yasiyofanya vizuri kuwa ni Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Bandari (TPA), Kampuni ya Miliki ya Rasilimai za Reli (Rahco) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

    Mafuru alisema Serikali haihitaji kuvuna fedha katika taasisi hizo, bali jambo kubwa ni kuona kuwa zinajiendesha na kutimiza malengo yanayotarajiwa na umma wa Watanzania.

    “Serikali haihitaji kuchukua fedha katika taasisi hizi. Isipokuwa tunataka (taasisi za umma) zifanye kazi na ziwe nguzo za uchumi wa nchi. Tuache bajeti inayotengwa (na serikali) ifanye kazi nyingine ya maendeleo kwa Watanzania,” alisema, huku akiyataja Tazara na TRL kuwa ni vinara wa kuomba fedha kwa Serikali Kuu ili kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.

    “Kwa mfano Tanesco, kwa kipindi chote ilichoanza kufanya kazi mpaka sasa tulitarajia iwe imefanya kazi nzuri ya uzalishaji, lakini badala yake tunaona kinyume chake na hapo isitegemee kwamba endapo itaendelea kufanya hivyo serikali itakuwa inaangalia tu,” alisema.

    “Ni vema kama kuna shirika au taasisi ya umma ambayo inaona haizalishi na ina wafanyakazi wengi iwapunguze wafanyakazi hao. Kama tunaona tunashindwa, ni vyema tupunguze watu au turudi nyumbani tukapumzike,” alifafanua Mafuru.

    Mafuru aliongeza kuwa baadhi ya sababu za kufanya vibaya kwa taasisi na mashirika ya umma ni uzembe wa baadhi ya watumishi ambao hawafanyi kazi kwa kiwango kinachotarajiwa na wala kuwajibika ipasavyo katika kutimiza majukumu yao.

    Alisema tatizo jingine ni viongozi wa baadhi ya taasisi na mashirika hayo ya umma kuchukulia nafasi za uteuzi wanazopewa kuwa ni zawadi, fikra ambazo hivi sasa wanapaswa kuzifuta mara moja na kutanguliza zaidi uwajibikaji hasa kwa kutambua kuwa serikali ya awamu ya tano inaangalia zaidi utendaji wenye matokeo chanya kwa umma na siyo kinyume chake.

    “Msifikiri kwamba nyie ndiyo wapishi (wajuzi) pekee… wapo watu wengine wanaojua zaidi, kwa hiyo mjiandae kufanya kazi. Kila mtu atawajibika kwa nafasi yake,” alisema.

    Alisema  pamoja na kwamba serikali imezipa mali  taasisi hizo kujiendesha, lakini zimendelea kuwa mzigo kwa serikali kwani baadhi hushindwa kuzalisha na kuwa vinara wa ‘kutembeza bakuli’ kwa maana ya kuomba msaada kwa Serikali Kuu mara kwa mara.

    Mafuru alikitaja Chuo cha IFM kuwa ni mojawapo ya taasisi za serikali zinazoshangaza kwani licha ya kuwa na fursa ya kuzalisha, bado kimekuwa kikiendeshwa kwa hasara na kuwa miongoni mwa vinara wa kuomba msaada kwa Serikali Kuu.

    “Kwa mfano Chuo Kikuu binafsi cha Tumaini, kinajiendesha kutokana na ada za wanafunzi pekee. Kwa nini IFM inashindwa kufanya hivyo?” alihoji.

    Alisema taasisi zinazojiendesha kwa hasara zimekuwa mzigo mzito kwa serikali, hivyo ni lazima sasa kwa wakuu wa taasisi husika kuhakikisha kuwa wanaongeza ufanisi ili kujikwamua kutoka katika hali mbaya kiuchumi waliyonayo.

    “Hivi sasa serikali ina taasisi 220 kutoka 600 zilizokuwapo awali. Pamoja na kwamba taasisi za serikali zimepewa assets (mali) za kuzalisha, bado (baadhi) zimeshindwa kufanya hivyo, badala yake nyingine kila siku zinaandika barua kuomba fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali kuongezewa mtaji,” alisema.

    Katika hatua nyingine, Mafuru alisema inasikitisha kuona kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni miongoni mwa taasisi zisizozalisha kwa kiwango kinachotarajiwa na kwamba hadi sasa, hakuna faida yoyote ambayo imekuwa ikirudisha serikalini.

    Alisema kama TPA inafanya vizuri, ilitakiwa kufanya maendeleo mengine ikiwamo kujenga bandari nyingine.
     
    Aliitaka taasisi hiyo na nyinginezo kama TPDC kujifunza kutoka kwa taasisi binafsi juu ya namna ya kuongeza uzalishaji.

    Alisema kutokana na uendeshaji wa hasara kwa baadhi ya taasisi na mashirika ya umma, matokeo yake mashirika na taasisi hizo, kwa pamoja huchangia asilimia 22 tu ya pato la Taifa kwa mwaka, hali ambayo haipaswi kuendelea.

    Wakati huo huo, Mafuru alitoa agizo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa taasisi za umma ifikapo Desemba 15, zikiwamo zote zilizobainika kuwa hazikuwa zikifanyiwa ukaguzi hapo kabla.
    Credit; Mpekuzi blog
    By: Unknown On: 01:33
  • Share The Gag
  • Sakata la Makontena: Polisi Kwa Kushirikiana na TRA Wakamata Makontena 9

    Mpekuzi blog
    Maofisa wa Jeshi la Polisi  Dar es Salaam kwa kushirikiana na TRA, wanayashikilia makontena 9   Mbezi Tanki Bovu baada  ya  kuyatilia shaka kuwa yalikuwa yanasafirishwa kinyememela usiku wa kumakia leo

    Madereva waliokuwa wanasafirisha makontena hayo baada ya kuhojiwa wamesema hawajui wanakoyapeleka na hawana nyaraka muhimu za kuonyesha kilichopo ndani.
     
    Credit; Mpekuzi blog

    'Rais Magufuli aombewe'

    By: Unknown On: 01:29
  • Share The Gag
  • VIONGOZI mbalimbali wa dini nchini, wamempongeza Rais John Magufuli na kuwaomba Watanzania kuendelea kumsaidia na kumuombea ili atekeleze majukumu yake kikamilifu katika kuboresha uchumi wa taifa.
    Aidha, takribani wachungaji 10, wamejikusanya kwa pamoja na kumfanyia maombi kiongozi huyo ili aendelee na moyo wake wa ujasiri katika kuwatumikia wananchi na kupambana na baadhi ya watumishi wasio waadilifu, wakiwemo wafanyabiashara wasio waaminifu. Viongozi hao walitoa rai hiyo kwa nyakati tofauti, ambapo walionesha kuguswa na kasi ya utendaji wa Dk Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika kushughulikia kero za wananchi ikiwemo tuhuma za ufisadi.
    Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya aliwaomba Watanzania wakiwemo wabunge, viongozi wa Serikali wa ngazi zote, viongozi wa vyama vya siasa na madhehebu ya dini kumsaidia kiongozi huyo katika kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
    Askofu huyo alisema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Dayosisi ya Kanisa la Anglikana mkoani Morogoro juzi, zilizofanyika makao makuu ya kanisa hilo.
    Alimpongeza Dk Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na kubainisha kuwa viongozi hao, wameanza kazi vizuri na kuonesha matumaini mema kwa Watanzania.
    Pia alimpongeza Rais mstaafu, Benjamin Mkapa aliyekuwa mgeni, kwa uongozi wake uliokuwa umejengwa na uwajibikaji na uwazi uliowezesha kukuza uchumi na kupunguza mfumuko wa bei na uchumi kuwa imara.
    Kwa upande wake, Mkapa alilipongeza Kanisa na kubainisha kuwa licha ya kutoa huduma za kiroho, pia limekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma za kijamii zikiwemo za afya na elimu. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, Emmanuel Makala, alisema wataendelea kumuombea Rais Magufuli kutokana na kuendelea kupambana na mafisadi ikiwemo wanaojihusisha na dawa za kulevya.
    Alisema hayo juzi wakati wa ibada ya kuingizwa kazini Mchungaji wa Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu, Aron Mkaro katika kanisa la KKKT Usharika wa Tumaini mjini humo. Makala alisema kuwa ni wajibu wa viongozi wa dini, kumwombea Rais na wasaidizi wake kuhakikisha wanabadilisha maisha ya Watanzania.
    Alisema watamuombea Rais Magufuli na viongozi wengine wakuu ili kuhakikisha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma inarejea, ikiwa pamoja na kupamba na mfumo mbovu wa utoaji huduma kwa jamii.
    Mkoani Mara, wachungaji zaidi ya 10 kutoka makanisa mbalimbali wilayani Tarime, wamefanya kikao cha kumuombea Rais Magufuli ili aendeleze juhudi zake za kuwakomboa wananchi, wakiwemo wa kipato cha chini kwa kuwabana na kuwachukulia hatua watumishi wa Serikali wasio waadilifu.
    Wachungaji walioshiriki katika dua hiyo, wakiongozwa na Makamu Askofu wa Kanisa la Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT) John Mwita, kumuombea Dk Magufuli ili Mwenyezi Mungu amwongoze na kumlinda dhidi ya maadui wa Taifa wenye nia mbaya kwa taifa. Habari hii imeandikwa na John Nditi, Morogoro, Samson Chacha, Tarime na Kareny Masasy, Bariadi.

    Bakhresa achunguzwa

    By: Unknown On: 01:26
  • Share The Gag
  • KAMPUNI ya Said Salim Bakhresa (SSB) inachunguzwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za kushiriki kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mabilioni ya fedha kutokana na makontena yaliyohifadhiwa kwenye bandari yake ya nchi kavu (ICD) ‘kupotea’ bila kulipiwa kodi. Tayari Mamlaka ya Mapato (TRA) imepiga marufuku SSB kuingiza makontena katika bandari hiyo kavu ambako ndiko kunadaiwa kufanyika kwa vitendo hivyo vya ukwepaji wa kodi kutokana na baadhi ya makontena kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
    Katika barua iliyoandikwa kwenda kwa Meneja Mkuu wa SSB iliyosainiwa na Wolfgang Salia kwa niaba ya Kamishna wa Ushuru na Forodha wa TRA, inaeleza kuwa usitishwaji huo unatokana na kampuni hiyo ya Bakhresa kuchunguzwa kwa tuhuma za kuwepo madai ya kujihusisha na ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya kontena zilizoingia na kutoka kwenye ICD yake.
    Kwa mujibu wa barua hiyo, vitendo hivyo vya ukwepaji wa kodi vimefanywa kinyume cha Sheria ya Ushuru wa Pamoja wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004 na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
    “Kwa hali hiyo, imeamriwa kusitishwa kuingizwa kwa makontena katika ICD yako, uamuzi huo unaanza mara moja tangu kuandikwa kwa barua hii. Pande zote zinashirikishwa katika kushughulikia suala hili,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyoandikwa Novemba 17, mwaka huu.
    Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alipoulizwa juu ya suala hilo jana, alikiri kampuni hiyo kuchunguzwa, lakini akagoma kuzungumzia kwa undani kwa kuwa suala hilo liko kwenye uchunguzi.
    “Mimi siwezi kulizungumzia suala hilo kwa sababu liko kwenye uchunguzi na wanaofanya uchunguzi huo ni state organ (vyombo vya dola). Katika hatua hiyo, mimi siruhusiwi kusema lolote,” alisema Kayombo.
    Meneja wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Said Mohamed alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema yeye hahusiki na masuala ya ICD badala yake mambo hayo aulizwe Meneja wa ICD aliyemtaja kwa jina moja la Khan. “Mimi niulizie unga umekosekana... Sihusiki kabisa na mambo hayo,” alisema Mohamed.
    Hata hiyo, Mohamed aligoma kutoa mawasiliano ya Khan, akisema: “Hiyo namba mimi hapa sina, wewe mtafute tu huko ICD atakupa maelekezo zaidi.”
    Habari zilizopatikana jana pia zilieleza kuwa mmoja wa wafanyakazi wa SSB anayeishi maeneo ya Kinyerezi (jina tunalihifadhi), alivamiwa na kundi la maofisa wa Serikali kuanzia asubuhi hadi jioni na kufanya upekuzi kwake.
    “Tangu asubuhi hawa jamaa wamekuja hapa wakamchukua mjumbe wa eneo hili na kwenda naye kufanya upekuzi, hadi sasa hivi wanaendelea kufanya kazi hiyo,” alisema Tito Bagule, mkazi wa eneo hilo.
    Tayari Rais John Magufuli ameshamsimamisha Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade kutokana na tuhuma za uzembe na rushwa na kusababisha upotevu wa makontena zaidi ya 349 yenye thamani ya Sh bilioni 80. Upotevu huo umegundulika baada ya makontena hayo kuonekana kwenye mifumo ya Mamlaka ya Bandari, lakini haimo kwenye mifumo ya TRA.
    Kabla ya kusimamishwa kazi, Bade alikiri kupotea kwa makontena hayo, wizi ambao alisema unafanywa kati ya bandari kuu na bandari kavu (ICD) ya Ubungo.
    Alisema kutokana na upotevu wa kontena hizo mmiliki wa bandari hiyo ameamriwa kulipa faini ya Sh bilioni 12.6 na hadi sasa alishalipa Sh bilioni 2.4. Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani Athuman, amesema tayari jeshi hilo limeanza upelelezi kuhusu kashfa ya upotevu wa makontena iliyobainishwa hivi karibuni na kusababisha baadhi ya vigogo wa TRA kusimamishwa kazi.
    Pamoja na upelelezi huo, alisema wameanza uchunguzi wa mali za wafanyakazi wote waliohusishwa na kashfa mbalimbali TRA kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kubaini kama zinaendana na kipato chao halisi. Akizungumza na gazeti hili jana, Diwani alikiri kuwa jeshi hilo linawashikilia watumishi wanne kati ya watano wa TRA ambao jeshi hilo liliagizwa liwakamate na kuwahoji kuhusu sakata la upotevu wa kontena 349.
    “Tuliagizwa tuwakamate watumishi watano, mpaka sasa tumewakamata wanne, mmoja ndio tupo kwenye utaratibu wa kumkamata, lakini kikubwa ni kwamba tumeanza upelelezi, kama tulivyoagizwa,” alisisitiza DCI Diwani.
    Kuhusu suala la mali za watumishi hao, alisema ni jambo ambalo bado lipo kwenye upelelezi na linahusisha taratibu nyingi za kisheria, hivyo asingependa kulizungumzia kutokana na sababu za kipelelezi.
    Kutokana na ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa alibainisha kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 bandarini bila kulipiwa kodi na kuisababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 80. Kutokana na kashfa hiyo, Rais Magufuli alimsimamisha kazi Bade na kumteua Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dk Philip Mpango kukaimu nafasi hiyo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika.
    Maofisa wengine waliosimamishwa ni Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Habibu Mponezya, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu, Eliachi Mrema. Wengine ni Anangisye Mtafya, Nsajigwa Mwandengele na Robert Nyoni.

    Created by Gazeti la HabariLeo.