Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali
imejipanga kutengeneza mwongozo wa kuwarudisha shuleni wanafunzi
waliopata mimba wakiwa masomoni ili kuhakikisha wanapata elimu hadi
kufikia ngazi za juu.
Hayo
yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi Masuala
Mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Venance Manori
alipokuwa akifungua warsha ya kuwawezesha Maafisa Waandamizi wa Serikali
kutoka nchi sita za Afrika katika kutengeneza mipango inayozingatia
jinsia katika elimu kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Prof. Joyce
Ndalichako.
Manori
amesema Serikali ya Tanzania inajitahidi kuzingatia jinsia katika
utoaji wa elimu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa elimu ya Msingi na
Sekondari uwiano wake ni moja kwa moja japo kuwa idadi ya wasichana
hupungua kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakumba hivyo lengo la
warsha hiyo ni kuwasaidia wadau kuweka mipango ya elimu inayozingatia
usawa wa kijinsia.
“Serikali
yetu imejipanga kuhakikisha wasichana wanapata elimu hadi ngazi za juu
lakini mpango huo unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za mimba
na ndoa za utotoni hivyo ili kuhakikisha mtoto wa kike anafikia ngazi za
juu za elimu tuko kwenye mchakato wa kuandaa mwongozo kwa ajili ya
wanafunzi waliopata mimba wakiwa bado wanasoma kupata nafasi ya
kuendelea na masomo,”alisema Manori.
Mkurugenzi
Msaidizi amezitaja changamoto zingine zinazowapelekea wanafunzi wa kike
kuacha shule zikiwemo za umaskini, mazingira rafiki ya kusomea, mila na
desturi zinazomkataza msichana kupata nafasi ya kusoma pamoja na kukosa
muda wa kujisomea kwa sababu ya kufanya kazi nyingi wanaporudi
majumbani.
Manori
ametoa rai kwa Watanzania kuelewa kuwa kila mtoto ana haki na wajibu wa
kupata elimu bila kujali jinsia pia ameiasa jamii kuacha kuwaozesha
wasichana wenye umri chini ya miaka 18 ili waweze kufikia malengo yao
waliyojipangia.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Plan International- Tanzania,
Jorgen Haldorsen ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
kuhakikisha mipango ya elimu nchini inaangalia usawa wa kijinsia kwa
kuwa ni njia moja wapo itakayochochea maendeleo ya elimu kwa watoto wa
kike.
“Warsha
hii imeandaliwa kwa ajili ya wadau wote kutoa mawazo yao juu ya
changamoto za usawa wa kijinsia zinazoikumba sekta ya elimu pamoja na
kuwapa fursa wadau hao kushauriana kuhusu mikakati mbalimbali ya kutatua
changamoto hizo ili kuinua sekta ya elimu sio tu kwa Tanzania bali kwa
Afrika nzima,”alisema Haldorsen.
Haldorsen
ameongeza kuwa mfumo wa elimu umetambua uhusiano uliopo kati ya elimu
na usawa wa kijinsia ndio maana wadau wa masuala ya elimu wa Serikali
kutoka katika baadhi ya nchi za Afrika wameamua kuungana kwa pamoja
kujadili juu ya tathmini, mpangilio na ufuatiliaji wa elimu
unayozingatia jinsia.
Tanzania
imekua nchi ya kwanza kuendesha warsha hiyo ya siku tatu
iliyoshirikisha maafisa waandamizi wa Serikali wanaoshughulikia mipango
ya elimu kutoka nchi za Mozambique, Zambia, Malawi, Uganda, Zanzibar na
Tanzania Bara.
Imeandaliwa
kwa ushirikiano wa shirika la Plan International- Tanzania, Global
Partnership for Education (GPE), Dubai Cares pamoja na United Nations
Girls’ Education Initiative (UNGEI).
Credit; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment