Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 23 Machi, 2017 amefanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar
es Salaam kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa
kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na
kutoka nchini kupitia bandari hiyo ikiwemo usafirishaji wa mchanga wa
madini kwenda nje ya nchi.
Katika
ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia makontena 20 ya mchanga wenye
madini kutoka kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa ambayo yamezuiliwa
kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku
usafirishaji wa mchanga nje ya nchi tarehe 02 Machi, 2017.
Pamoja
na kushuhudia makontena hayo, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa
Jeshi la Polisi Nchini IGP - Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola
kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa popote ulipo, mpaka hapo
uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.
“Nataka
niwaambie nchi yetu inachezewa mno, nimekuja kuyaona haya makontena
kama yapo, na kweli nimeyaona, sasa utaratibu utakapokamilika nataka
Watanzania na dunia nzima ione kilichomo humu ndani kama ni mchanga
kweli ama dhahabu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Akiwa
bandarini hapo Mhe. Dkt. Magufuli pia ameshuhudia udanganyifu mwingine
unaofanywa na wafanyabiashara wanaoagiza mizigo kutoka nje ya nchi baada
ya kuoneshwa makontena ambayo nyaraka zinaonesha yamebeba mitumba ya
nguo na viatu wakati ndani yake kila kontena moja limebeba magari matatu
ya kifahari.
Maafisa
wa bandari ya Dar es Salaam na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wamemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kufuatia maelekezo aliyoyatoa ya
kuhakikisha mizigo yote inakaguliwa kwa mitambo ya mionzi (Scanning
Machines) wamefanikiwa kubaini udanganyifu mwingi unaofanywa na
wafanyabiashara wanaoingiza nchini na kusafirisha nje ya nchi mizigo
mbalimbali yakiwemo makontena 10 ambayo yamepatikana yakiwa na magari ya
kifahari ilihali nyaraka zake zikionesha yana mitumba ya nguo na viatu.
Mhe.
Rais Magufuli amewapongeza maafisa na wafanyakazi wa bandari ya Dar es
Salaam na TRA kwa kazi nzuri wanayofanya kudhibiti upotevu wa fedha za
umma bandarini hapo na amewataka kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa
uzalendo na kujiepusha na rushwa.
“Leo
mmenifurahisha sana, ninawatia moyo endeleeni kuwakamata wote
wanaofanya udanganyifu huu na muwachukulie hatua kali za kisheria,
lakini msimuonee mtu na msipokee rushwa, tunataka watu wajifunze kuwa
hapa sio shamba la bibi” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha,
ametoa wito kwa vyombo vyote vinavyoshughulikia udhibiti wa mizigo
inayoingia na kutoka kupitia bandari ya Dar es Salaam na bandari
nyingine hapa nchini, kuendelea kushirikiana ili kukomesha vitendo vyote
vya udanganyifu ambavyo vinasababisha nchi kupoteza mapato mengi.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Creted; Mpekuzi Blog
0 comments:
Post a Comment