Saturday, 17 September 2016

Tagged Under:

Lipumba, Sakaya, Kambaya watuhumiwa kupanga njama za utekaji viongozi wa CUF

By: Unknown On: 00:01
  • Share The Gag
  • Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha ambaye pia ni Kaimu Naibu Mkuu CUF, Bara Joran Bashange
    Chama cha Wananchi (CUF) kinawatuhumu waliokuwa viongozi wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho na Magdalena Sakaya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bara kufanya jaribio la kumteka Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha ambaye pia ni Kaimu Naibu Mkuu CUF, Bara Joran Bashange.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma CUF inadai kuwa jana majira ya 2:30 asubuhi vijana wanaosadikiwa kuwa wa Prof Lipumba wamefanya jaribio la kutaka kumteka Bashange wakati akitoka nyumbani kwake eneo la Buguruni.

    Na kwamba watekeji hao wakiwa na gari aina ya Noah yenye namba ya Usajili T 760 CEX  baada ya jaribio la kumteka, walifanikiwa kumuingiza katika gari hiyo ya NOAH iliyokuwa na vioo vyeusi (tinted).

    Taarifa hiyo ilieleza kuwa Bashange alipambana na kuomba msaada kwa kuita watu waliojirani kwa yowee la kuita “Majambazi” ndipo wananchi wakalizingira gari hilo na kuweka mawe na magogo na kuita Polisi.

    Baada ya Polisi kufika waliwakagua vijana hao na kuwakuta na pingu, silaha kadhaa na kitambulisho feki cha polisi.

    Baada ya ukaguzi kufanyika vijana watatu walikamatwa na mmoja alifanikiwa kukimbia.

    Taarifa hiyo ilifafanua kuwa mmoja kati ya vijana waliokamatwa ni mlinzi wa karibu wa Prof. Lipumba aitwaye HAJI “Mrangi” ambaye ni maarufu na anadaiwa kujulikana kwa ushiriki wake wa vitendo vya kihuni na kiharamia kama hivyo.

    Hata hivyo, katika mahojiano ya awali mmoja wa vijana hao alitoa ushirikiano na kueleza kuwa wametumwa na Abdul Kambaya na kwamba anayeongoza oparesheni yao hiyo ni mtu aitwaye Athumani (Mganga wa Kienyeji na Mwalimu wa mafunzo ya Kareti) aishiye Ilala akisaidiwa na watu wengine wanaojulikana Abubakar Fambo, Mohamed Ibrahim na Hassan Kingwele ( Mlinzi wa Magdalena Sakaya (MB).

    Vijana hao waliokamatwa wanakiri kuwa mipango yote hiyo Prof. Lipumba anaijua kama vile walivyoongoza mpango wa kuhujumu Mkutano Mkuu Maalumu wa CUF ulioahirishwa pale Blue Pearl Hotel, Ubungo Plaza.

    Joran Bashange ameumizwa maeneo kadhaa ya mwili na anaendelea na matibabu na taarifa za ndani zinaonesha kuwa wahusika walielekezwa kumshambulia vibaya na kumuua ikiwa wangelifanikiwa kuondoka naye.

    Vijana waliohusika na utekaji huo na gari lao wanashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Polisi Buguruni.

    Chama cha CUF kimelaani kitendo hicho na kimesema kinachukua hatua stahiki.

    Pia Chama hicho kimesema kinaamini kuwa kwa sasa Prof. Lipumba na watu wake wamekusudia kuendesha hujuma za wazi na kuvuka mipaka ya ushindani wa kisiasa za ndani ya Chama na kujivika joho la ‘Uintarahamwe na Umungiki’ wa wazi dhidi ya Chama na kuhatarisha na kutishia usalama wa maisha ya viongozi wa Chama.


    ==

    cREDIT Mpekuzi Blog

    0 comments:

    Post a Comment