Tuesday, 23 February 2016

Baba Amchoma Mwanawe vidole kisa Mboga Ya Sh. 500

By: Unknown On: 22:18
  • Share The Gag


  • MKAZI wa kitongoji cha Kazima – Kichangani Kata ya Kawajense, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Emmanuel Joseph (31) amemfanyia unyama mtoto wake wa kumzaa, George Emmanuel (4) kwa kuvichoma kwa moto vidole vyake vya mkono wa kushoto, akimtuhumu kukomba mboga yote ya majani aina ya ‘chainizi’ yenye thamani ya Sh 500.

    Inasemekana baba huyo amekuwa akiishi na watoto wake watatu baada ya kuachana na mkewe wa ndoa, Semsni Jahala (28) Machi mwaka jana.

    Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Rashid Mohamed amethitibisha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema lilitokea juzi saa 12 jioni katika kitongoji cha Kazima– Kichangani.

    Akisimulia mkasa huo, Kaimu Kamanda Mohamed alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa kwa mahojiano na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa awali wa shauri lake kukamilika.

    “Jioni hiyo ya tukio saa kumi na moja jioni mtuhumiwa huyo (Emmanuel) alipika chakula cha jioni, ugali na mboga za majani maarufu chainizi kisha akakihifadhi chakula hicho jikoni na kuondoka … aliporudi nyumbani saa kumi na mbili jioni ili kuandaa chakula cha jioni ndipo alipobaini mtoto wake (George) amekomba mboga yote ya majani. 
    "Alikasirishwa na kitendo hicho na kusababisha kumpiga kisha kumchoma moto vidole vyake vitatu vya mkono wa kushoto na kumsababishia maumivu makali,” alieleza Kaimu Kamanda.

    Kwa mujibu wa mashuhuda kutoka eneo hilo la tukio, mtoto huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako amelazwa kwa matibabu.

    Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya Wilaya ya Mpanda, Oscar Mkenda alisema mke aliamua kuachana na mumewe huyo baada ya kuchoshwa na ukatili na unyanyasaji aliokuwa akifanyiwa, ikiwemo kupigwa mara kwa mara bila sababu yoyote.

    “Mtoto George alikomba mboga hizo zote za majani baada ya kushinda na njaa mchana kutwa kwani hata kifungua kinywa hakupa asubuhi… hivyo baada ya baba yake kubaini mtoto wake George amekomba mboga zote, ndipo alipochochea moto na kuukandamiza mkono wake wa kushoto na kuunguza vibaya vidole vyake vitatu,” alieleza Mkenda.
     
    Credit;Mpekuzi blog 

    Simbachawene awabana Ma-DED

    By: Unknown On: 22:12
  • Share The Gag
  • Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikari za mitaa (Tamisemi), George Simbachawene (kulia) akimhoji jambo Mkurugenzi Mtendendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Azimina Mbilinyi, wakati wa kikao kilichowakutanisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa wilaya za mkoa huo alipokuwa katika ziara mkoani Morogoro.
    WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amesema kuwa wakurugenzi wa halmashauri nchini, wakaoshindwa kutekeleza agizo la kujitosheleza kwa madawati katika shule ya msingi na sekondari hadi Juni mwaka huu, wajitambue wameshindwa kazi.
    Pia wakurugenzi wa halmashauri watakaozalisha madeni ya watumishi pamoja na ya wazabuni wa vyakula katika shule za serikali, watakuwemo kwenye kundi la kuwajibishwa.
    Waziri huyo wa Tamisemi alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na Viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri (Ma-DED), makatibu tawala wa wilaya, na wakuu wa idara za halmashauri zote za mkoa huo chini ya Mkuu wa Mkoa, Dk Rajab Rutengwe.
    Hivyo alisema agizo lililotolewa na Rais John Magufuli la kutaka kuona kila mwanafunzi anaketi kwenye madawati, halina mjadala na kwamba ifikapo Juni mwaka huu pasiwepo na mwanafunzi anaketi sakafuni na wakurugenzi watakaoshindwa, watakuwa wameshindwa kazi na watawajibishwa.
    Aliagiza wakuu wa mikoa na wilaya, ambao ndiyo wasimamizi wa rasilimali zilizopo katika maeneo yao hasa ya misitu, wasisite kutoa vibali vya uvunaji wa miti ya kutengeneza madawati kwenye wilaya zao ili watoto wote waliopo shuleni wawe wanakaa kwenye madawati.
    “Tumieni vyema nafasi zenu za kuwa wenyeviti kamati za kutoa vibali vya uvunaji rasilimali za misitu... ili madawati yaweze kupatikana na utekelezaji wa matumizi ya vibali hivyo ufuatiliwe ili visitumiwe vibaya na waliopewa kazi hizo,” alisema Waziri.
    Alitoa mfano kuwa Mkoa wa Morogoro ambao una rasilimali nyingi za misitu, umekuwa na upungufu wa madawati ni 73,972 katika shule za msingi na 11,038 katika shule za sekondari za serikali.
    Pia alisema mkoa una upungufu wa vyumba vya madarasa 4,508 kwa shule za msingi na madarasa 352 kwa shule za sekondari za serikali wakati eneo la afya lina upungufu wa zahanati 334.
    “Kuna kazi kubwa katika sekta ya elimu ambapo kwa Mkoa wa Morogoro pekee unakabiliwa idadi ya madawati mengi sembuse wilaya kama ya Kibaha,” alisema.
    Waziri Simbachawene pia alionya tabia ya uzalishaji wa madeni ya watumishi wa halmashauri na wazabuni, wanaotoa huduma ya vyakula shule za serikali unaofanywa na watumishi wa Idara ya Uhasibu na maofisa utumishi kuwa siku zao, zinahesabika na wajiandae kutumbuliwa majipu.
    Ili kutekeleza agizo la kukomesha uzalishaji wa madeni, alitoa maelekezo kwa maandishi kwa wakurugenzi wa halmashauri zote 181 kwa ajili ya utekelezaji wake.
    Alisema halmashauri hizo, zina uwezo wa kulipa madai ya wafanyakazi wake kama nauli ya likizo, gharama za matibabu na mambo mengine kwa kutumia fedha za makusanyo yake ya ndani kwa kuwa fedha za mishahara na mengine zinatolewa na Serikali Kuu.
    “Serikali inalaumiwa kwa sababu wakurugenzi hawatekelezi wajibu wao na matatizo mengi yapo katika Idara ya Uhasibu na Idara ya Utumishi,” alisema na kuongeza: “Wahasibu ni chanzo cha matatizo yote haya wanakuwa na mahusiano na wenye kutoa huduma, utakuta deni la shilingi bilioni 25 likihakikiwa linabakia shilingi bilioni tano, zimeongezwa tarakimu hapo na haya yameshatokea.”
    Aliongeza, “Hawa sasa wajiandae kutumbuliwa, tunaelekea ngazi ya wakuu wa idara wa halmashauri, akitumbuliwa mkurugenzi naye mkuu wa idara anayehusika na kashfa hiyo atawajibishwa si kwa mkurugenzi pekee.”
    Aliwakumbusha wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kutambua jukumu walilopewa la ukamilishaji wa vyumba vya maabara na wasiokamilisha hicho ni mojawapo ya kigezo cha kupoteza nafasi zao.

    Chanzo HabariLeo.


    NECTA Yasitisha Kugawa vyeti kwa Wahitimu wa Kidato cha Sita 2015 ......Vilivyogawiwa Vyatakiwa Kurudishwa Haraka

    By: Unknown On: 22:05
  • Share The Gag

  • Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limeagiza kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti vya kidato cha sita kwa wanafunzi waliohitimu mwaka 2015, huku vile vilivyokwisha gawanywa kwa watahiniwa hao vikitakiwa kurejeshwa kwenye chombo hicho.

    Hali hiyo imeibua utata mkubwa, huku baadhi ya wadau wakiwamo maofisa elimu, wakihisi hatua hiyo ya Necta huenda inalenga kuvibadili vyeti hivyo kutoka kwenye mfumo wa wastani wa alama (GPA), kwenda kwenye ule wa jumla (division).

    Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda, alipoulizwa  kama amepokea agizo hilo, alithibitisha kuwa shule zote za mkoa huo zenye kidato cha tano na sita zimepewa taarifa ya kutakiwa kurudisha vyeti hivyo Necta.

    Alisema sababu ya kuvirudisha vyeti hivyo anadhani ni kufanya mabadiliko kutoka GPA na kurudi kwenye divisheni.

    Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Nestory Mloka, alisema amepata barua ya maelekezo hayo kutoka Necta ikimuelekeza kuwataka maofisa elimu wilaya wawasiliane na wakuu wa shule za kidato cha tano na sita wasigawe vyeti vya wanafunzi waliohitimu mwaka 2015.

    Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Matthew iliyoko Kongowe, Mkuranga mkoani Pwani, Abraham Shafuri, naye alikiri kuwapo kwa agizo la Necta la kusimamisha utoaji wa vyeti hivyo kwa wahusika.

    Alisema aliambiwa na maofisa wa Necta kuwa vyeti hivyo vinatakiwa kurejeshwa kwenye baraza hilo na kwamba sababu zilizotolewa ni kuwa kuna marekebisho kidogo yanapaswa kufanyika.

    “Nilichoambiwa ni kwamba shule karibu zote za Dar es Salaam zimesharejesha vyeti hivyo na kwamba kwa sisi wa mkoa wa Pwani, maofisa hao watapita kuvichukua lakini hatujui ni lini watakuja,” alisema Shafuri.

    Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde, alipoulizwa   alikanusha vikali madai hayo, akisema vyeti hivyo havitabadilishwa kutoka kwenye mfumo wake bali vimesitishwa kugawanywa ili baraza lijiridhishe na baadhi ya vitu.
    “Vyeti hivi baraza limevigawa hivi karibuni na lilichofanya sasa limezuia kwanza shule zisigawe mpaka litakapotoa maelekezo mengine, msingi huo wa kuzuia uko kwenye hoja ya kuhakikisha tu kwamba linajiridhisha kwenye takwimu zake kama zimekaa sawasawa katika vyeti vilivyokwenda kila shule.

    “Baadhi ya vyeti kwenye mkoa wa Dar es Salaam vipo Necta, lakini kwenye mikoa mingine yote viko shuleni,” alisema Dk Msonde na kuongeza;
     
    “Kama mkuu wa shule alikuwa amegawa vyeti viwili, vitatu kabla havijarejeshwa baraza ni suala jingine, lakini kiujumla kinachofanywa na baraza hapa ni kuhakiki cheti hiki, kama vimekaa kama utaratibu wetu ulivyo.”

    Alisema suala la kubadilisha kutoka kwenye GPA kwenda kwenye divisheni halipo na kwamba matokeo yaliyotangazwa kwa utaratibu wa GPA vyeti vyake vitaendelea kuwa katika mfumo wa GPA na matokeo yaliyotangazwa kwenye utaratibu wa divisheni vyeti vyake vitabaki kuwa kwenye divisheni.

    Alisema kwa wale ambao tayari wako nje ya nchi, hakuna atakayeathirika na kama baraza likihitaji cheti chake litafanya utaratibu wa kukipata.
     
     Credit;Mpekuzi blog
     
     

    Monday, 22 February 2016

    Dk. Shein awataka vijana kuyalinda mapinduzi

    By: Unknown On: 21:52
  • Share The Gag
  • VIJANA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kujizatiti zaidi kulinda na kuendeleza mapinduzi ya mwaka 1964 na muungano uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
    Wito huo umetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohamed Shein, alipokuwa akizungumza na viongozi wa UVCCM Mkoa wa kichama wa Mjini Unguja.
    Alisema kuwa kuyalinda na kuyadumisha mapinduzi na muungano ni kulinda na kuendeleza amani na utulivu nchini, hivyo vijana hilo ndilo jukumu lao la msingi kama warithi wa taifa.
    “Hakuna mbadala wa mapinduzi, hakuna mbadala wa muungano, wala hakuna mbadala wa amani na utulivu wa nchi yetu, hivyo ni lazima vijana mchukue nafasi yenu kulinda misingi hiyo ya nchi yetu,” alisisistiza Dk. Shein kwa viongozi hao wa vijana kuanzia ngazi ya matawi hadi mkoa.
    Alisema ni wakati wao vijana wa sasa kuchukua majukumu hayo kwa kuwa hata wao walikuwa vijana na walihimizwa kufanya hayo hayo na viongozi wao, ndiyo maana wamefanikiwa kukabidhiwa uongozi wa nchi.
    “Ni lazima vijana mzingatie historia ya ukombozi wa nchi yenu na ya uongozi wake ndiyo mtaweza kuwa viongozi wazuri na tegemeo la maendeleo ya nchi yenu,” alisema.
    Dk. Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alisema vijana ni lazima wasome na kukumbushana mara kwa mara historia ya mapambano ya uhuru wa Zanzibar kwa kuwa ni muhimu katika kujenga mustakabali wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

    Chanzo Mtanzania.

    Mwanamkakati wa Maalim Seif aswekwa ndani Z’bar

    By: Unknown On: 21:47
  • Share The Gag
  • Na Khelef Nassor, Zanzibar MWANAMKAKATI  wa aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Mohamed Sultan Mugheiry, maarufu kwa jina la Eddy Riyami, amewekwa ndani na Jeshi la Polisi mjini Unguja kwa tuhuma za kumtukana Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
    Eddy Riyami ambaye ni mmoja wa wana mkakati wa timu ya ushindi wa aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikutwa na mkasa huo jana baada ya kuitwa polisi kutoa maelezo kutokana na tuhuma zinazomkabili.
    Riyami ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, alikwenda Polisi Makao Makuu kuitikia wito wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, SSP Simon Pasua, huku akiandamana na Mwanasheria wa CUF, Masoud Faki Masoud.
    Akizungumza na MTANZANIA jana, mwanasheria huyo alisema Riyami anatuhumiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya kimtandao.
    Alisema licha ya kuzikana tuhuma hizo, lakini Jeshi la Polisi bado lilimshikilia kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
    “Ni kweli ameshikiliwa na polisi kwa ajili ya kupitisha uchunguzi na yupo Polisi Madema, eti Eddy kaambiwa kamtukana Dr. Shein kwenye ‘audio’ ambayo hata si sauti yake, lakini dhamana ipo wazi na tutamchukulia dhamana,” alisema Masoud.
    Akizungumzia kukamatwa kwa Riyami, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Salum Msangi, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
    “Kitu ninachoweza kuthibitisha ni kuwa tunamshikilia Riyami kwa ajili ya kupitisha uchunguzi,” alisema Naibu Kamishna Msangi.
    Februari 17, mwaka huu Ofisi ya Mkurunzi na Makosa ya Jinai, ilimwandikia Riyami barua ya wito na kumtaka kufika ofisi ya upelelezi iliyopo Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
    Riyami alitii wito huo ambapo wiki iliyopita alikwenda lakini mmoja wa maofisa wa Jeshi la Polisi aliyemwandikia barua alikuwa nje ya Zanzibar kwa shughuli za kikazi na kumtaka kwenda jana jumatatu
    Riyami si mwanachama wa CUF, lakini mara kadhaa amekuwa akitumiwa na chama hicho kwa ajili ya mikakati mbalimbali pamoja na ushauri.

    Chanzo Mtanzania.

    Miguu yamsumbua Samuel Sitta

    By: Unknown On: 21:45
  • Share The Gag
  • Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam HALI ya afya ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, inaendelea vizuri baada ya kusumbuliwa na goti kwa siku za hivi karibuni.
    Sitta mmoja wa mawaziri machachari ambao wamepata kuhudumu awamu zote nne zilizopita, alipelekwa Hospitali ya Agha Khan, Dar es Salaam kwa ajili ya kukandwa goti ambalo limekuwa likimsumbua.
    Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, mtoto wa waziri huyo, Benny Sitta, alisema baba yake anaendelea vizuri tofauti na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa anaumwa.
    “Baba anaendelea vizuri, amekuwa akisumbuliwa na goti hivyo hulazimika kwenda Hospitali ya Agha Khan kukandwa kutokana na tatizo linalomsibu,” alisema Benny.
    Mwaka jana, Sitta alikuwa miongoni mwa makada 40 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliotangaza nia ya kugombea urais, huku akieleza anataka kulifanyia taifa mambo matano, ikiwa ni pamoja na kutenganisha biashara na siasa na kusimamia maadili ya viongozi wa umma.
    Baada ya kuenguliwa na Kamati Kuu ya CCM, Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, alitangaza kustaafu masuala ya siasa.
    Sitta aliongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa kiasi cha kumfanya apewe kirahisi uenyekiti wa Bunge la Katiba na kutangaza tena nia yake ya kutaka kurudi tena kuongoza Bunge la 11.
    Lakini hakufanikiwa kupitishwa kuwania urais wala kugombea uspika, ambao aliahidi kuwa angeenguliwa angefika hata mahakamani.
    Mambo mengine aliyoahidi kuyafanya kama angechaguliwa kuwa rais, ni kusimamia Muungano, kukamilisha mchakato wa kuandika Katiba mpya, kuweka mfumo wenye motisha kwa wote ili kuchochea uchumi endelevu na wa viwanda, vita dhidi ya rushwa na kuiimarisha CCM kiuchumi.
    Sitta alisema mikataba mibovu ya huduma na mauzo, ununuzi hewa, ununuzi uliojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni kwa rushwa na hasa rushwa katika ajira, kumelisababisha taifa hasara kubwa.
    Alisema hatua ya pili ya kupambana na rushwa ni kutunga sheria mpya kali na ambazo zitakuwa na matokeo ya kumzuia mtu asitamani kusaka rushwa.

    Chanzo Mtanzania.

    Wiki mpya majipu matano

    By: Unknown On: 21:43
  • Share The Gag
  • TUNU NASSOR NA FROLIAN MASINDE, DAR ES SALAAM WAKATI Watanzania wakiingia katika juma jipya kwa ajili ya majukumu ya ujenzi wa taifa, mawaziri wa Rais Dk. John Magufuli, wameendelea kutumbua majipu bila ganzi kwa watendaji wa Serikali.
    Jana kwa nyakati tofauti Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, ametangaza kutumbua watendaji watatu, huku mwenzake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, akitumbua watendaji wawili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN).
    Akizungumza jana Dar es Salaam, Waziri Kairuki alitangaza kumsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Said Nassoro kutokana na utendaji usioridhisha.
    Pia amewasimamisha kazi Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Tabora, Silvanus Ngata na Dk. Joseph Mbwiro wa tawi la Dar es Salaam kutokana na ubadhirifu wa fedha.
    Waziri Kairuki aliwaambia waandishi wa habari kuwa Nassoro ameshindwa kuwasimamia watumishi na kusababisha matumizi mabaya ya fedha.
    Alisema kutokana na makosa ya kiutendaji, Nassoro aliotoa mwanya kwa viongozi wa matawi kufanya ubadhirifu wa mali za umma kwa masilahi binafsi.
    “Kwa mfano aliyekuwa mkuu wa tawi la Mtwara, Silvanus Ngata alizidisha fedha za gharama za ujenzi tofauti na zilizoainishwa.
    “Pamoja na tuhuma hizo, Nassoro hakuchukua hatua yoyote zaidi ya kumbadilisha kituo cha kazi na kumpeleka mkoani Tabora,” alisema Kairuki.
    Kuhusu Dk. Mbwiro, alisema kuwa alitumia vibaya fedha za ada na kusababisha hasara ya shilingi bilioni moja alipokuwa anakaimu kitengo cha fedha.
    “Pamoja na tuhuma hizi, bado aliteuliwa kuwa mkuu wa chuo wa tawi la Dar es Salaam nafasi ambayo alikuwa akiitumikia hadi sasa,” alisema Waziri Kairuki.
    Alisema ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zilionyesha kuwapo ubadhirifu huo.
     NAPE NA JIPU TSN
    Nayo Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), imemsimamisha kazi Mhariri Mtendaji wa magazeti hayo, Gabrieli Nderumaki, kupisha uchunguzi kutokana na utendaji usioridhisha ndani ya kampuni hiyo.
    Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Profesa Moses Warioba, alisema hatua ya kumsimamisha kazi Nderumaki imetokana na kuwapo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo na nafasi yake itachukuliwa na Naibu Mhariri, Tumma Abdallah.
    “Kumekuwa na mambo mengi yanayofanyika bila kufuata utaratibu ndani ya kampuni hii ikiwamo wafanyakazi kutoelewana na menejimenti katika kulipwa stahili zao, pamoja na wafanyakazi kupewa  majukumu ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza,” alisema Prof. Warioba.
    Alisema pamoja na hayo, pia bodi imetengua uteuzi wa Felix Mushi, ambaye alikuwa Meneja Mauzo na Masoko katika kiwanda cha uzalishaji kwa kukosa sifa na utendaji mbovu uliosababisha kampuni kushuka katika uzalishaji.
    Hatua hiyo ya kuwawajibisha watendaji hao imetokana na ziara iliyofanywa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika kampuni hiyo, ambapo pia hakuridhiswa na utendaji mbovu uliosababisha wafanyakazi 21 kuacha kazi.
    “Nataka bodi itafakari juu ya malalamiko yaliyopo kwa wafanyakazi na wachukue hatua kabla mimi sijakutana na wafanyakazi hao wiki ijayo ili kujua mapungufu yako wapi,” alisema Nape.
    Hata hivyo, bodi hiyo ya wakurugenzi inaendelea kutafuta namna ya kuboresha utendaji ndani ya kampuni hiyo ili iendane na kasi iliyopo katika uzalishaji wa magazeti kwa kiwango kikubwa.
     MAJIPU YALIYOTUMBULIWA
    Katika siku zaidi ya 100 za uongozi wa Rais Magufuli, watendaji zaidi ya 150 wamefukuzwa kazi kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za ufisadi.
    Katika mpango wake huo Rais Magufuli aliwang’oa vigogo wapatao 23 wa Mamkala ya Bandari (TPA) pamoja na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa makontena.
    Bodi hiyo ilikuwa na vigogo kadhaa akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Maji (Ewura), Haruna Masebu.
    Hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, ilitokana na kushindwa kuisimamia vyema TPA, hali iliyosababisha makontena 2,716 kutolewa katika Bandari ya Dar es Salaam bila kulipia kodi na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
    Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Magufuli ambaye pia alitengua uteuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaban Mwinjaka kutokana na ubadhirifu wa Sh bilioni 16 ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRL).
     JIPU LA RAHCO
    Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli nchini (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito.
    Uamuzi huo umelenga kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
     JIPU LA TAKUKURU
    Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, Desemba 16, mwaka jana.
    Akitangaza uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Rais Magufuli kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa, hususani kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.
     JIPU LA NIDA
    Januari 26, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza pia kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu.
    Maimu alisimamishwa pamoja na maofisa wengine wanne wa NIDA kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.
    Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
    Balozi Sefue alisema taarifa zilizomfikia Rais zinaonyesha kuwa NIDA hadi wakati huo ilikuwa imetumia Sh. bilioni 179.6 kiasi ambacho ni kikubwa.
     WALIOKIUKA AMRI YA KUSAFIRI NJE
    Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza  kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takukuru ambao walisafiri nje ya nchi licha ya Serikali kupiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma.
    Watumishi hao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais ama Katibu Mkuu Kiongozi.

    Chanzo Mtanzania.