Sunday, 13 December 2015

Mwakyembe- Nitaenda sawa na Magufuli

By: Unknown On: 00:28
  • Share The Gag
  • Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema atafanya kazi kwa kasi ya Rais Magufuli katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika wizara hiyo.
    Amesema changamoto ziko nyingi kuanzia chini mpaka juu, katika Mahakama, magereza na kwingineko, hivyo aliomba apewe muda kuangalia hali ikoje ili abadilishe mifumo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Akizungumzia suala la Katiba Mpya, alisema Rais alieleza vizuri kuwa litafanyiwa kazi, kwani halikuishia pabaya hivyo muda ukifika litakamilika.
    Alisema watafanya kazi kubwa ili mfumo wa sheria usiwe pingamizi, bali uendeleze kasi aliyoanza nayo Rais Magufuli. Nape Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye alisema atatengeneza utaratibu katika wizara hiyo, ili kuondoa utamaduni wa mtu mmoja kufanya mambo mengi peke yake na kuahidi kuwa msikivu na kutengeneza sheria, ili kila mmoja atimize wajibu.
    Akizungumzia changamoto katika michezo, Nape alisema tatizo katika michezo ni usimamizi wa sheria na kutokuwa na nidhamu kwa kila mtu kufanya anavyotaka. Alisema zamani wanamichezo walikuwa wakifanikiwa kutokana na nidhamu, hivyo watasaidiana na wadau mbalimbali kurudisha nidhamu.
    Manyanya na elimu ya juu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, alisema kinachosubiriwa ni kasi ya kuleta mabadiliko kwa muda muafaka na jambo la msingi ni kazi na kila mtu ahakikishe anatimiza wajibu wake.
    Alisema changomoto katika wizara hiyo ni nyingi, ikiwemo suala la mikopo ya elimu ya juu na kusisitiza kwamba wanafunzi wote wenye sifa ya kupata mikopo, wanapaswa kupewa kwa kuwa huo ni mkopo ambao wataurudisha.
    Manyanya alisema wizara hiyo haitamvumilia mwalimu yeyote mzembe, atakayetumia muda wake vibaya kwa kutotimiza wajibu, kwa kuwa hatua zitakazochukuliwa ni kumfukuza kazi na sio kuhamishwa kituo cha kazi.
    Mhagama, Kairuki Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama, alimshukuru Rais kutambua mchango wake katika Serikali iliyopita na kilichobaki ni kutimiza wajibu wao katika wadhifa huo.
    “Rais katambua mchango wangu, nashukuru na sasa ni kuhakikisha nakwenda na kasi yake, ili tumsaidie kutimiza ndoto za wananchi na hasa kuondokana na tatizo la ajira,” alisema Mhagama.
    Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki alisema anawiwa deni kubwa kuhakikisha anakwenda na kasi ya utendaji kazi ya Rais Magufuli.

    Created by Gazeti la HabariLeo.

    Saturday, 12 December 2015

    Wafanyabiashara 15 Waliokaidi Agizo la Rais Kukiona Cha Moto

    By: Unknown On: 23:46
  • Share The Gag

  • MAKAMPUNI 15 yaliyokwepa kodi baada ya kutorosha makontena yao, yamejisalimisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini yameshindwa kulipa kodi ndani ya siku saba za msamaha wa Rais John Magufuli.

    Kodi inayodaiwa kwa kampuni hizo ni Sh bilioni 3.75, hivyo watachukuliwa hatua za kisheria kwa kukwepa kulipa kodi, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

    Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango alisema hayo jana wakati akielezea makusanyo ya kodi ya makontena yaliyoondolewa katika bandari kavu ya Azam, kinyume cha sheria pamoja na kumalizika kwa siku saba alizotoa Rais Magufuli kwa wafanyabiashara hao kulipa kodi waliyokwepa, bila kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.

    Dk Mpango alisema siku hizo saba zimefikia kikomo juzi, hivyo hatua kali za kisheria kwa wafanyabiashara ambao hawakulipa kodi katika kipindi hicho zinafuata hivyo wasubiri cha moto.

    “Tumewasihi waje kulipa kwani huruma ya Rais sasa imeisha... tulifanya uhakiki na kuthibitisha kuwa kampuni hizo zipo. Wamekuja kulalamika lakini hakika hakuna atakayesamehewa kulipa na sasa tunafuata mkondo wa sheria ili kuwafikisha mahakamani,” alisisitiza.

    Wadaiwa 
    Alitaja kampuni hizo kuwa ni Ahmed Saleh Tawred anayedaiwa Sh milioni 59.23; Cla Tokyo Limited Sh milioni 77.52; Farida Abdullah Salem Sh milioni 75.33 na Juma Kassem Abdul Sh milioni 190.18.

    Wengine ni Libas Fashion Sh milioni 52.94; Rushy Wheel Tyre Center Co Ltd, Sh bilioni 1.8; Said Ahmad Hamdan Sh milioni 68.36; Said Ahmed Said Sh milioni 68.73 na Salum Continental Co Ltd Sh milioni 151.17.
     
     Pia yumo Salum Link Tyres Sh milioni 343.44; Simbo Yonah Kimaro, Sh milioni 69.22; Snow Leopard Building Material Co Ltd Sh milioni 93.97; Swaleh Mohamed Swaleh Sh milioni 34.68; Tybat Trading Co Limited, Sh milioni 598.69 na Nasir Saleh Mazrui Sh milioni 70.10.

    Alisema mpaka kufikia jana TRA walikuwa wamekusanya Sh bilioni 10,643.004,948.46 kutoka kwa kampuni 28 ambapo kampuni 13 zimelipa kodi yote iliyokadiriwa, ambayo ni Sh 4,167,130,173.89 na Sh 2,303,637,554.57 kutoka kampuni 15 zilizolipa sehemu ya kodi iliyokadiriwa.

    Dk Mpango alisema Sh bilioni 4.17 zimelipwa na kampuni ya Azam ICD, ikiwa ni dhamana ya kodi iliyokwepwa, hivyo atatakiwa kumaliza kulipa kodi yote inayodaiwa kwa mujibu wa nafasi yake kama mwenye dhamana.

    Alisema wakati utekelezaji huo ukiendelea, ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi hiyo ya makontena yaliyoondolewa bandarini kinyume cha sheria na taratibu za forodha, TRA imefungua akaunti maalumu katika Benki Kuu yenye namba 9921169785 inayoitwa Commissioner for Customs and Excise – Container Account.

    Kwa mujibu wa Dk Mpango, mpaka sasa watumishi 36 wa TRA wanaotuhumiwa kushiriki katika upotevu wa kodi kutokana na makontena hayo kuondoshwa bandarini.

    Watumishi wachongewa 
    Aidha, alisema TRA imepata taarifa zisizopungua 15 kutoka kwa wananchi kuhusu mali za kifisadi na mwenendo mbaya wa baadhi ya watumishi na walipakodi wanaokwepa kodi. 
     
    Aliwashukuru wananchi waliotoa taarifa na kuwaomba wengine wajitokeze kutoa taarifa zaidi na mamlaka hiyo inawahakikishia kuwa itawalinda.

    Dk Mpango alisema wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais katika ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni pamoja na kupiga picha makontena yote badala ya sampuli ya kontena ilivyo sasa na wanafanya utaratibu wa kupata mashine za kupiga picha za nyongeza.
    Credit;Mpekuzi blog

    Thursday, 10 December 2015

    Mjadala waendelea mkutano wa Paris

    By: Unknown On: 22:20
  • Share The Gag
  • Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amewasilisha rasimu ya mkataba mpya kwa wajumbe katika mkutano mkuu unaojadili kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi mjini Paris, kwa usiku wa pili wa majadiliano.
    Fabius amesema kwamba lengo lao kuu ni kuhitimisha mazungumzo kwa dhima, sheria, matarajio,na makubaliano ya haki na ya kudumu mpaka kufikia siku ya Ijumaa, nakuongeza kusema kwamba wajumbe wa mkutano huo wanakaribia kufikia makubaliano ya mwisho.
    Awali, mkurugenzi wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachojishughulisha na mazingira, Achim Steiner, alisema kwamba wajumbe wanajadiliana kuhusiana na masuala matatu ama manne, ikiwa ni pamoja na mgawanyiko kati ya mataifa tajiri na maskini zaidi dhidi ya fidia kwa kuongezeka joto duniani lilikuwa ni moja ya suala ambalo bado liko mezani kwa majadiliano.
    "Wote tunaelewa ukweli kwamba ushirikiano unahitajika ili kuweza kupata suluhisho la kila mmoja na kila mmoja aridhike. Hiyo ndio kazi ambayo inatukabili kwa sasa .Tunataka makubaliano.Tunakaribia kuyapata,hivyo tunapaswa kuonesha umuhimu wa kila mmoja kuchukue majukumu yake katika masaa machache yajayo.Kwa maneno mengine,huu ni muda wa kupata makubaliano."

    Created by BBC Swahili.

    JPM arejesha sura 13, atema 13 wa Kikwete

    By: Unknown On: 22:15
  • Share The Gag
  • Waziri Mteule wa Habari, Nape Nnauye.
    RAIS John Magufuli amerejesha sura 13 zilizokuwemo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, ambao sasa wanaunda Baraza lake la Mawaziri la watu 34 na kuwatupa mawaziri wengine 13 walioshinda ubunge.
    Kati ya sura hizo, saba walikuwa mawaziri na watano walikuwa ni manaibu waziri, ambao Dk Magufuli amewaamini na sasa watakuwa mawaziri kamili, ambao wataungana naye kuunda Serikali ya Awamu ya Tano.
    Mawaziri 7 wa JK warudishwa George Simbachawene ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini sasa anakuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, William Lukuvi amebaki Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Harrison Mwakyembe kutoka Ushirikiano wa Afrika Mashariki na sasa anakuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
    Mwingine ni Profesa Makame Mbarawa ametoka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia sasa anakuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jenista Mhagama ametoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge na sasa ataongoza Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu na Dk Hussein Mwinyi aliyebakizwa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Mwingine ni Profesa Sospeter Muhongo.
    Wakati huo, aliteuliwa na Rais kuwa mbunge, lakini safari hii ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini. Manaibu waziri 5 wa JK wapanda Manaibu wa JK waliopandishwa na Magufuli ni January Makamba anakuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto), Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na Uwekezaji), Mwigulu Nchemba (Kilimo, Mifugo na Uvuvi) na Angela Kairuki (Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora) na Charles Kitwanga (Mambo ya Ndani ya Nchi.
    Mawaziri waliotupwa nje ambao ni wabunge ambao wameshinda ubunge, lakini hawakurudi kwenye Baraza la Mawaziri ni Dk Mary Nagu aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi Rais, Mahusiano na Uratibu, Profesa Jumanne Maghembe (Maji), Dk Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Hawa Ghasia (Tamisemi), Sophia Simba (Jinsia, Wanawake na Watoto), Saada Mkuya Salum (Fedha) na George Mkuchika (Utawala Bora).
    Manaibu waliotupwa nje ambao ni wabunge, ni Stephen Masele ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Charles Tizeba (Uchukuzi), Greyson Lwenge (Ujenzi), Janet Mbena (Viwanda na Biashara), Juma Nkamia (Habari) na Mahmoud Mgimwa (Maliasili na Utalii).
    Mawaziri na manaibu walioshindwa kwenye uchaguzi Mawaziri wa JK walioshindwa Uchaguzi Mkuu na hawakufikiriwa tena na Magufuli ni Stephen Wassira (Kilimo, Chakula na Ushirika), Christopher Chizza (Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Fenella Mukangara (Habari), Godfrey Zambi (Naibu-Kilimo), Aggrey Mwanry (Naibu-Tamisemi), Anne Kilango (Naibu-Elimu) na Dk Steven Kebwe (Naibu-Afya).
    Mawaziri walioteuliwa na JK waliosahauliwa na JPM ni Dk Rose Migiro (Sheria na Katiba) yeye aliteuliwa kuwa mbunge na JK na safari hii hakugombea tena ubunge. Mawaziri wa JK walioshindwa kwenye kura za maoni Gaudetia Kabaka (Kazi na Ajira), Dk Bilinith Mahenge (Mazingira), Dk Seif Idd (Afya), Dk Titus Kamani (Uvuvi na Mifugo), Mathias Chikawe (Mambo ya Ndani), Adamu Malima (Naibu-Fedha), Kaika Telele (Naibu-Mifugo na Uvuvi), Amos Makalla (Naibu-Maji), Dk Abdallah Juma Abdallah (Naibu-Afrika Mashariki), Mahadhi Juma Maalim (Naibu Mambo ya Nje), Pereira Ame Silima (Naibu Mambo ya Ndani) na Pindi Chana (Naibu-Wanawake).
    Mawaziri na manaibu wa JK ambao safari hii hawakugombea ubunge ni Mizengo Pinda (Waziri Mkuu), Bernard Membe (Mambo ya Nje), Profesa Mark Mwandosha (Kazi Maalumu), Samuel Sitta (Uchukuzi), Dk Makongoro Mahanga aliyehamia Chadema. Mawaziri wa JK ambao walifariki dunia ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda na Celina Kombani (Utumishi).

    Created by Gazeti la HabariLeo.


    Mwasisi wa CHADEMA ( Edwin Mtei ), Prof. Lipumba na Spika Msekwa Wammwagia Sifa Rais Magufuli

    By: Unknown On: 22:11
  • Share The Gag

  • Watanzania wa Kada mbalimbali wamempongeza Rais John Magufuli kwa kuokoa mamilioni ya shilingi ambayo yangetumika kwenye maazimisho ya miaka 54 ya uhuru wa Tanzania .

    Mwenyekiti wa kwanza wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia Muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, amesema kuwa uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta sherehe za uhuru utakuwa umeleta tija kubwa kwa taifa ambapo miaka mingi taifa limekuwa likichezea mabilioni ya shilingi bila faida kwa taifa.

    Mtei amesema kuwa sherehe hizo zilizokuwa zikifanyika kwa shamrashara  zilikuwa zinagharimu fedha za walipa kodi kwa anasa za kula,kunywa na kulewa huku watanzania wakikosa huduma muhimu.

    Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),Profesa Ibrahim Lipumba ameshauri kuwa sherehe hizo zifanyeke mara moja kila baada ya miaka mitano ambapo zisihusishe matumizi mabaya ya fedha za wananchi kama zilivyokuwa za awamu iliyopita kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

    Naye spika wa kwanza wa Bunge la Tanzania Pius Msekwa amesema kuwa kitendo hicho kinapaswa kuungwa mkono kwa kila ambaye anayeitakia mema Tanzania.
     
    Sherehe hizo jana zimewaunganisha waatanzania wote kwa kufanya jambo moja ambapo sherehe hizo zilikuwa zikifanyika Dar es Salaam pekee kwa gharama kubwa lakini jana  zilikuwa za nchi nzima na zenye maslahi na taifa.
    Credit; Mpekuzi blog

    Uteuzi mawaziri wagusa wengi, wapongezwa

    By: Unknown On: 22:08
  • Share The Gag

  • Rais John Magufuli akisalimiana kwa furaha na wanahabari mara baada ya kutangaza baraza lake la mawaziri, Ikulu Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).

    WATU wa kada mbalimbali wamepongeza uamuzi wa Rais John Magufuli kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri kwamba hatua hiyo itasaidia kuwa na watu wachache watakaofanya kazi ya kusaidia kuinua uchumi wa nchi. Aidha, uteuzi wake wa Baraza la Mawaziri umewagusa viongozi wa taasisi mbalimbali na wasomi nchini ambao wamelitaja baraza hilo kuwa ni la viwango lililozingatia weledi.
    Kwa upande wao, viongozi wa dini wamempongeza Dk Magufuli kwa uteuzi wa Baraza la Mawaziri ambalo wamesema ni dogo lenye weledi lililobeba vijana wachapakazi. Jana, Dk Magufuli alitangaza Baraza jipya la Mawaziri ambalo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, ndio baraza lenye idadi ndogo ya wizara na mawaziri wake. Lina wizara 18, zenye mawaziri 19, ambapo kati ya hao, wizara nne hazijapata mawaziri, huku idadi ya manaibu waziri ikiwa ni 15.
    Wangwe apongeza idadi ndogo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini (REPOA), Profesa Samuel Wangwe, amesifu Rais kupunguza mawaziri kwa maelezo kuwa mawaziri ni watu wa kusimamia sera tu na watendaji wakubwa ni makatibu wakuu, wakurugenzi na watumishi wengine. Kuhusu mawaziri wa zamani kurejeshwa kwenye baraza, Profesa Wangwe alisema mawaziri waliorudi ni wazuri na wana kasi kubwa na ndio maana Dk Magufuli amewaamini na kuwateua wamsaidie kufanya kazi.
    “Watu wanabadilika kulingana na mawaziri, wengine ni watendaji wazuri ila inategemea na kiongozi wao,” alisema Profesa Wangwe na kuongeza “Sio suala la kuangalia ku-balance (kuweka uwiano) mikoa, baraza hili ni la kazi.”
    Naye Mwanaharakati wa Masuala ya Haki za Binadamu, Onesmo Olengurumwa amepongeza hatua ya Dk Magufuli ya kupunguza Baraza la Mawaziri kwa maelezo kuwa nchi haiwezi kutegemea wanasiasa kufanya kazi, bali wanaotakiwa kufanya hivyo ni watendaji walioko kwenye wizara ambao wamedumu humo kwa muda mrefu.
    “Ukiangalia wanasiasa hawa wanakaa muda mfupi wanaondoka kwa kubadilishwa au kufukuzwa, hivyo Dk Magufuli ana haki ya kupunguza baraza lake,” alisema Olengurumwa na kuongeza kuwa, wananchi walitarajia angekuja na sura nyingi mpya, lakini badala yake amerejesha nusu ya baraza la serikali iliyopita jambo ambalo alisema linampa wasiwasi kama wanaweza kumudu kasi ya Rais huyo.
    Kuhusu wizara nne kutokuwa na mawaziri, Olengurumwa alisema ni jambo jema kwa kuwa wizara hizo ni nyeti zinahitaji kuwa na watu makini, kwani ndio uti wa mgongo wa nchi.
    Bana:
    Rais amezingatia weledi, uzoefu Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Siasa, Dk Benson Bana alisema Rais ameteua baraza hilo kwa kuzingatia weledi wa kila waziri kwa maana ya uzoefu na maarifa.
    Aidha, alisema amevutiwa na kitendo cha Rais Magufuli kuiweka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) chini ya ofisi yake, kwa kuwa wizara hiyo ndio inayogusa wananchi kwa maana ya huduma na ulinzi na usalama wao.
    Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani kwa Waislamu ya Islamic Peace Foundation (TIPF), Sadiki Godigodi amepongeza hatua ya Rais kupunguza idadi kwa kiasi kikubwa ya mawaziri, kwani ameonesha kujali maslahi ya nchi.
    Alisema kwa sura chache za zamani zilizorudi anaamini amefanya uchambuzi wa kina katika utendaji wao, hivyo kutaka kuendana na kasi ya Rais huyo mpya ili wasimuangushe, kwani amewaamini kuwapa nafasi hizo.
    Alisema kuacha kuteua mawaziri wa wizara nyeti kama Fedha, Uchukuzi na Ujenzi, Maliasili na Utalii na Elimu ni kuonesha asivyokuwa na masihara katika masuala nyeti na kutaka atakaowateua kuwa na kasi zaidi kama ilivyokuwa enzi zake akiwa Waziri wa Ujenzi.
    Tucta yamsifu kwa umakini Naye Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema amefurahi kwa baadhi ya mawaziri watendaji kurudi kwa lengo la kumsaidia Rais kwenda na kasi yake akiwemo William Lukuvi aliyekuwa ameanza vizuri kazi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
    Alisema ameonesha jinsi alivyo makini kwa kuteua baraza dogo, lenye watu makini na Baraza la Mawaziri aliloteua litamsaidia kupeleka mbele nchi na iwapo angekosea kazi aliyofanya kwa muda mchache isingekuwa na maana. Kilaini avutiwa na vijana Akizungumzia uteuzi huo, Askofu wa Kanisa Katoliki, Methodius Kilaini alisema baraza aliloliteua Rais John Magufuli ni zuri na dogo ambalo limebeba vijana wengi ambao wataendana na kasi yake.
    Alisema mawaziri waliokuwepo katika Serikali ya Awamu ya Nne na sasa hawakuchaguliwa hawakuwa wabaya, lakini wengi wao wasingeweza kuendana na kazi ya kiongozi huyo ambaye ameonekana kutaka kushirikiana na watu wenye kasi. ‘Mseto’ wamvutia Shehe wa Dar Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema Baraza la Mawaziri lililoteuliwa na Rais Magufuli ni la kipekee ambalo kila Mtanzania anapaswa kupongeza hatua hiyo.
    Alisema kitendo cha kuchanganya vijana ambao ni wachapakazi na mawaziri wazoefu ambao miaka yote ya uongozi wao, utendaji wao umeonekana kuwa mzuri utasaidia kuendana na kasi ya Rais Magufuli. “Mchanganyiko huu wa vijana wachapakazi na waadilifu pamoja na ambao wameshawahi kuwa mawaziri ni wazi kuwa watafanyakazi kuendana na kaulimbiu ya Rais Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu.’
    “Kuanzia viongozi wakubwa wa zamani na hawa vijana wapya wote wako vizuri wanaonekana ni wachapakazi, kikubwa ni kuwapa ushirikiano lakini pia tuwaombee ili waweze kututumikia vizuri sisi wananchi,” alisema Shehe Alhad. Alisema uteuzi huo wa baraza hilo dogo la mawaziri unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania ili lifikie malengo yaliyowekwa na Rais ya kuwatumikia wananchi ipasavyo.
    Baregu:
    Lingebanwa zaidi Naye aliyekuwa Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Profesa Mwesiga Baregu alisema Baraza lililotangazwa jana ni dogo kuliko lile lililopita, lakini lingeweza kuwa dogo zaidi na lenye tija.
    Alitolea mfano wa Marekani kuwa ina Baraza la Mawaziri 15 na China 20 na kwamba hata katika mapendekezo ya Tume hiyo katika Rasimu ya Pili ya Katiba ilieleza umuhimu wa kuwa na baraza lenye watu sio chini ya 15.
    Alisema kikubwa ni kufahamika kuwa waziri sio sehemu ya mgawo wa kula, badala yake kutambulika kuwa ni kazi. Kuhusu waliotajwa katika Baraza la Mawaziri, Profesa Baregu alisema kuna waliotajwa akitolea mfano wa Profesa Sospeter Muhongo ambaye alikuwa na mtazamo hasi jambo lisiloweka wazi ni ujenzi wa taswira ipi alionao.
    Alisema baraza hilo limeibua maswali mengi zaidi ya majibu hasa kutokuwa na semina elekezi ambayo kwa hilo, haioneshi baraza hilo litawajibika kwa Rais ama litawajibika kwa umoja kama timu shirikishi kwa Watanzania.
    Dodoma yamshangilia Muhongo Mkoani Dodoma, wakazi wake wamesifu uteuzi huo wakisema umefanyika baada ya kufanyika utafiti wa watu wanaoweza kwenda na kasi ya Rais, na wamefurahishwa na uteuzi wa Profesa Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
    Mhadhiri wa Utafiti, Mitaala na Ufundishaji wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John (St John’s), Dk Michael Msendekwa alisema uteuzi umefanikiwa kutokana na kufanyika kwa utafiti wa kina. Alisema uteuzi huo ni wa kitafiti zaidi, kwani kuna wizara zimeachwa wazi, ikimaanisha Rais yuko makini kutafuta watu wanaofanya kazi kweli.
    Alisema anataka kuhakikisha walioteuliwa wanakuwa mfano bora wa utendaji. Alisema uteuzi wa Muhongo ni mzuri, kwani ni mchapakazi na kwa uteuzi huo amepatia licha ya kipindi kilichopita mambo ya chuki na siasa yaliingilia kumtoa.
    Naye mkazi wa Zuzu, Amos Magimba alisema amefurahishwa na uteuzi huo hasa Profesa Muhongo kwani anaamini sasa vijiji vyote vitapata umeme na kwamba baraza hilo ni la kisayansi zaidi na kuwataka walioteuliwa wakachape kazi ili kupunguza changamoto ya umasikini nchini. Mkazi wa Viwandani, Mary Aloyce alisema amefurahishwa na uteuzi huo, akisema haukuwa wa kiupendeleo.
    Imeandikwa na Halima Mlacha, Shadrack Sagati, Theopista Nsanzugwanko, Sophia Mwambe, Katuma Masamba, Lucy Lyatuu (Dar), na Sifa Lubasi, Dodoma.

    Created by Gazeti la HabariLeo.
    By: Unknown On: 22:05
  • Share The Gag
  • Namba za Simu za Kuripoti Kero TRA na taarifa za siri za Watumishi Wabadhirifu

    Mpekuzi blog

    Dk Mpango ametaja namba za simu na kuomba wananchi waripoti taarifa zinazohusu watumishi wa ofisi ya Mamlaka na Mapato Tanzania (TRA), wanaojilimbikizia mali kinyume na kanuni za utumishi wa umma.

    Pia ameomba namba hizo zitumike kutoa taarifa kuhusu kero wanazokumbana nazo wananchi katika ofisi za TPA.
    • Piga simu 0689 122 515
    • Tuma ujumbe mfupi wa maneno (sms) 0689 122 516
    Pia ametoa namba yake kuwa ni 0787 570 714 na ya Naibu wake kuwa ni 0784 228 095

    Video iliyopachikwa hapo chini akizungumza Dk Mpango, ina maelezo haya na mengineyo.
    Credit; Mpekuzi blog