Tuesday, 23 February 2016

Uhamiaji wasafishwa Dar na Kilimanjaro

By: Unknown On: 22:38
  • Share The Gag

  • Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga
    WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ameagiza watumishi wa Idara ya Uhamiaji walioko katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam na Kilimanjaro (KIA), wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
    Katika maagizo ya waziri huyo, amesisitiza kuwa anataka kuwepo na mabadiliko makubwa katika vitengo mbalimbali vya idara ya uhamiaji ili kuboresha huduma na kuimarisha uadilifu katika vitengo hivyo.
    Aidha, utafiti uliofanywa hivi karibuni, umeonesha kuwa matatizo ya rushwa katika idara ya uhamiaji, yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka.
    Kitwanga alitoa maagizo hayo Dar es Salaam jana, alipozungumza katika kikao cha ndani na viongozi wa idara ya uhamiaji na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara.
    Pamoja na watumishi hao wa Idara ya Uhamiaji wa viwanja hivyo vya ndege kutakiwa kuhamishwa, wengine walioagizwa na waziri huyo kuhamishwa ni kutoka Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
    Aidha, ameagiza pia kuwa Wakuu wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo jijini Dar es Salaam, Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo, wahamishiwe maeneo mengine, wakiwemo watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka mitatu katika vituo hivyo.
    “Hatua hii inayochukuliwa ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali,” alisisitiza Kitwanga.
    Alisema katika kuisafisha idara hiyo, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa hakuna mtumishi anayeonewa wala kupendelewa, lengo likiwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wasiowajibika.
    Alisema kutokana na utafiti uliofanywa hivi karibuni, umeonesha kuwa matatizo ya rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia 30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka.
    Aidha, alisema asilimia 15 inahusisha vitendea kazi, mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia 10 huduma mbovu na asilimia tano ukabila na upendeleo.
    Aliwataka viongozi na watumishi wote katika idara hiyo kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi na kuepuka vitendo vya kupokea rushwa na kusaidia wahamiaji haramu na wauza dawa za kulevya.

    Chanzo HabariLeo.

    Kampuni Ya Kichina Matatani Kwa Kutengeneza Vibao Vya Namba Za Magari Kinyume Cha Sheria

    By: Unknown On: 22:36
  • Share The Gag

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya msako wa kushtukiza katika kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development Ltd iliyoko Barabara ya Nyerere Dar es salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema na kukamata vifaa pamoja na malighafi za kutengeneza na kutoa vibao vya namba za pikipiki kinyume na sheria.

    Katika msako huo uliofanyika tarehe 19 Februari 2016 katika kampuni hiyo, Maofisa wa TRA waliweza kukamata na kutaifisha vibao vyenye namba za pikipiki 2,500 na vibao 5,600 ambavyo havikuwa na namba. Pia maofisa wa TRA walikamata malighafi za rangi ya vibao katoni tatu, pamoja na mashine ya kupaka vibao rangi yenye uzito wa kilo 155.

    Mashine nyingine iliyokamatwa katika msako huo ni ya kutengeneza namba za magari yenye uzito wa kilo 902 ambayo imezuiwa isihamishwe kutoka katika kampuni hiyo pamoja na kompyuta mpakato ambayo imepelekwa katika maabara ya uchunguzi TRA kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

    Taarifa za kuwepo kwa utengenezaji wa vibao vya magari kinyume na taratibu na sheria zilitolewa na msamaria mwema ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni husika Donglinh Guo, Meneja wa Kiwanda Yong Qing Cheng na Meneja wa ghala Peng Zhan walikamatwa baada ya kutokea fujo wakati wa msako na kufikishwa katika kituo cha Polisi Changombe.

    Kampuni ya Tanzania China Trade and Tourism Development LTd ndio waingizaji pekee wa pikipiki za Falcon tangu mwaka 2008 ambapo inatuhumiwa kutoa vibao vya namba za pikipiki kwa wateja wake kwa shilingi 5,000 kinyume na sheria.Uchunguzi wa thamani ya kodi iliyopotea bado unaendelea.
     
    Vibao vya magari na pikipiki hutolewa na kampuni ambazo zinatambuliwa na TRA baada ya kupewa idhini. Kampuni hizo ni Masasi Sign, Auto Zone, Sign Industry, Kiboko, Budda Auto works, Parkinson Ltd na Next Telecom.

    Ili kujiridhisha kuwa kadi za pikipiki zinazotolewa kwa wateja wa kampuni hiyo ni halali, TRA ilifanya uchunguzi na kugundua kuwa kadi hizo zinatolewa kihalali.

    TRA inawatahadharisha wananchi kufuata taratibu na sheria ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea endapo watagundulika kujihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria.
     
    Credit; Mpekuzi blog

    Ndege iliyowabeba watu 21 yatoweka Nepal

    By: Unknown On: 22:34
  • Share The Gag
  • Ndege ndogo iliyowabeba abiria 21 imetoweka ikiwa maeneo yenye milima nchini Nepal.
    Ndege hiyo ilikuwa safarini kutoka Pokhara, magharibi mwa mji mkuu Kathmandu, kwenda Jomsom, eneo ambalo watu wengi wanaoenda kukwea milima ya Himalaya huanza safari yao ya kukwea milima hiyo.
    Hakuna viwanja vya ndege kati ya maeneo hayo mawili na inahofiwa kwamba ndege hiyo imeanguka.
    Ndege hiyo ni ya shirika la ndege la Tara Airlines.

    Chanzo BBC Swahili.

    Jengo la posta Dodoma lateketea kwa moto

    By: Unknown On: 22:31
  • Share The Gag

  • JENGO Posta lililopo katika eneo la sabasaba katika Manispaa ya Dodoma  jana limeteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa

    Akizungumzia kutekeleza kwa jengo hilo Meneja wa Posta Mkoa wa Dodoma, Magreth Mlyomi alisema mpaka sasa kuna hasara kubwa kutokana na kutekeleza jengo hilo sambamba na vifaa vyote vya ofisi.

    Mlyomi alisema licha ya kuwa hakuna mfanyakazi hata mmoja aliyepoteza maisha katika jengo hilo lakini mpaka sasa kuna vitendea kazi vingi vya ofisi pamoja na mizigo ya wateja imeteketea.

    “Kuna mizigo mingi pamoja na vifaa vya kazi vyote vimeteketezwa na moto na kwa taarifa nilizopata kulikuwa na mizigo ya watu, inaonesha kuwa chanzo cha moto ni umeme,” alieleza Meneja huyo.

    Akizungumzia kuhusu masuala ya miundombinu ya maeneo husika alisema ni mibovu na kutokana na changamoto hiyo suala hilo lipo katika mamlaka husika ya manispaa.

    Kwa upande wake katibu wa wafanyabiashara katika soko la Sabasaba katika Manispaa ya Dodoma, Gergod Lugusi alisema jana saa nne asubuhi kulitokea moto mkali ambao uliunguza jengo hilo.

    Alisema chanzo cha moto huo inasemakana kuwa ni tatizo la umeme na uongozi ulilazimika kutoa taarifa katika kikosi cha zima moto na bila kuchelewa walifika kwa wakati.

    Hata hivyo alisema licha ya kufika kwa wakati katika tukio bado kikosi hicho kilikutana na kikwazo kwa kutokana na miundombinu kuwa mibovu na migumu kupitika.
    Credit;Mpekuzi blog

    Utafiti zaidi wafanywa Brazil kuhusu Zika

    By: Unknown On: 22:27
  • Share The Gag
  • Wanasayansi wa Marekani wanachunguza uhusiano kati ya virusi vya Zika na hali ya watoto kuzaliwa na vichwa vidogo
    Wanasayansi kutoka kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa CDC nchini Marekani wameanza kufanya utafiti nchini Brazil ili kujua uhusiano kati ya Virusi vya Zika na watoto kuzaliwa wakiwa na vichwa vidogo.
    Timu za wanasayansi zimekuwepo katika jimbo la Paraeeba, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, jimbo ambalo limeathirika zaidi na Virusi.
    Timu nane zinazoundwa na cdc na mawakala wa maswala ya afya walienda kwenye maeneo yaliyoathirika na kuchukua sampuli ya damu na kuwahoji wamama walioathirika na wamama ambao watoto wao walizaliwa wakiwa na vichwa vidogo.
    Katika kipindi cha majuma yajayo, watakusanya taarifa kutoka kwa mamia ya wamama katika jimbo la Paraeeba, jimbo la pili lililoathirika zaidi.
    Katika Ripoti ya siku ya jumanne Wizara ya Afya ya Brazil imethibitisha watoto 587 wana vichwa vidogo asilimia 75 zaidi ya wiki iliyopita huku maelfu ya watoto wanachunguzwa.
    Baada ya kutangazwa hali ya taadhari ya kiafya, Rais wa Shirika la Afya duniani, Margaret Chan aliwasili Brasilia kufuatilia hali ilivyo.
    Akiwa huko alikutana Rais wa Brazil,Dilma Roussef siku ya jumanne na kusema kuwa anafurahishwa na namna Serikali inavyoshughulikia tatizo hilo na kutaka jamii isaidiwe kupambana na mbu anayeeneza virusi vya Zika

    Chanzo BBC Swahili.

    Nkurunziza atuma salamu, asema Burundi ni shwari

    By: Unknown On: 22:23
  • Share The Gag

  • Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

    RAIS Pierre Nkurunziza wa Burundi amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa hali ya Burundi ni shwari na kwamba tangu juzi nchi hiyo imepokea ugeni mkubwa wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na inatarajia kupokea marais watano kutoka nchi za Umoja wa Afrika kesho.
    Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, ujumbe wa Rais Nkurunziza umewasilishwa na Mjumbe Maalumu ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi, Leontina Nzeyimana Ikulu Dar es Salaam jana, alipokutana na Rais Magufuli na kufanya naye mazungumzo.
    Pamoja na kumpa taarifa kuwa Burundi inaendelea vizuri, Nzeyimana pia alimueleza Rais Magufuli kuwa Burundi ipo tayari kupokea nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka kwa Rwanda, ikiwa ni kwa mujibu wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaoelekeza kuwa nchi inayofuata kutoa Katibu Mkuu baada ya Katibu Mkuu wa sasa kumaliza muda wake, ni Burundi.
    Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi watatu wanaowakilisha nchi zao nchini.
    Balozi wa Uholanzi nchini, Jaap Frederiks aliwasilisha salamu za Mfalme wa Uholanzi, Mtukufu Willem- Alexander ambaye amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa alizoonesha katika mwanzo wa utawala wake katika kusimamia uadilifu serikalini na katika biashara na pia kuisaidia Mahakama.
    Alisema Uholanzi inaamini kuwa maeneo hayo ndio yamekuwa yakileta vikwazo vya maendeleo, biashara na uwekezaji, na alimhakikishia Rais Magufuli kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo kama ilivyofanya katika miaka 45 iliyopita huku akitaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano kuwa ni kilimo na nishati.
    Balozi wa India nchini, Sandeep Arya aliwasilisha salamu za Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ambaye pamoja na kuitaja Tanzania kuwa lango muhimu katika mpango wake wa ushirikiano na Afrika, alimhakikishia kuwa India itaendeleza uhusiano wake na Tanzania hususani katika biashara na uwekezaji ikiwemo kuunga mkono mpango wa ujenzi wa viwanda Tanzania.
    Kwa upande wake, Rais Magufuli aliwahakikishia mabalozi hawa kuwa serikali yake ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na nchi hizo.

    Chanzo HabariLeo.

    Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Akana Kutoa Amri ya Kufuta Matokeo ya Uchaguzi Zanzibar

    By: Unknown On: 22:21
  • Share The Gag


  • MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amesema hajahusika kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar kwa kumpigia simu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

    Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Chama ya Kibaha Mjini mkoani Pwani na kusema maneno hayo ni ya uongo, hayana ukweli wowote na watu hawapaswi kutoa shutuma hizo juu yake.

    Rais huyo wa Awamu ya Nne alisema maneno hayo hayana kichwa wala miguu wala hajawahi kumpigia simu Jecha kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwani tume hiyo inajitegemea.

    “Wasitoe lawama zisizohusika, wapuuzeni sikuwahi kufanya hivyo hata kwa Damian Lubuva wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania hivyo nashangaa watu wanavyosema kuwa nimehusika kufutwa uchaguzi huo,” alisema Kikwete.

    “Tume ya Zanzibar ni tume huru na inajitegemea kwani ina mambo yake hata Dk Ali Mohamed Shein (Rais wa Zanzibar) hana uwezo wa kuingilia na kuahirisha uchaguzi huo, watu hao wasipake watu matope wasio husika kwani kila mtu ana nafasi yake,” alifafanua Kikwete.

    Alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuwaombea Wazanzibari wafanye uchaguzi wao mkuu wa marudio kwa amani na utulivu ili wapate viongozi wao wa kuiongoza Zanzibar na wawaombee wagombea wa CCM washinde.

    Aidha, alisema chama hicho kinapaswa kuwaadhibu watu waliokihujumu chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa kutomwonea mwanachama, bali watende haki na si kwa kwa uonevu.

    Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao alisema Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka ameonesha njia ya kiongozi kutumia fursa kuboresha mazingira ya utendaji kazi Awali, Koka ambaye ndiye aliyejenga ofisi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 100, alisema aliamua kujitolea kujenga ofisi hiyo kwa lengo la kukisaidia chama kiendeshe shughuli zake.

    Koka alisema aliamua kujenga kama kumbukumbu kwa wanaKibaha ili iwe kielelezo cha uongozi wake kama mbunge wa Jimbo hilo kwa ajili ya kufanya shughuli za chama badala ya kufanyia sehemu zisizo na hadhi yao.
    Credit;Mpekuzi blog