Sunday, 7 August 2016

KRC Genk ya Samatta Imepoteza Mechi Dakika ya 90 Dhidi ya KAA Gent

By: Unknown On: 23:12
  • Share The Gag

  • Usiku wa August 7 2016 Ligi Kuu Ubelgiji iliendelea tena kwa klabu ya KAA Gent kuikaribisha KRC Genk katika uwanja wa GHELAMCO wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 20,000 ili kucheza mchezo wao wa pili wa Ligi Kuu Ubelgiji.

    Katika dakika zote 90 KRC Genk walicheza na kumiliki mpira kwa asilimia 40 wakati wenyeji wao KAA Gent walikuwa wameutawala mchezo kwa asilimia 60, licha ya KRC Genk kufanya mabadiliko katika safu ya ushambuliaji kwa kumtoa Nikolaos Karelis na kumuingiza mtanzania Mbwana Samatta dakika ya 66, walifungwa goli  1-0.

    KRC Genk kutokana na kuwa ugenini na kushambuliwa kwa kiasi kikubwa, hali ilikuwa mbaya dakika ya 90 baada ya KAA Gent kupata goli la ushindi na kujichukulia point tatu kupitia kwa mshambuliaji wao aliyeibuka mfungaji bora msimu uliopita Jeremy Perbet, Genk itacheza nyumbani August 13 2016 dhidi ya W. Bevern.


    Credit; UDAKU SPECIAL

    Mkuu wa Wilaya ya Nzega Awapiga Marufuku Madiwani na Wabunge Kufanya Mikutano ya hadhara nje ya maeneo yao waliyochaguliwa

    By: Unknown On: 23:06
  • Share The Gag

  • SERIKALI wilaya ya Nzega mkoani Tabora imepiga marufuku wabunge na madiwani wa vyama vyote, kutofanya mikutano ya hadhara nje ya maeneo yao waliyochaguliwa.

    Imechukua hatua hiyo ili kuepusha uchochezi wa kisiasa, ambao unaweza kujitokeza na kuhatarisha amani.

    Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla amesema viongozi hao wanapaswa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao ya uchaguzi.

    Amesema mbunge ama diwani, haruhusiwi kufanya mikutano nje ya eneo lake na endapo atabainika, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya dola.

    Amesema serikali imetoa agizo hilo ili wananchi waweze kupata taarifa za maendeleo na sikuendelea kutoa lugha za kukashifu viongozi wa serikali.

    Ngupulla aliongeza kuwa serikali haijakataza mikutano ya siasa, bali viongozi hao wanapaswa kufanya siasa safi katika maeneo yao na si kutoka nje ya maeneo yao, kwani wanaweza kuhatarisha amani ya nchi.



    ==

    Credit; Mpekuzi Blog 

    Thailand kuruhusu jeshi kuendelea kutawala

    By: Unknown On: 22:53
  • Share The Gag
  • Wapiga kura nchini Thailand wameidhinisha katiba mpya ambayo itaruhusu jeshi kuendelea kuongoza taifa ilo.
    Raia wa Thailand wakipiga kura Kampeni zote za kupinga uamuzi huo zikiwa zimezuiliwa na serikali ya kijeshi pasipo kutoa ufafanuzi wa kutosha.
    Matokeo ya kura zilizopigwa yanaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wapiga kura wanaunga mkono mabadiliko ya katiba. Huku asilimia hiyohiyo ndiyo itakayohusika kumchagua waziri mkuu.
    Nchi ya Thailand inaongozwa kijeshi baada ya kufanya mapinduzi miaka miwili iliyopita. Nchi ya Thailand inaongozwa kijeshi baada ya kufanya mapinduzi miaka miwili iliyopita. Jeshi linaamini kuwa katiba mpya itaimarisha nchi hiyo kufuatia misukosuko ya kisiasa iliodumu kwa takribani miaka kumi.

    Chanzo BBC

    Muhimbili kubadilisha figo, kutibu sikio

    By: Unknown On: 22:43
  • Share The Gag

  • Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Maseru


    HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imepanga kuanzisha huduma za matibabu ya figo na sikio kati ya Desemba mwaka huu na Januari mwakani. Itaanzisha huduma hiyo kwa lengo la kuhakikisha inapunguza gharama na idadi kubwa ya wagonjwa wanaoenda nje ya nchi, kutafuta huduma za matibabu.
    Akizungumza katika kipindi cha Funguka, kinachorushwa na televisheni ya Azam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Lawrence Maseru, alisema Septemba mwaka huu, madaktari bingwa wataenda India kwa ajili ya kupatiwa mafunzo kwa ajili ya huduma hizo za matibabu.
    Alisema hatua hiyo, imetokana na dhamira ambayo hospitali hiyo imejiwekea ya kuhakikisha huduma zote muhimu za matibabu, zinapatikana katika hospitali hiyo ili kuwapunguzia Watanzania gharama za matibabu kutoka hospitali za nje.
    Alikiri kuwa hospitali hiyo imekuwa ikishuhudia idadi kubwa ya wagonjwa wenye matatizo ya figo na masikio, wanaoenda nje ya nchi, kufuata huduma ya matibabu, hatua inayoigharimu serikali fedha nyingi.
    Akizungumzia huduma ya tiba ya masikio, alisema ni kitendo cha kuweka kifaa cha elektroniki sikioni kwa ajili ya kuwasaidia wenye matatizo ya kusikia. “Huduma hii kwa kawaida operesheni yake inagharimu takribani Sh milioni 100 kwa masikio yote mawili,” alisema.
    Alisema madaktari bingwa watakaokwenda India kwa ajili ya mafunzo zaidi kuhusu huduma hizo, watapatiwa mafunzo hayo kwa miezi miwili na pindi watakaporejea ndipo huduma hizo rasmi zitaanza kutolewa katika hospitali hiyo ya MNH.
    Alisema huduma ya tiba ya masikio ikianzishwa nchini itasaidia watoto na watu wazima wenye usikivu hafifu au wasiosikia kabisa kuwa na uwezo wa kusikia na hivyo kuweza kuendelea na shughuli zao za kawaida ikiwemo kuhudhuria shule za kawaida.
    Kuhusu huduma ya kubadilisha figo, Profesa Maseru alisema hospitali hiyo imekuwa ikipokea pia wagonjwa wengi wenye matatizo ya figo, ambapo wapo wagonjwa takribani 100 wanapatiwa huduma ya kusafishwa figo na wengine zaidi ya asilimia 80 wanahitaji operesheni ya kuwekewa figo mpya.
    Huduma ya chakula Akizungumzia suala la mfumo mpya wa kutoa chakula hospitalini na mgonjwa kuchangia gharama, uliositishwa na Serikali, Profesa Maseru, alisema huduma hiyo itaanza tena upya hivi karibuni baada ya serikali kuitaka hospitali kujipanga upya.
    “Si kuwa utaratibu huu umesitishwa ila tumeambiwa tujipange upya na hivi karibuni tutaanza kutoa hicho chakula kupitia kwa mzabuni kwa awamu. Tutaanza na kutoa chakula kwa wagonjwa ambao hospitali ndio inawagharamia chakula tuone changamoto zitakazokuwepo,” alisisitiza.
    Alisema endapo utaratibu huo, utaenda vizuri, hospitali itaandaa ripoti na baada ya miezi sita itajadiliana na wizara kuona namna ya kutekeleza vyema mfumo huo mpya.
    Alisema kwa kawaida hospitali nyingi duniani hutoa chakula kwa wagonjwa wanaolazwa, ila kwa hapa nchini utaratibu huo ulibadilika katika miaka ya 1990 kutokana na hali ya uchumi na ndugu ndio walioachiwa wajibu huo.
    Alisema MNH kwa sasa ina takribani wagonjwa 13,000 wanaolazwa kwa siku kati ya hao, hospitali hiyo huwapatia chakula wagonjwa 600 hadi 700 wanaotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam.
    Akizungumzia uhaba wa madaktari, alisema pamoja na kwamba kuna takribani vyuo saba vinavyozalisha madaktari nchini, bado idadi ya madaktari wanaohitimu kwa mwaka ambao ni 1,500 haitoshelezi mahitaji.
    Alisema kwa sasa Tanzania ina wastani wa madaktari mmoja kwa wagonjwa 18,000 wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) viwango vyake vinataka angalau daktari mmoja kwa wagonjwa 10,000.

    Chanzo HabariLeo.

    Rais Erdogan azungumzia sheria ya kifo nchini Uturuki

    By: Unknown On: 22:40
  • Share The Gag
  • Rais Erdogan amewaambia watu mjini Istanbul kuwa atapitisha sheria ya kifo kama italetwa tena na bunge la nchi hiyo.
    Rais wa Uturuki Recep Tyyip Erdogan, amehutubia mkutano wa watu zaidi ya milioni moja baada ya jaribio la mapinduzi kushindwa mwezi uliopita.
    viongozi wawili wa upinzani pamoja na mkuu wa majeshi waliungana katika mkutano huo kama ishara ya umoja.
    Rais Erdogan amewaambia watu mjini Istanbul kuwa atapitisha sheria ya kifo kama italetwa tena na bunge la nchi hiyo.
    Ujerumani imetoa onyo kwa Uturuki kama itapitisha sheria hiyo basi matumani ya yake ya kujiunga na umoja wa ulaya yataisha.
    Jeshi tiifu kwa Rais Erdogan lilifanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi mwezi mmoja uliopita Rais Erdogan amesema nchi hiyo itaondokana na wafuasi wote wa mhubiri wa kimarekani Fethullah Gulen, mhubiri huyo amekataa kuhusika na jaribio la mapinduzi.

    Chanzo BBC

    Kiama cha wauza ‘unga’ nchini chawadia

    By: Unknown On: 22:21
  • Share The Gag

  • Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba


    WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametoa siku 14 kwa maofisa wanaohusika na udhibiti wa dawa za kulevya kwenye mpaka wa Tunduma mkoa wa Songwe, kuwakamata watu wanaohusika na uvushaji wa dawa hizo kutoka nchini kwenda nchi jirani ya Zambia na nyingine zilizopo ukanda huo.
    Nchemba alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kukagua mpaka huo, ambapo alisema ni jambo lisilofichika kuwa kwa sasa Tanzania imechafuka kutokana na dawa za kulevya.
    Alisema kutokana na Watanzania wengi kukamatwa katika nchi mbalimbali duniani, wakijihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya, imefikia hatua kwa baadhi ya nchi kufikiria kuongeza masharti zaidi kwa kila atakayejitambulisha kuwa Mtanzania.
    “Hatuwezi kuacha nchi ikachafuka kwa sababu tu ya watu wachache.Ukienda China Watanzania zaidi ya 200 wanashikiliwa kwa dawa za kulevya, Pakistan wapo, India, Afrika Kusini ni Watanzania. Hili linatuchafua sana,” alisema Nchemba.
    Aliutaja mpaka wa Tunduma kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa kupitisha dawa hizo na kutaka nguvu kuongezwa zaidi ili kuwezesha misako.
    Alisema wapo watu ambao si makondakta wa mabasi wala abiria, lakini wamekuwa wakisafiri kila siku kwenye mabasi, hatua inayodhihirisha kuwa ndiyo wanaojihusisha na usafirishaji wa bidhaa hizo haramu.
    Alisema watu hao wamekuwa na ushirikiano na watu wengine katika miji ya jirani, kabla ya kufika mpakani ikiwemo kijiji cha Mpemba wilayani Momba mkoani Songwe, ambapo wakifika hapo basi husimamishwa na mzigo kushushwa, kisha kusafirishwa kwa njia za panya hadi ng’ambo ya nchi.
    “Wakati ninyi mnafanya utaratibu wa kawaida wa kupitisha gari husika hapa mpakani, wao wanavusha kupitia njia za panya. Basi likishavuka na mzigo unakuwa umefika Zambia wanakutana na kuupakia tena kisha wanaendelea na safari. “Na katika hili ni lazima mzungumze pia na wenzenu wa upande wa pili, wadhibiti pia mji unaofuata baada ya huo wa mpakani maana huko ndiko wanakopakia tena. Kama mtashindwa katika wiki mbili, nitakuja mimi mwenyewe na nitawakamata tu,” alisisitiza.

    Chanzo HabariLeo.

    Polisi wazuia ghafla mkutano wa CHADEMA Chalinze........Mbowe Asema Wapo Tayari Kufa Kwa Kupigania Demokrasia

    By: Unknown On: 22:19
  • Share The Gag

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limefuta mkutano wa hadhara wa Chadema uliopangwa kufanyika katika Uwanja wa Miembe Saba mjini Chalinze.
    Mkutano huo uliokuwa ufanyike jana, ulikuwa uhutubiwe na Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati ya Chadema, Frederick Sumaye.
     
    Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Pwani Baraka Mwago alisema jana kuwa alishangazwa na hatua hiyo ya ghafla ya polisi kwa kuwa mkutano huo ulifuata taratibu zote na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chalinze, aliruhusu kufanyika kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 12.00 jioni.
     
    Alisema wakati maandalizi yote yakiwa tayari, ilipotimia saa nane mchana waliitwa polisi na kuelezwa kuwa mkutano huo umezuia kwa maelezo kuwa intelijensia ya polisi imeonyesha kuwa ungehudhuriwa na viongozi wengi wa kitaifa, hivyo polisi Chalinze haijajipanga kutoa ulinzi kwa viongozi hao.
     
    “Hii sababu imetushangaza kwa sababu kiongozi wa kitaifa ambaye angehudhuria ni Sumaye peke yake."
     
    Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema kipengele cha 7.5.3 (f) inamtambua mjumbe wa kamati kuu au baraza kuu anayeishi katika mkoa kuwa ni mjumbe wa baraza la mkoa husika.
     
    “Kutokana na kipengele hicho, Sumaye ana sifa za kuhudhuria mkutano huu kwa sababu anaishi Kiluvya wilayani Kisarawe,” alisema Mwagu.
     
    Alisema lengo la mkutano huo, lilikuwa ni kuutambulisha uongozi mpya wa Chadema kwa wananchi baada ya kufanyika uchaguzi mdogo Juni 4, mwaka huu wilayani Mkuranga.
     
    Katibu wa Chadema mkoani humo, Halfani Milambo alisema waliandika barua kuwataarifu polisi na likakubali, lakini walishangazwa kuzuiwa baada ya kufika katika Uwanja wa Miembe Saba walikotakiwa kufanya mkutano.
     
    “Tuliwaandikia barua tarehe Agosti 4 na siku iliyofuata Agosti 5 tulikubaliwa na Mkuu wa Polisi Chalinze (OCD), SSP J. Magomi kufanya mkutano kwa masharti,” alisema.
    Alitaja masharti ambayo jeshi hilo liliwapa kuwa ni pamoja na kutokuwapo kwa maandamano ya bodaboda, ya miguu au magari, kutokukashifu chama au utawala wa kiongozi yeyote na kuzingatia muda wa kuanza na kumaliza mkutano.
     
    Alisema kuwa cha kushangaza jana baada ya kukamilisha maandalizi yote ikiwamo kufanya matangazo na kufunga vyombo vya muziki, baadhi ya viongozi waliitwa kwenye Ofisi ya Polisi Wilaya ya Chalinze na kuambiwa wasifanye mkutano huo.
     
    Alisema walielezwa kuwa ujumbe ambao unaenea kwenye mtandao unasema mkutano huo utaleta watu wengi sana, hivyo usalama utakuwa mdogo.
     
    Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Boniventura Mushongi alisema lengo la Polisi si kuwakataza kufanya mkutano, lakini kilichoonekana ni kuwa walikiuka maelekezo kwani awali walipaswa kufanya mkutano wa ndani na si wa nje.
     
    “Sisi hatuwakatazi kufanya mikutano yao, lakini ni vema wafuate makubaliano, maana sisi Jeshi la Polisi tuliwaruhusu wafanye mkutano wa ndani lakini tulishangazwa kuona wanaanza kufanya nje huku wakipiga muziki,” alisema.
     
    Mushongi alisema pia polisi inazuia mikutano yote ambayo haina madiwani wala wabunge katika eneo husika, jambo ambalo halikuwa kwenye maelekezo ya OCD.
     
    “Chadema katika eneo la Chalinze hawana diwani wala mbunge, hivyo wamekosa sifa za kufanya mkutano huu. Kama ni kikao cha ndani hatuna tatizo wafanye hata wakialika watu 200,” alisema Mushongi.
     
    Hata hivyo, Mushongi alisema Chadema Pwani walipopeleka barua ya maombi mkutano huo walipewa masharti hayo.
     
    Mbowe: Tuko tayari kwa lolote 
    Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema yeye na makamanda wake wako tayari kwa lolote kwa ajili ya kutetea misingi thabiti ya utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
     
    Akizungumza  jana, Mbowe alisema hakuna mtu wa kuwafundisha makamanda wa Chadema, hivyo mikutano ya Ukuta itafanyika nchi nzima kuanzia Septemba Mosi.
     
    “Ambao hawako tayari warudi nyuma, hakuna aliyelazimishwa, watuache sisi tutangulie wa kufa wafe na wa kupona wapone. Haiwezekani mtu apuuze sheria, avunje katiba halafu taifa linyamaze,” alisema.
     
    “Sisi tumeamua kuchukua mzigo huo kwa niaba ya wananchi wote. Kama ataua wacha aue tu, kama atatufunga wacha atufunge tu lakini tutakuwa tumeacha legacy (kumbukumbu) duniani,” alisisitiza.
     
    Mbowe alisema sifa ya kiongozi bora anayeheshimu misingi ya kidemokrasia ni kuheshimu utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
     
    Kwa mujibu wa Mbowe, Rais anakiuka Katiba na sheria za nchi zinazoruhusu vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara na hakuna mtu ndani ya CCM anayezungumzia hilo.
     
    Mbowe alisema Rais amejisahau kuwa yeye (Mbowe) ni mwenyekiti wa taifa kama alivyo Rais, hivyo anastahili kuzunguka nchi nzima kujenga uhai wa chama.
     
    “Rais anazunguka kwenye mikoa anavisema vyama vya upinzani na kutoa amri mbalimbali lakini sisi (upinzani) hatuna jukwaa la kujibu au kutoa ufafanuzi. Anasema tusubiri hadi 2020,” alilalamika Mbowe.
     
    “Rais anatoa amri, wakuu wake wa mikoa wanatoa amri, wakuu wa wilaya wanatoa amri, watu wanafukuzwa kazi ovyo. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii,” alisema.
     
    “Wewe unanyanyuka tu na kusema watu wahamie Dodoma kivipi? Issue ya kuhamia Dodoma ni suala la kitaifa siyo mamlaka ya mtu mmoja tu kwa kuwa ni Rais.”

     “Hata Nyerere 1973 alipopitisha hoja ya watu kuhamia Dodoma kilikuwa ni kikao cha NEC ya Tanu. Mpaka leo hakuna sheria ya kuhamia Dodoma na nchi hii inaoongozwa kwa sheria.” 

    Mbowe alisema kwa kutambua kuwa hakuna sheria ya kuhamia Dodoma, ndiyo maana Ilani ya CCM (2015-2020) imeeleza kutengeneza sheria ya kuhamia makao makuu Dodoma.
     
    “Hakuna sheria. Rais hawezi kuamua matakwa yake binafsi yakawa ni sheria ya nchi. Alipaswa apeleke muswada wa sheria bungeni na ipitishwe na Bunge siyo kauli ya mtu mmoja,” alisisitiza Mbowe.
     
    Lissu: Tutafuata sheria 
    Wakati huohuo, mwanasheria Mkuu wa Chadema na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema katika utekelezaji wa Ukuta watafuata sheria kwa kupeleka barua za taarifa ya mikutano kwa wakuu wa polisi nchi nzima saa 48, kabla ya kuanza mikutano hiyo Septemba Mosi mwaka huu.
     
    Akizungumza juzi katika mahojiano na Redio ya Sauti ya Ujerumani (DW), Lissu alisema mikutano hiyo itafanywa kwa kufuata sheria na taratibu ikiwamo kutoa taarifa kwa wakuu wa polisi wa wilaya.
     
    Lissu ambaye aliachiwa na mahakama juzi kwa dhamana, alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kwanini chama chake kisitafute njia mbadala ya operesheni Ukuta ambayo Serikali imesema itakabiliana nayo kwa njia yoyote ile.
     
    “Tumesema hatutafanya mkutano wowote usiokuwa na taarifa.Tutapeleka taarifa kwa wakuu wa polisi wilaya wote Tanzania nzima kama inavyotakiwa. Sasa hiyo hatuvunji sheria, tunatekeleza sheria,” alisema Lissu.
     
    Mbunge huyo, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi na kuidharau mahakama, alibainisha kuwa mikutano ya hadhara kuanzia Septemba Mosi, itafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi kama Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa inavyoeleza.
     
    Alisema sheria inasema chama cha siasa ambacho kimeandikishwa kikitaka kufanya mkutano wowote wa hadhara wa siasa, kinatakiwa kupeleka barua ya taarifa kwa mkuu wa polisi wa wilaya saa 48 kabla ya mkutano huo.
     
    “Sheria inasema huyo ambaye tunampelekea taarifa atupe ulinzi kwenye mikutano yetu. Ndicho tunachotaka,” alisema Lissu.
     
    Alipoulizwa kama ni sawa iwapo polisi ikisema haiwezi kuwapa ulinzi na wasifanye mkutano katika eneo husika kwa wakati huo, Lissu alijibu, “(OCD) Ana uwezo wa kutuambia msifanye leo, msifanye kwenye eneo hili au msifanye saa hii, lakini hana uwezo wa kukataa katakata.” 

    Mbunge huyo alisema kilichotokea nchini na kinachofanyika sasa si mikutano kudhibitiwa bali inakatazwa.
     
    “Hakuna sheria inayokataza au inayowapa mamlaka ya kukataza mikutano moja kwa moja kama hakuna tangazo la hali ya hatari,” alisema Lissu.
     
    Alisema kama Magufuli hataki mikutano atangazie dunia kwamba Tanzania ina hali ya hatari.
     
    “Akitangaza hali ya hatari tutamwelewa na wengine tutamuuliza kilichotokea ni kitu gani mpaka kuwe na hali ya hatari,” alisema Lissu.

      

    ==

    Credit; Mpekuzi Blog