Monday, 7 March 2016

Maalim Seif Alazwa Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam

By: Unknown On: 21:26
  • Share The Gag

  • Siku tatu baada ya kutoka India alikokwenda kwa ajili ya kupata matibabu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad jana alilazwa katika hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam.

    Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassoro Mazrui amesema kuwa chanzo cha Maalim Seif kulazwa katika hospitali hiyo jana asubuhi ni uchovu wa safari yake ya India ambayo alienda kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.

    Mazrui alikanusha taarifa zilizokuwa zinaenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kiongozi huyo wa CUF alilazwa kutokana na matatizo ya moyo. Alisema kuwa hakuna kumbukumbu yoyote ya ripoti ya daktari inayoonesha kuwa Maalim Seif ana tatizo la moyo.

    Naibu Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema kuwa kiongozi huyo anaendelea vizuri kiafya na kwamba hayuko katika hali mahututi kama ilivyokuwa ikielezwa.

    “Anakula na kufanya kila kitu mwenyewe na hata jioni hii nimeongea naye, anakula kila kitu, hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya afya ya Maalim Seif,” alisema Mazrui.

    Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa waliwasili katika hospitali hiyo kumjulia hali akiwemo aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
     
    Credit; Mpekuzi blog

    Kampuni ya utalii yamchefua Majaliwa

    By: Unknown On: 21:24
  • Share The Gag
  • KAMPUNI ya uwindaji na utalii wa picha ya Mwiba Holding Limited imemchefua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutokana na madai ya kunyanyasa Watanzania na kutoa angalizo kwamba itafutiwa uwekezaji huo.
    Mwiba Holding Limited inayofanya utalii wa uwindaji na picha katika Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu katika mkoa wa Simiyu, inashutumiwa kwa vitendo vya unyanyasaji wa wananchi wanaozunguka eneo la ranchi walilolitwaa kuendesha shughuli hiyo.
    Mbunge wa Meatu, Salum Khamis, alidai mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa kuwa kampuni hiyo inanyanyasa Watanzania kwa kuwateka, kuwatesa na kwamba imeingia mikataba ya ovyo yenye harufu ya rushwa na vijiji saba katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Makao.
    Wilaya ya Meatu iliyoanzishwa Julai 1, 1987, ina ukubwa wa kilometa za mraba 8,835, na asilimia 49 ya eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori ambazo ni Pori la Akiba la Maswa, sehemu ya Hifadhi ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na WMA. Kutokana na madai hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Eraston Mbwilo, kuchunguza madai hayo na ifikapo Ijumaa wiki hii, awe amempa ripoti.
    “Leo (juzi) ni tarehe tano… Hadi tarehe kumi na moja nipate ripoti. Ikibidi waondoe, siyo lazima abaki yeye. Mwekezaji lazima afuate masharti, kama sivyo afutwe aondoke. Huo mwiba utamchoma mwenyewe,” aliongeza Waziri Mkuu huku akishangiliwa na wananchi wa Meatu.
    Katika maelezo yake baadaye kwa gazeti hili, Mbunge Salum alidai kuwa Mwiba Holding Limited na kampuni dada ya TGT imemilikishwa hekta 12,000 katika kijiji cha Makao kwa ushirikiano na Halmashauri, na kupewa ranchi ambayo ilikuwa inategemewa na wananchi kwa kilimo na mifugo.
    Aidha, alisema vijiji vya Mwangudo, Irambandogo, Sungu, Mbushi, Lukale na Sapa vimejumuishwa katika WMA na wawekezaji hao kuchukua hekta 29,000 na kuingia mkataba mwingine na kijiji cha Mwangudo na kupewa hekta nyingine 79,000.
    Alidai kuwa wawekezaji hao wanatumia askari wao wanaolipwa mishahara, na kwamba katika mikataba hiyo, Halmashauri inalipwa Sh milioni 40 kwa mwaka na kijiji cha Makao Sh milioni 24, fedha alizoeleza kuwa ni ndogo kulinganisha na mapato ya Mwiba inayomiliki hoteli ya nyota tano katika eneo hilo.
    Alivitaja vitendo vya unyanyasaji vinavyofanyika kuwa ni pamoja na mifugo kufukuzwa kwa kutumia helikopta na kuingizwa makorongoni pamoja na askari wake kuwafuata wananchi umbali wa kilometa 50 na kuwatesa.
    Akizungumzia tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga alisema kwa kuwa Waziri Mkuu amemwagiza Mkuu wa Mkoa kufanya uchunguzi, ni vyema wao wakasubiri uchunguzi huo na kama kutakuwa na jukumu linalowataka kulifanya, watafanya hivyo.

    Chanzo HabariLeo.

    Thursday, 3 March 2016

    Trump akabiliwa mdahalo wa Republican

    By: Unknown On: 22:38
  • Share The Gag
  • Wagombea wakuu Republican sasa wamebaki wanne
    Mgombea urais Donald Trump ameshambuliwa sana na wagombea wenzake katika mdahalo wa chama cha Republican, muda mfupi baada ya wanasiasa wakongwe wa chama hicho kuwahimiza wapiga kura wasimuunge mkono.
    Bw Trump, anayeongoza kwenye kura za maoni kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea wa urais wa chama cha Republican, amelazimika kujitetea vikali dhidi ya shutuma kutoka kwa Marco Rubio na Ted Cruz.
    Katika mdahalo huo uliofanyika Detroit, Bw Trump amekiri kwamba amebadilisha msimamo wake mkali lakini akasema kwamba kuweza kubadilika ni nguvu na si udhaifu.
    Baadhi ya wanachama wakuu wa Republican wanasema Bw Trump hafai na kwamba hawezi kushinda urais dhidi ya chama cha Democratic.
    Mdahalo huo ulioandaliwa na kituo cha Fox News ulianza kwa Bw Trump kuulizwa kuhusu shutuma za awali kutoka kwa Mitt Romney, aliyewania urais 2012, aliyesema mfanyabiashara huyo ni mchokozi, mlafi na aliyejaa chuki.
    Trump na Mitt Romney awali Bw Trump amempuuzilia mbali Romney na kumtaja kuwa “mgombea aliyefeli”. Lakini mara moja alijipata akishambuliwa na Bw Rubio.
    Seneta huyo wa Florida alisema hatasalimisha vuguvugu la wahafidhina kwa mtu anayedhani “nuclear triad” (mkusanyiko wa silaha za nyuklia) ni bendi ya rock kutoka miaka ya 1980.
    Miongoni mwa mengine:
    • Bw Trump ameahidi kurejesha viwanda vyake vya kutengeneza nguo kutoka Marekani hadi Uchina.
    • Seneta wa Texas Bw Cruz amesema Bw Trump ni sehemu ya mfumo fisadi wa Washington, uliofadhili kampeni ya Hillary Clinton 2008
    • Gavana wa Ohio John Kasich amesema yeye ndiye “mtu aliyekomaa” jukwaani aliye na nafasi bora zaidi dhidi ya mgombea wa Democratic Hillary Clinton
    • Akitumia michoro mikubwa kwenye skrini, mtangazaji wa Fox Chris Wallace amemuuliza Bw Trump kuhusu ukweli wa mpango wake wa akiba
    • Bw Trump ametetea mbinu ya kutumia maji kupata habari kutoka kwa “wanyama walio Mashariki ya Kati” na kuuawa kwa familia za magaidi
    • Lakini amekataa pendekezo la kuruhusu New York Times waachilie huru kanda za sauti yake zilizonaswa bila yeye kujua.
    Katika moja ya matukio ya kushangaza, Bw Trump ametetea ukubwa wa mikono yake kisha akafanya mzaha kuhusu kiungo kingine chake.
    Amewatusi pia wenzake, akimweleza Rubio kama mtu mdogo” na Ted kama “muongo”.
    Mfanyabiashara huyo kutoka New York amelazimika kufafanua kuhusu kesi ya kusambaratika kwa chuo kikuu chake cha Trump University.
    Amesema atashinda kesi hiyo lakini Bw Rubio amesema mfanyabiashara huyo anajaribu kuhadaa watu wampigie kura, sawa na alivyowahadaa wamkabidhi pesa zao.
    Bw Trump pia ameulizwa na jopo la Fox News kuhusu kubadilika kwa msimamo wake kuhusu wahamiaji wa Syria, vita Afghanistan na Rais George W Bush.
    Amejibu: "Mimi ni mtu thabiti sana. Lakini sijawahi kumuona mtu aliyefanikiwa ambaye hakubadili msimamo wak wakati mwingine.”
    Bw Trump, ameshinda majimbo 10 kati ya 15 yaliyofanya mchujo chama cha Republican.
    Wagombea wakuu sasa wamesalia wane baada ya Ben Carson kujitoa.
    Awali walikuwa 17.
    Mdahalo huo, wa Fox News, ulikuwa wa kwanza kwa Trump kukabiliana moja kwa moja wa wapinzani wake tangu ashinde majimbo saba Jumanne Kuu.
    Aidha, ulimkutanisha na mtangazaji Megyn Kelly, ambaye alishutumu sana mdahalo wa kwanza na baadaye akasusia mdahalo kwa sababu yake.
    Katika chama cha Democratic, Hillary Clinton ameshinda majimbo 10 naye Bernie Sanders majimbo matano.
    Wawili hao watakutana katika mdahalo Flint, Michigan, mnamo Jumapili.

    Chanzo BBC Swahili.

    Alichofanya Nay ni Kama Kichekesho Kwangu-Shetta

    By: Unknown On: 21:57
  • Share The Gag
  • Msanii Sheta alimaarufu kama Baba Kayla amefunguka na kusema alichokifanya Nay wa Mitego kwenye wimbo wa ‘Shika Adabu yako’ ni kama kichekesho kwake.
    Shetta amesema hayo kupitia kipindi cha Planet Bongo cha East Africa Radio na kusema yeye na Nay ni washikaji tu na wanaongea wote na kudai kuwa alikuwa anatambua hilo toka hata wimbo huo haujatoka.
    shetta23
    “Hiyo kwangu ni kama kichekesho sababu huyo Nay wa Mitego mwenyewe anajua alichofanya ni kama kichekesho kwangu siyo issue ya kufanya mimi nikachukulia kama tatizo sababu ukweli wote hata yeye anajua, sisi ni kama familia ndiyo maana unaona mimi nimepost video yake kwangu ku support, ni vizuri alivyosema usikute hata yeye hajui story ya gari yangu, This is my car ndiyo maana yeye kasema hajui labda muulize Shetta sababu yeye hajui” Alisema Shetta
    Lakini mbali na hilo Shetta amesema yeye mbali na muziki ni mfanyabiashara hivyo anapata maendeleo na pesa za kutosha ndio maana anaweza kumiliki gari kama hiyo.
    “Mimi nafanya mitikasi yangu, mfanyabiashara na mwanamuziki hivyo napiga show za kutosha na bado na hustle sana hivyo na kila sababu ya kupata maendeleo na maendeleo ndiyo haya sasa, hivyo sioni kama ni tatizo na wala sioni kama amenisema kwani nilikuwa najua toka before lakini pia mimi ndie mwenye mamlaka ya kila mtu na hakuna mtu mwingine mwenye mamlaka ya gari langu sababu kila kitu ninacho mimi” Alimalizia Shetta.
    Eatv.tv

    Paul Makonda Amkataa Hakimu Anayesikiliza Kesi ya Kuwakashfu Makada Wenzake wa CCM.....Kubenea Naye Akutwa na Kesi Ya Kujibu Sakala la Kumtusi Makonda

    By: Unknown On: 21:50
  • Share The Gag

  • Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda jana alitinga mahakamani na kumkataa hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi iliyofunguliwa dhidi yake na makada wawili wa zamani wa CCM wanaodai aliwakashifu.

    Kesi dhidi ya Makonda, ambayo awali ilikuwa inasikilizwa na Hakimu Hellen Liwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilishafikia hatua ya utetezi na Makonda alitakiwa kuanza kujitetea jana, baada ya mahakama hiyo kumuona kuwa ana kesi ya kujibu.

    Hata hivyo, jana Makonda ambaye alifika mahakamani kwa mara ya kwanza tangu kesi hiyo ilipofunguliwa, alishikilia msimamo wa kutokuwa na imani na hakimu huyo na hivyo kuomba apangiwe hakimu mwingine.

    Makonda alifikia msimamo huo kutokana na maneno aliyoelezwa na wakili wake, ambayo kwa mtazamo yalionyesha kuwa hakimu atakuwa anawapendelea wadai na hivyo asingemtendea haki.

    Kutokana na madai ya Makonda, Hakimu Liwa amejitoa kwenye kesi hiyo na amepanga ianze kusikiliza upande wa mashtaka Machi 23.
    Kesi dhidi ya Kubenea 
    Wakati Makonda akimkataa hakimu, mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea ameonekana ana kesi ya kujibu katika kesi inayomkabili ya tuhuma za kumtukana mkuu huyo wa wilaya. 
    Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anayesikiliza kesi hiyo, ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake.

    Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Simba alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa na mashahidi watatu, aliridhika kuwa mshtakiwa ana kesi ya kujibu.

    Baada ya uamuzi huo wakili wa Kubenea, Peter Kibatala aliieleza mahakama kuwa mteja wake atajitetea kwa kiapo na kwamba watakuwa na mashahidi wanne na wanakusudia kuwaita wote mahakamani siku ya kujitetea.

    Hakimu Simba alipanga mshtakiwa huyo aanze kujitetea Machi 7, mwaka huu.

    Kubenea, ambaye alipandishwa kizimbani, mahakamani hapo Desemba 15, mwaka jana, anadaiwa kumtolea DC huyo lugha ya matusi Desemba 14 mwaka jana wakati wakiwa kiwanda cha Tooku Garments kilichoko Mabibo External, Kinondoni, jambo ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

    Anadaiwa kuwa siku hiyo alimuita Makonda kuwa ni “kibaka, mpumbavu na mjinga” na kwamba cheo chenyewe cha ukuu wa wilaya ni cha kupewa.

    Wakati wa ushahidi wake, Makonda aliieleza mahakama kuwa alitumia nafasi yake ya ukuu wa wilaya kwenda kiwandani kwa lengo la kuzungumza na wafanyakazi waliokuwa wamegoma.

    Mashahidi wengine wa upande wa mashtaka walikuwa ni maofisa wa polisi waliokuwapo eneo la tukio siku hiyo.

    Alisema alipomaliza kuzungumza na wafanyakazi hao na kufunga kikao hicho, wakati anageuka alishangaa kumsikia mshtakiwa akimtukana. 
     
    Credit; Mpekuzi blog

    Madaktari 2 na Wauguzi 4 Wasimamishwa kazi Jijini Mwanza Kwa Kukataa Kumzalisha Mjamzito Ambaye Alijifungua Mapacha Wawili Chooni Wakafariki

    By: Unknown On: 21:47
  • Share The Gag

  • Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Baraka Konisaga, amemwamuru Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Adam Mgoyi kuwasimamisha kazi madaktari wawili na wauguzi wanne katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana iliyopo Kata ya Butimba kwa kushindwa kumuhudumia mama mjamzito aliyefikishwa hospitalini hapo na kusababisha kujifungua watoto mapacha na baadaye kufariki.

    Hatua hiyo imesababishwa na tukio la mgonjwa Suzana John (27) mkazi wa Kata ya Mkolani kufikishwa na ndugu zake katika Hospitali hiyo, aliyekuwa mjamzito na kupokelewa na Dk Norin Magesa na Muuguzi, Janet Foya waliokuwa zamu ya usiku siku ya Machi Mosi, mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku na kushindwa kumuhudumia zaidi ya kutoa lugha isiyoridhisha, pamoja na uzembe.
    Akielezea tukio hilo, mwanamke huyo ( Suzan John ) alidai kuwa alianza kusikia uchungu na kuomba msaada kutoka kwa madaktari na wahudumu wa afya waliokuwa hospitalini hapo bila mafanikio.
     
    “Nilifika nikiwa hoi, nikawaambia muda wangu tayari  lakini hawakunisaidia zaidi ya kunitolea maneno machafu.
    "Wakati muda ukizidi  kwenda huku nikiwa sipewi huduma yoyote, nilihisi kubanwa haja ndogo hivyo nikaamua kwenda chooni .
    Kule chooni mambo yakabadilika ghafla, mtoto wa kwanza akawa keshaanza kutoka.Bahati nzuri mle chooni kulikuwa na beseni
    "Nililichukua lile beseni kwa ajili ya kuwaweka watoto huku niwakaita manesi.Manesi hao walikuja wakanichungulia halafu wakarudi. Akaja Nesi mmoja mwanafunzi, akakata kitovu akawaweka kwenye nguo, wakawa wamefariki,” Bi. Suzan alieleza kwa uchungu huku akilia.
    Baada  ya mapacha hao kufariki, ndugu wa mwanamke huyo pamoja na wagonjwa wengine walioshuhudia mkasa huo walipandwa na hasira huku wakitaka kuwapiga wauguzi hao.
    Taarifa za vurugu hizo zilimfikia DC Konisaga ambaye alifika hospitalini hapo  na kukutana kwa dharula na Mkurugenzi wa Jiji, Adamu Mgoyi, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nyamagana, Kaimu Mganga Mkuu Mkoa, Uongozi wa Hospitali na baadhi ya ndugu wa mgonjwa Suzana John aliyejifungua watoto mapach.

    Katika kikao hicho cha dharura, walipokea maelezo ya pande mbili, kutoka kwa wauguzi na familia ya mgonjwa Suzana, na kupitia taarifa zilizokuwa zimeandikwa na Madaktari wawili waliomuona mgonjwa huyo, ndipo DC Konisaga akamuagiza Mkurugenzi Mgoyi na Kaimu Mganga Mkuu kuwasimamisha kazi madaktari wawili na wauguzi wanne ili kupisha uchunguzi wa kitaalamu juu ya tukio hilo.

    Konisaga aliwataja wanaotakiwa kusimamishwa kazi kuwa ni Dk Magesa na muuguzi Foya waliompokea mgonjwa wakiwa zamu ya usiku wa Machi Mosi, mwaka huu na kushindwa kumpatia huduma zaidi ya kumtolea lugha chafu na uzembe huku wakishindwa kutoa maelezo wakati wa kukabidhi majukumu kwa madaktari na wauguzi walioingia zamu ya asubuhi ya Machi 2, mwaka huu.

    DC Konisaga pia alieleza kuwa pamoja na kuingia kwa madaktari na wauguzi wa zamu ya asubuhi ya Machi 2, bado hawakumjali na kumhudumia mgonjwa huyo huku baadhi wakitoa lugha zisizo za faraja kwa ndugu wa mgonjwa. 
    Hata alipozidiwa na kupewa taarifa na ndugu wa mgonjwa huyo, hawakufika na mara kadhaa walikuwa wakifika na kutoka bila kumudumia pamoja na kumsikiliza akilalamika.

    Aliwataja wengine wanaotakiwa kusimamishwa kazi mara moja ni Dk Emiliana Mvungi, wauguzi ni Maria Mkankule, Suzana Sindano na Bibiana Moshi ambao walikuwa zamu na kutomhudumia mgonjwa ambaye alijifungua katika mazingira hatarishi akiwa Hospitalini hapo.

    Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo amemwagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Rweyendela Onesmo ambaye ni Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Sekou -Toure kupewa maelezo ya kina kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Nangi William na Mganga Mkuu wa Jiji, Dk John Andrew juu ya kushindwa kuchukua hatua pamoja na kupewa taarifa hizo.

    Mulongo pia amemuagiza Dk Onesmo kuunda tume ya uchunguzi itakayoshughulikia suala la tukio hilo na kisha kukamilisha kazi hiyo kwa siku moja na kumpatia taarifa ili hatua kali za maadili ya utumishi wa umma zichukue mkondo wake ili pia kuwezesha kusaidia jinsi ya kuboresha utendaji wa kitaalamu na kitabibu katika hospitali hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kutokuwa na huduma nzuri kwa wagonjwa.
     
    Credit; Mpekuzi blog

    Rais Magufuli Awaongoza Wakuu Wa Nchi Za Jumuiya Ya Afrika Mashariki (EAC ) Kushiriki Katika Uzinduzi Wa Barabara Ya Arusha-Holili/Taveta-Voi Km 234.3 Marchi 3,2016

    By: Unknown On: 21:46
  • Share The Gag
  • Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta, wameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili - Taveta - Voi, yenye urefu wa kilometa 234.3 ambayo inaunganisha nchi za Tanzania na Kenya.

    Hafla ya uwekaji wa jiwe hilo la Msingi imefanyika jana  katika eneo la Tengeru Mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Makamu wa pili wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Dkt. Joseph Butore, Mwakilishi wa Rais Paul Kagame wa Jamhuri ya Rwanda ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Rwanda Mheshimiwa Valentine Rwabiza na Makamu wa Pili wa Rais Sudan Kusini Mheshimiwa James Wan Iga.

    Uzinduzi huo pia umehudhuriwa  na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.

    Kwa upande wa Tanzania ujenzi wa barabara hiyo unatakelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Arusha hadi Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1, na ujenzi wa barabara ya mzunguko yaani "Bypass" yenye urefu wa kilometa 42.4. 
    Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru hadi Usa River yenye urefu wa kilometa 8.2 na Kutoka Usa River hadi Holili mpakani mwa Kenya na Tanzania yenye urefu wa kilometa 100.2

    Gharama za upanuzi wa barabara ya Arusha - Tengeru na barabara ya kuzunguka nje ya jiji la Arusha kwa upande wa Tanzania ni shilingi bilioni 209.6, ambapo kati ya fedha hizo Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) itatoa mkopo wa shilingi bilioni 190.2 na serikali ya Tanzania itatoa shilingi Bilioni 19.4.

    Aidha Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo kwenye mazungumzo na serikali ya Japan ili kupata mkopo wa ujenzi wa awamu ya pili inayoanzia Tengeru hadi Holili.

    Kwa upande wa Kenya, mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara mpya kwa sehemu ya Taveta hadi Mwatate yenye urefu wa kilometa 100. Sehemu ya Mwatate hadi Voi ujenzi wake umekamilika.

    Akizungumza katika hafla hii, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema wananchi wa Afrika Mashari hawapaswi kuwa masikini na kueleza kuwa mradi huo na mingine itakayotekelezwa chini ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itasaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi.

    Kwa upande wao Marais Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya, Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na wawakilishi wa marais wa Burundi, Rwanda, Sudani Kusini wameuelezea mradi huo kuwa ni moja ya miradi muhimu ya kuimarisha uchumi wa jumuiya ya Afrika Mashariki na wametoa wito kwa nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo kushirikiana kukuza biashara baina yake.

    Viongozi hao wote wamekiri kuwa Jumuiya hii yenye watu zaidi ya milioni 160, inayo nafasi ya kupiga hatua kubwa za kiuchumi na kuondokana na umasikini, ikiwa italitumia vizuri soko la pamoja kwa kubadilisha bidhaa kutoka nchi moja hadi nyingine na kujenga viwanda vingi badala ya kuendelea kutegemea bidhaa kutoka nje.

    Gerson Msigwa
    Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
    Arusha
    03 Machi, 2016
    c