Mkazi
mmoja wa Dodoma anayejitangaza kama nabii, Tito Machija amesema watu
wasimuone kuwa hana akili kutokana na mahubiri yake ambayo
yanatofautiana kwa kiasi kikubwa na imani za waumini wa dini nyingine,
hasa Wakristo.
Machija,
ambaye anajulikana kama ‘Nabii Tito’ anahamasisha kuoa mke zaidi ya
mmoja, ikiwa ni pamoja na kutembea na wafanyakazi wa ndani; anatumia
pombe kunasa waumini na anadai hataki nyimbo za injili kwenye ‘ibada’
zake, ambazo nyingi hufanyikia baa.
‘Nabii’
huyo anaonekana kwenye mitandao ya kijamii akiwa amevalia kanzu nyeupe
yenye misalaba miwili, chupa ya bia na kitabu kitakatifu aina ya Biblia.
“Nawashangaa wanaoniona mimi sina akili, niko timamu kabisa na ninaelewa ninachokifanya,” alisema.
“Narudia tena kusisitiza kuwa walevi ndio watakaoingia ‘mbinguni’ na mafundisho ninayoyatoa ni sahihi,”
Tito
amekuwa akionekana kwenye mitandao ya kijamii, hususani kwenye video
fupifupi za Instagram, akiwa amevalia mavazi kama ya kichungaji na
kucheza muziki huku akinywa bia na akiwa ameshika biblia.
‘Nabii’
huyo, mwenye wake watano na watoto 12, amedai kuwa kwa sasa hitaji lake
kubwa ni kumuoa mwigizaji Wema Sepetu ili aungane naye katika huduma
zake.
“Wema
ni msichana mzuri wa sura na umbo nataka nimuoe awe sehemu ya kanisa
langu na nina imani watu wengi wataongezeka kwenye ibada ili kuja
kumuona yeye na wake zangu hawana tatizo na hilo hata mmoja wao
ananisaidia kumshawishi ili tuungane naye,” alisema Tito.
Tito anakiri kuwa ‘kanisa’ lake halijasajiliwa ila anadai kwamba anapata ufadhili kutoka kwa walevi mbalimbali.
Tito
amedai kuwa ‘kanisa’ lake lipo karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma na mara
nyingi ibada zake huwa anazifanya kwenye baa na ana wafuasi wengi
kiasi cha kutojua idadi yao.
Amesema
kabla ya ibada kufanyika kwenye baa husika, huanza kwa kupeleka
vipeperushi kwa mmiliki ili kuwapa taarifa waumini wake siku hasa ya
ibada kufanyika katika baa hiyo.
“Siku
ya ibada ikifika naenda pale nikiwa na bia zangu za (anaitaja aina ya
bia) ambazo nimeshaziombea. Zina ‘upako’. Kila anayetaka kuingia kwenye
ibada analipa kiingilio cha Sh12,500. Ukilipa pesa hiyo unapata bia zako
tano ndiyo huduma inaendelea usipotoa unafukuzwa,” alisema.
Tito
anajinasibu kuwa ana waumini wengi ambao hujitokeza kusikiliza
mafundisho yake ambayo kwa kiasi kikubwa yanahamasisha ulevi na mapenzi
kwa wasichana wa kazi wa majumbani.
Amesema kwenye huduma zake nyimbo za injili hazina nafasi kwa kuwa huwaburudisha waumini wake kwa nyimbo za kisasa.
“Mtu akishaweza safari zake kichwani ukimuwekea bongofleva anacheza na kufurahi huku ibada inaendelea,” alisema.
Nabii huyo amedai kuwa hakuna anachokizungumza kutoka kichwani mwake bali anasimamia mistari ya vitabu vitakatifu.
“Wapo
wengi wanaopinga huduma zangu ila nawaambia sijakurupuka nafanya kitu
ambacho kipo na wala sioni kama ninakosea,” alisema.
Kwanini ‘ibada’ kwenye baa
Tito
amedai kuwa anaingia makubaliano na wenye baa kwa kuwa ndiyo sehemu
ambayo walevi hukutana na kwake ni mahali sahihi pa kutoa huduma.
“Pale
nakwenda na bia zangu kadhaa kwa ajili ya waumini watakaoingia kwenye
‘ibada’. Zikiisha naondoka zangu, nawaacha wanaendelea kununua za baa
hapo ndipo mwenye baa anaponufaika,” alisema.
Watu wengi wamekuwa wakilaumu mafundisho ya Tito kuwa yanapotosha na wameiomba Serikali kuchukua hatua.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment