Mrema wakati akimnadi Magufuli wakati wa kampeni.
MWENYEKITI wa Taifa wa chama cha siasa cha Tanzania Labour (TLP),
Augustine Mrema amesema hakufanya makosa na wala hajutii kumnadi Rais
John Magufuli kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa sababu alitambua
Watanzania wamelamba dume la maendeleo.
Akizungumza na gazeti hili jana mjini Moshi, Mrema alisema Watanzania
wamepata mtu wa kuendeleza kazi aliyokuwa akiifanya kipindi yeye wakati
akiwa Naibu Waziri Mkuu katika miaka ya 1990, ya kupambana na wahujumu
uchumi, wala rushwa na wafanyakazi wazembe.
Mrema alisema Dk Magufuli ndiye mwenye uwezo pekee wa kuyaleta
mabadiliko ya kweli yanayohitajika, japo wengi waliamini hayawezi
kupatikana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio maana alichukua
jukumu la kumpigia kampeni.
Mrema aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo mwaka 2010 hadi mwaka
2015, alisema anamfahamu vizuri Dk Magufuli tangu akiwa Waziri wa
Ujenzi, kutokana na uchapakazi wake, ambapo walisaidiana kujenga
barabara za Vunjo, hali iliyosaidia jimbo hilo kuwa na mtandao mkubwa wa
barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
“Watu walishangaa sana kwa nini nilimpigia kampeni Dk Magufuli, na
kumwacha mgombea wangu…nilijua mtu pekee wa kuyaleta mabadiliko makubwa
na kweli ni yeye… Kwanza nampongeza sana na nafurahi sana kwa taifa hili
linahitaji kiongozi mchapakazi, mwadilifu kama yeye,” alisema Mrema.
Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu, akiwa jimboni Vunjo, Dk
Magufuli alikutana na Mrema wakati huo naye akiomba kura za ubunge, na
alimshika mkono na kumtambulisha akiwa katika moja ya mikutano yake, na
Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alimpigia debe mgombea
huyo wa urais wa CCM.
Mrema alifanya hivyo huku chama chake, TLP kikiwa kimemsimamisha
MacMillian Lyimo kuwania urais wa Tanzania, hali iliyoibua mijadala
wakati huo wa kampeni, huku mwanasiasa huyo machachari nchini akitetea
msimamo wake huo wa kumnadi Dk Magufuli badala ya Lyimo.
Mrema alisema Uchaguzi Mkuu umeibua rais mwema, mwadilifu na mwenye
uchungu na Watanzania wote. Aliwataka Watanzania kuacha ushabiki wa
vyama vyao vya kisiasa na kuangalia mtu anayefanya kazi ya kulikomboa
Taifa hili, kama Dk Magufuli kwa kumuunga mkono na kumuombea.
Alisema tangu Taifa lipate Uhuru, kwa sasa Tanzania imeandika
historia ya kuwa na viongozi mahiri watatu wa kupambana na umaskini,
ambapo aliwataja viongozi hao ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine (sasa hayati) na Dk Magufuli.
Created by Gazeti la HabariLeo.
Tuesday, 1 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

0 comments:
Post a Comment